Habari ndugu msomaji wa makala za kila siku kuhusu wanyamapori, karibu kwenye makala ya leo ambayo tunajifunza  na kutafakari kuhusu nafasi zetu kama wanadamu na watanzania katika kutunza na kuhifadhi mazingira yetu. Makala ya leo itakuwa ni kujitafakari na  kujua nafasi zetu kwenye jamii na majukumu yetu hapa duniani. Inaweza ikaonekana ni jambo la kawaida sana kusikia kwenye katiba ya nchi, sheria za nchi na hata kwenye dini zetu kuwa jukumu la kulinda na kuhifadhi wanyamapori wetu ni la kila mtanzania. Mara nyingi sentensi hii huonekana kama ni sentensi ya jumla na haimuhusu mtu, lakini leo nataka tufikiri mara mbili kwenye jambo hili.

Nchi ya Tanzania imezungukwa na kila kitu chenye uzuri wa asili, kuna mbuga za wanyama, kuna mito, kuna rasilimali nyingi sana zilizopo katika ardhi hii ya Tanzania. Ambazo nyingine zinateketea, na  watu bila kujua wanaziharibu kwa kujua zipo nyingi. Tuna weka thamani ndogo sana kwenye vitu vizuri ambavyo Mungu ameviweka kwenye nchi yetu, kuna rasilimali nyingi sana ambazo zipo na zinapatikana katika nchi yetu pekee na sio sehemu nyingine duniani.

Kwa asili watanzania ni waongeaji sana, ni watu wanaopenda kusifia na kukuza vitu vya watu wengine ambavyo havina msaada kwetu. Watu wanasifia sana na kujadili mambo ambayo hayapo kwenye msingi wa maisha yao. Kwa hili watanzania tujichunguze. Sikatai kusifia vitu vingine au mambo ya watu wengine ila kumbuka wewe ni mtanzania na una wajibu wa kuitangaza nchi yako na rasilimali zake.

Suala jingine ni kutofuatilia na kutotilia manani mambo yanavyokwenda kwenye sekta hii muhimu ya wanyamapori na maliasili kwa ujumla. Tumekuwa tunasikia tu matukio mbali mbali ya uhribifu na ubadhirifu na kuyatilia manani. Badala ya kuwa wazalendo wa kweli na kwenye maliasili zetu. Hivyo basi kwa kuwa sheria na katiba ya nchi inasema kila mtanzania ana haki ya kunufaika na rasilimali za nchi yake. Pia ana wajibu wa kutunza na kuhifadhi rasilimali hizo zilizopo kwenye nchi yake.

Hivyo popote pale ulipo tambua una wajibu, na kama umepata nafasi ya kuishi Tanzania unawajibu wa kulinda na kuhifadhi maliasili hizi, uhifadhi na utunzaji wa mazingira ninaomaanisha hapa sio kwenda hifadhini bali ni kufanya kila kitu kwa manufa mapana ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho, kwa mfano unaweza kupanda miti, unaweza kutunza mazingira yanayokuzunguka, unaweza kuelimisha familia na jamii yako kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na usafi wa mazingira, unaweza kuzuia na kuacha kabisa vitendo vya uchomaji mioto kwenye vyanzo au kwenye maeneo ya hifadhi ya wanyamapori. Popote pale ulipo unaweza kufanya jamobo kama hili ili kuokoa na kunusuru mazingira yetu na wanyama wetu.

Tuna mengi ya kujifunza kwa kadri siku zinavyokwenda, ila leo mimi nakundikia na kukwambia wewe ni muhifadhi hapo ulipo. Hivyo tumia nafasi yako kulinda na kuhifadhi mazingira yako kwa faida yako na jamii yako, kwa vizazi vya sasa na vya baadae.

Ahasante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania