(Part XIX; Repeal, Savings and Transitional Provisions)

Habari Rafiki, karibu kwenye makala yetu ya leo ambayo tunachambua sheria yetu ya wanyamapori ya mwaka 2009. Naamini kabisa kupitia makala hizi unajifunza mambo mbali mbali kuhusu sekta hii ya wanyamapori na maliasili kwa ujumla. Kumbuka hili siku zote hakuna mwisho wa kujifunza, hivyo tunatakiwa kuwa na bidii kujifunza vitu vipya ambavyo vina mchango kwa jamii na maisha yetu. Maarifa na ufahamu tunaoupata hapa utusaidie kuboresha  maamuzi yetu tunayochukua kwenye matumizi, usimamizi na uhifadhi wa maliasili zetu.

Siku ya leo ndio tunamaliza kabisa uchambuzi wa sheria hii ya Uhifadhi wa  Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, tunachambua Sehemu ya mwisho kabisa sehemu ya Kumi na tisa. Ni sehemu ambayo inahusu mabadiliko na mwisho wa matumizi ya sheria hii ya wanyamapori. Naamini hata kwa vifungu vichache tutakavyovichambua hapa vitaleta maana kwako na kuongeza maarifa kuhusu mambo ya wanyamapori. Kifungu cha mwisho kabisa ni kifungu cha 122 ambacho tutakichambua hapa.

122.-(1) Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori inaweza kubatilishwa au kuisha matumizi yake kwa mujibu wa sheria hii.

(2) Baada ya kuanza kutumika kwa Sheria hii, mtu atakaye hukumiwa kuwa na kosa chini ya sheria ya uhifadhi wa wanyamapori, licha ya mapendekezo na masharti ya sheria nyingine zilizoandikwa atawajibika kisheria kuona kuwa amefanya kosa chini ya sheria inayofanana na kuendana na Sheria hii ya Wanyamapori. Ufafanuzi kwenye kipengele hiki ni kwamba, mtu akifanya kosa atawajibika kisheria kwa kosa lake sawa na makosa mengine yanayofanana na kosa alilofanya yaliyopo kwenye Sheria hii ya wanyamapori au yaliyopo chini ya sheria hii.

(3) Kanuni yoyote, amri, mapendekezo, maelekezo, notisi, tagazo, taarifa au sheria nyingine zilizotungwa na uongozi au utawala, kutolewa au kupewa au kuanza kutumika kabla ya sheria hii au chini ya sheria nyingine yoyote iliyobatilishwa au kubadilishwa kwa maudhui ya sheria hii, kama ilishatungwa, kutolewa au kutekelezwa chini ya masharti yanayofanana na kuendana na Sheria hii, itaendelea kutumika na kuwa na  nguvu kama ilivyotungwa, kutolewa, kuwekwa, kama itakavyokuwa chini ya Sheria hii.

Ufafanuzi kwenye kifungu hiki ni kwamba, endapo kutakuwa na sheria, kanuni au masharti yoyote kwenye uhifadhi wa wanyamapori kabla ya kutumika kwa sheria hii, masharti, kanuni na sheria hizo zitaendelea kutumika na kuwa na nguvu, ikiwa mapendekezo hayo na sheria hizo zimetungwa chini ya sheria hii mama ya wanyamapori, au kanuni hizo ziendane na zisitofautiane na masharti na mapendekezo ya sheria hii ya wanyamapori ya mwaka 2009.

Kufikia hapa nakushukura sana Rafiki na msomaji wa makala hizi wa wanyamapori. Kama nilivyotangulia kusema hapo mwanzo kuwa hii sehemu tuliyoichambua leo ni sehemu ya kumi na tisa ya sheria ya uhifadhi wa wanyamapori Tanzania, hivyo ni sehemu ya mwisho kabisa, kwa sababu sehemu za majedwali ya wanyama nimeshayachambua na kuyaelezea kwa makala zilizopita. Nikutie moyo na kukuhamasisha kwamba uendelee kujifunza mambo haya, kwani kuisha kwa sehemu hii ya uchambuzi maana yake kuna makala nyinine nzuri na bora zaidi zitakuja. Endelea kuwashirikisha wengine maarifa na makala hizi, ili tufanye kazi hii kwa pamoja.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania