Habari msomaji wa Wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo, leo ni siku nyingine bora kabisa tuliyopewa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kufanya mambo bora na mazuri kwenye maisha yetu na maisha ya watu wengine. Katika makala hii nataka nielezee utaratibu mwingine mzuri kwako msomaji wa makala hizi. Kwa kuwa umekuwa rafiki yangu kupitia makala hizi na mimi nataka nikuandalie kilicho bora zaidi kwa ajili yako. Naamini utafurahia utaratibu huu mpya ninaotaka kuanzisha kupitia usomaji na uandishi wa makala hizi. Lengo kubwa likiwa ni kutoa elimu ya uhifadhi wa maliasili zetu na mazingira yetu.

Utaratibu mpya nitakaounzisha ni huu, kila Jumapili nitakua naandika makala nitakazokuwa naziita barua za wazi, au barua za Jumapili kwa watanzania wote. Barua hizi zitakuwa zenye kugusa mambo mbali mbali yanayotokea kwenye mazingira yetu tunayoishi, vitendo na maamuzi mbali mbali vinavyofanyika kwenye mazingira yetu ambavyo vinatishia maliasili na mazingira yetu. Kwa hiyo tutakua tunajifunza mambo mbali mbali mengi yakiwa yanahusiana na uhifadhi wa mazingira, utunzaji wa mazingira na usafi wa mazingira yetu. Lengo kuu la makala au barua hizi za Jumapili ni kutoa elimu ya mazingira na pia kila mtu ajione ana wajibu mkubwa wa kutunza na kuyahifadhi mazingira yake.

Dunia tunayoishi sasa inabadilika kwa kasi mno, kila kitu kinabadilika, kila kukicha utasikia mambo mapya na habari mpya ambazo zinaelezea maendeleo na ukuaji wa teknolojia mbali mbali. Mabadiliko haya yanayotokea katika dunia yetu yana kuwa na mambo mengi mazuri na mengine sio mazuri hasa kwa usalama wa mazingira yetu. Mabadiliko yanayotokea sio ya kiasili bali kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na shughuli za kibinadamu ambazo zinaenda mbali hadi kuharibu mfumo mzima wa asili wa mazingira yetu. Mfano mambo kama ongezeko la watu duniani, ukuaji wa uchumi na njia za kuingizia kipato zimekua zinatishia kwa kiasi kikubwa mazingira asilia ya viumbe hai wengine. Nadhani wengi tunasikia kila kukicha mashirika ya umoja wa mataifa yakipiga kelele kuhusu suala hili la mazingira, umesikia mataifa na nchi zikizozana kuhusu masula haya ya mazingira.

Suala la uhifadhi wa mazingira ni la muhimu sana kuliko kitu kingine chochote, kwa mfano ukiangalia kwenye vitabu vitakatifu binadamu wa kwanza alipoumbwa kazi kubwa ya kwanza aliyopewa ilikuwa ni kuyatunza mazingira. Hata kabla ya mwanadamu kuja duniani Mungu alihakikisha kuwa mazingira yote muhimu yanayofaa kwa kuishi binadamu yanakamilika kabla ya kumleta mwanadamu duniani kuyatawala, kuyalinda na kuyatunza mazingira hayo. Hii inamaanisha kwamba Kama Muumba wetu alituwekea mazingira kabla ya sisi inamaana mazingira ndio yana amua sisi tutaishije hapa duniani, na hapo ni mazingira ya aina zote (mazingira ya kiroho na ya kimwili). Lakini mimi kwenye makala hizi nitazungumzia mazingira ya kimwili yanayotuzungunguka.

Kama nilivyowahi kuandika kwenye makala moja iliyopita kuwa maisha yetu hapa duniani yana muunganiko wa ajabu na mkubwa sana. Maisha hayaongozwi na kitu kimoja tu, maisha sio kufanya kitu kimoja tu, maisha yetu yanagusa vitu vingi sana. Kwa hiyo watu wengi wanaweza wakawa wanafanya vitu lakini hawajui madhara yake kwa vitu vingine. Ninaposema maisha yetu yanamuunganiko wenye kugusa vitu vingi hapa namaanisha hivi, kwa mfano mtu anahitaji chakula anachofanya ni kwenda kutafuta shamba alime, na hapo anapolima atakuta kuna mimea na miti ataamua kukata, kuchoma ili apate mahali pa kulima mazao yake. Lakini pia kumbuka hapo alipoenda kulima kulikuwa na viumbe hai wengine wanategemea eneo hilo alilolima kwa ajili ya maisha yao. Kwa hiyo moja kwa moja atakuwa ameharibu maeneo ya viumbe hai muhimu ambao nao wana manufaa kwa watu hao hao walioharibu maeneo ya viumbe hawa. Kwa hiyo ukiangalia kwa makini mzunguko huo utaona jinsi binadamu anavyojimaliza mwenyewe na kujiwekea mazingira magumu yasiyofaa kuishi.

Kwa hiyo tunapojifunza uhifadhi wa wanyamapori na uhifadhi wa mazingira sio tu kwa ajili ya wanyamapori kuwepo na mazingira kuwepo bali hata sisi kuendelea kuwepo. Kila kitu kinaanza na sisi na kinaishia na sisi. Maamuzi na hatua tunazochukua kila siku kwenye maisha yetu ndio vinaamua ni mazingira gani tunayataka kuishi hapa duniani. Ndio maana suala hili linatakiwa kuwa la kila mtu. Hivi unajua kwanini wazungu wanapenda kuja Afrika hasa Tanzania? Unafikiri wanakuja Tanzania kushangaa maghorofa? Hapana, kama ni maghorofa wanayo kule kwao makubwa na mazuri zaidi ya huku kwetu, wanakuja kushangaa na kuona vitu ambavyo kule kwao havipo. Wakija huku kwetu tena kwa gharama kubwa huwa wanakimbilia kukaa au kwenda maeneo ya asili kama vile kwenye hifadhi za wanyama, misitu ya asili, na sehemu nyingine za asili zinazovutia. Wanakuja kuona vitu ambavyo kule kwao hawana.

Hivyo nikwmbie tu rafiki yangu unayesoma makala hii, maenedeleo ya kweli kiuchumi na kisiasa lazima yaendane na utunzaji na uhifadhi wa mazingira ya asili. Tukishindwa hapo juhudi zote tunazoweka kuimarisha uchumi na siasa hazina faida kama mazingira tunayoyategemea yanaendelea kuharibika. Suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira ni la muhimu kama ilivyo kunywa maji kwa kila mtu. Tuchukue hatua stahiki kwenye mazingira yanayotuzunguka.

Mwisho, kama nilivyokupa utaratibu hapo mwanzo kuhusu uandishi wa makala ambazo nitakuwa naziandika siku ya Jumapili, zote zitakuwa za kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira na zitakuwa ni barua za wazi, au barua za Jumapili kwa watanzania wote. Hivyo usikose fursa hii ya kupata elimu hii muhimu kwa ajili ya kila mtu. Pia makala nyingine zitaendelea kwenda hewani kama kawaida. Mwambie na rafiki yako habari hii njema. Kama utakuwa na maswali, maoni mapendekezo usisite kuwasiliana nami kwa mawasiliano yaliyopo hapa chini ya makala hii.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania