Ujenzi wa kitu chochote ulio imara umejengwa kwenye misingi imara iliyojengwa na watu makini na wenye weledi na ufahamu wa kutosha kuhusiana na ujenzi huo. Fundi mzuri akiwa katika kujenga anajua uimara wa jengo lake utadumu kwa muda gani, anajua hata ikija mvua na upepo au vimbuga vya aina gani msingi wa ujenzi wake unaweza kuhimili na kustahimili changamoto yoyote  itakayotokea hapo baadaye. Hapa namaanisha fundi mzuri na makini lazima aone jengo lake likikaa zaidi ya miaka hamsini au mia moja. Hapo hapo ukikutana na fundi mbabaishaji mwenye haraka na mwenye tamaa hawezi kufikiri kwa makini nini kitatokea baada ya miaka ijayo kwenye ujenzi wake.

Kila kitu kwenye maisha kina misngi yake, hakuna kitu ambacho kipokipo tu hakuna, mafanikio yana misingi yake, furaha ina misingi yake, binadamu wana misingi yake , biashara zina misingi yake, wanyama wana misingi yake, hata mahusiano yana misingi yake. Siri ya mafanikio ya kudumu kwenye jambo lolote ipo kwenye misingi. Changamoto na mtafaruku hutokea pale misingi inapoachwa kufuatwa, pale watu wanapoamua kutumia zaidi hisia na ubinafsi kwenye mambo nyeti yanayogusa maisha ya wengi badala ya kufikiri kwa kina na  kufuata misingi ya jambo hilo, kumeishia kuleta matokeo mazuri ya muda mfupi na migogoro ya kudumu, au wakati mwingine migogoro isiyoisha tangu pale wanapoamua kutumia hisia binafsi zisizo na msaada kwa wengine.

Katika sekta ya wanyamapori na sekta ya maliasili kwa ujumla wake kuna misingi na makubaliano hai yaliyopo kwenye maandishi, ingawa jambo au kitu kuwa kwenye maandishi haimaanisha jambo hilo ni sahihi na la haki. Kwa mfano msingi wa Wakoloni waliotutawala siku za nyuma ulikuwa ni msingi wa kinyonyaji, msingi wa uonevu na wa ugandamizaji. Hivyo kwa kila kitu kilichokuwa kinafanyika kwa watawaliwa kilikuwa cha kinyonyaji na kuonewa. Ndio maana baada ya Nchi yetu kupata uhuru kutoka kwa wakoloni wa kizungu kitu cha kwanza kubadilishwa ilikuwa ni misngi au sheria. Kuondoa kabisa kila sheria na misingi yote ya kinyonyaji na ya uonevu katika nchi ya watu huru. Hivyo basi baada ya kupata uhuru misingi ya nchi yetu ikawa ni ya haki, usawa na amani.

Misngi ya nchi yetu iliyojengwa na kuwekwa na watu makini na wenye upeo mkubwa na wasio sukumwa na tamaa wala ubinafsi wowote waliweka misingi mizuri ya kuongoza taifa huru lenye kujali, kuheshimiana na kusaidiana kwa watu wote, walihakikisha kila kinachotishia kuharibu misingi ya nchi hii kinakemewa na kuharibiwa vikali sana, ndio maana hatuna kwenye nchi yetu misngi ya kibaguzi wa kikabila, dini, rangi nk. Taifa lilijengwa kwa misngi ya uzalendo na upendo, na hapo ndipo amani huja na kuwa sehemu yetu. Amani inatengenezwa haiji tu, na gharama yake ni kubwa sana. Asante sana Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa kuongaza kwa vitendo nchi yetu kujengwa kwenye misngi mizuri na imara.

Katika historia inayonyesha sehemu yoyote ile ampapo binadamu anaonewa, ananyanyaswa, au kugandamizwa sehemu hizo hakuna amani kabisa, hata kama kuna maendeleo ya uchumi au kuna utajiri mkubwa kiasi gani. Kama kuna ubaguzi au matabaka ya walio nacho na wasio nacho, kama hakuna usawa kwenye kula keki ya taifa, hiyo sehemu au nchi huwa haikaliki. Roho ya binadamu haijaumbiwa kugandamizwa, kunyanyaswa au kutawaliwa kinyonyaji haijaumbiwa hivyo, imeumbiwa kutawala na kuwa huru. Ndio maana sehemu yoyote ile duniani haki ianapokosekana huwa kelele haziishi, hata kama kuna utawala mkali na wa kidikteta kiasi gani, kama kuna uonevu kwenye maisha ya watu, uzoefu na historia inaonyesha sehemu hizo hazikaliki wala kutawalika mpaka pale haki itakapopatikana. Ninachotaka kusema hapa ni kwamba huwezi kujenga kitu kwenye msingi mbovu usio na haki na wa kinyonyaji ukaendelea kuwa salama, haiwezekani!.

Mahusiano yetu na mamlaka za hifadhi za wanyamapori yanasema mengi ambayo hata nikiyaandika hapa sitayamaliza, mtazamo wa jamii kwenye uhifadhi wa wanyamapori umekuwa na ukakasi, kama sio wa kusadikika. Zipo sababu nyingi zinaweza kuingia katika hali hii, sababu zinaweza kuwa za kihistoria au za kiutendaji. Pia sababu zinaweza kuwa kwa pande zote mbili kushindwa kutimiza wajibu wake sawa sawa. Kwa kuwa suala la uhifadhi wa wanyamapori ni jukumu la kila mtu,  hata matokeo na faida za rasilimali hizi zinatakiwa kuwa za kila mtu, yaani kumnufaisha kila mtu.

Kuna kelele tunazisikia kila pembe ya hifadhi za wanyamapori, wengi wakiwa ni wakulima na wafugaji. Ukienda Kaskazini hadi Kusini, Nyanda za Juu Kusini malizia mpaka Magharibi na Kanda ya Ziwa kelele huwa zinafana sana. Wengi wa watu hawa huwa wanalalamika kuonewa na kunyimwa haki zao, wengi wanalalamika mazao na mifugo yao kuliwa na wanyamapori, mbaya zaidi awea hajalipwa fidia au imecheleeshwa. Tafiti na majarida mengi yameeleza kuwa faida inayotolewa kwa jamii hizi kutokana na uwepo wa wanyamapori karibu na maeneo yao ya kuishi ni ndogo sana kulinganisha na faida inaotokana na mapato yanayopatikana, kwa mfano kuna takwimu zinaonyesha kuwa kiasi cha asilimia 1.8 ndio hupelekwa kwa jamii zilizopo kando kando ya hifadhi kwa ajili ya maendeleo yao.

Unaonaje kiasi hicho kinachotolewa miaka nenda miaka rudi, sijajua kwa sasa kama asilimia ya kiasi hicho imeongezeka. Sikatai kama nchi tunachangamoto na tuna mambo mengi ya kufanya yanayohitaji fedha nyingi. Lakini unaonaje gharama kubwa zinazotumika kwenye vita dhidi ya ujangili, lakini bila kujua kuwa kwa asilimia kubwa sana wanaohusika kwenye ujangili, uwe ni ujangili wa meno ya faru au tembo au ujangili wa kurina asaili au kuvua samaki ndani ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori ni jamii hii iliyopo karibu na maeneo ya hifadhi.

Kama wahifadhi, wataalamu na Serikali tukae chini tupitie misingi ya mahusiano yetu, tujue kitu gani kitasaidia mahusiano yawe mazuri na ya kudumu. Mahusiano mazuri na jamii ni pamoja na kupata taarifa za ujangili na ushirikiano mkubwa kwenye kuhifadhi wanyamapori. Kwenye uhifadhi wa wanyamapori kuna historia ndefu sana yenye mizizi sawa na ujangili, hivyo tunapotaka kuondoa ujangili kwenye hifadhi zetu hatupaswi kufanya maamuzi ya zima moto, au kwa hisia bali kwa ubora na weledi huku misingi na sheria zikifuatwa ipasavyo.

Natambua juhudi za Serikali kwenye uhifadhi wa wanyamapori, natambua juhudi za Mashirika na Mamlaka za Umma na Mashirika Binafsi kwenye uhifadhi wa wanyamapori, ni juhudi kubwa inayopaswa kuungwa mkono. Natoa rai kwa watanzania wenzangu tutambue kuwa suala la uhifadhi wa wanyamapori na malisaili nyingine sio la serikali au mashIrika ya kimataifa pekee, bali ni jukumu la kila mtanzania kwa nafasi yake ana wajibu wa kuhifadhi, kulinda na kufaidika na maliasili za nchi yake. Kama Mwal.Nyerere alivyowahi kusema  uhifadhi wa wanyamapori sio Ssuala kundi fulani tu au serikali pekee, bali ni la dunia nzima. Hivyo fanya sehemu yako Rafiki yangu.

Nakutakia kila la kheri kwenye majukumu na wajibu wako kama mtazania kuhifadhi maliasili zetu popote pale ulipo. Mshirikishe mwenzako makala hii ili na yeye awe balozi mzuri kwenye uhifadhi.

Ahasante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania