Habari za siku kidogo ndugu msomaji wa makala za wanyamapori. Ni matumaini yangu ubukheri wa afya na unaendelea na majukumu ya ujenzi wa taifa kama kawaida. Nimekuwa kimya kidogo kutokana na shughuli nyingine lakini napo pata nafasi kama hivi basi sinabudi kukuandikia makala ya wanyamapori ili uendelee kuburudika na kutambua mengi sana dhidi ya maliasili tulizo jaaliwa na Mwenyezi Mungu. Ukweli ni kwamba kila kitu ambacho kimeumbwa na Mwenyezi Mungu basi ujue kina makusudi yake ya kuwepo hapa duniani na si vinginevyo. Hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha kitu hicho kinaendelea kuwepo tena kwa ubora zaidi ili kije kukutwa na vizazi vijavyo.

Leo darasani kwetu tutamjua mnyama mwenye rangi ya kuvutia sana na hata kwa kumuangalia tu nadhani utafurahi. Ni mnyama ambae anapatikana maeneo mengi au niseme nchi nyingi hapa barani Afrika japo kuna baadhi ya nchi tayari mnyama huyu kasha toweka na haonekani kabisa. Kwa nchi nyingine mnyama huyu alikuwa akionekana katika maeneo mbali mbali lakini kwa sasa kuna baadhi ya maeneo hayupo tena katika nchi hiyo hiyo. Sasa kujua yote haya nakusihi uwe na mimi mwanzo hadi mwisho wa makalahii.

Darasani kwetu leo tutamzungumzia mnyama ajulikanae kwa jina la “NZOHE”. Kabla sijaendelea napenda tu ndugu msomaji ujue kuwa na huyu Nzohe ni mnyama jamii ya “Swala”

SIFA NA TABIA ZA NZOHE

Nzohe wana sura nyembamba zilizo chongoka kidigo mfano wa digi digi huku mashingo yao pia yakiwa marefu na membamba kidogo.

Wana miguu myembamba na miguu ya nyuma ni mirefu kidogo kuliko miguu ya mbele. Miguu hii ya nyuma kuwa mirefu ndio huwafanya Nzohe kuonekana na umbo la kubinuka kidogo pindi unapo muangalia akiwa amesimama.

Nzohe ukiwachunguza vizuri huwa wana rangi tofauti tofauti kidogo lakini kiujumla ni kwamba, dume huwa na rangi ya majivu ambayo inaelekea kuwa kama kahawia, jike na nzohe wadogo ambao wanaendelea kukuwa  huwa na rangi mchanganyiko wa wekundu na kahawia.

Wote madume na majike huwa na alama nyeupe za kipekee kwenye mashavu, shingoni, mapajani na usoni kati kati ya macho. Kwa kuongezea hapa huwa wana madoa meupe na mistari kati ya sita hadi minane iliyo simama wima katika miili yao.

Dume huwa na umbo kubwa kidogo kuliko jike. Wanyama hawa dume tu ndio huwa na pembe ambazo ni ndefu na zimejikunja ambazo hufikia urefu wa sentimita 45 – 90.

Kadri wanavozidi kukuwa, madume huota manyoa na kuwa na mstari mweupe unaoteremka chini eneo la mgongini.

Wana uwezo mkubwa sana wa kuogelea. Pale wanahisi hata hukimbilia ndani ya maji na wakati mwingine kuzama kabisa chini wakiogelea huku wakiacha sehemu ya pua kwa juu kwa ajili ya kupumua.

Nzohe ni wanyama ambao wana uwezo wa kuona mchana na usiku pia japo inasemekana huwa wapo vizuri zaidi kipindi ambacho jua linaanza kuzama, yani kuanzia mida ya laasiri.

Ni wanyama ambao huishi katika maeneo yenye eneo dogo sana ukilinganisha na swala wengine japo kuna wakati wanaweza kuondoka katika eneo hilo hasa mida ya usiku hasa pale wanapowa wamejificha muda mrefu wakati wa mchana dhidi ya maadui zao.

Wanyama hawa huishi kwenye kundi na mara nyingi kundi huwa na kina mama tu na watoto ambao bado wanaendelea kukua. Mara nyingi madume huungana na majike pale unapofika wakati wa kuzaliana.

KIMO, UREFU NA UZITO WA NZOHE

Kama tulivoona hapo juu kuwa dume huwa kidogo mkubwa kuliko jike. Sasa hapa tutachukua wastani tu kwa kuangalia uzito kwa nzohe kuwa wanakuwa na uzito na kimo kiasi gani.

Kimo=sentimita 75sm – 125sm

Urefu=Kichwa na kiwiliwili sentimita 115sm – 170sm huku mkia ukifika hadi urefu wa sentimita 35sm.

Uzito=Kilogramu 40kg – 120kg.

MAZINGIRA

Nzohe hupenda maeneo yenye majani mengi na marefu ambayo yapo karibu na mabwawa  au hata mabwawa ya misimu. Wanyama hawa hutumia zaidi ya nusu ya maisha yao kuishi sehemu zenye maji nahii kupelekea kuitwa ni miongoni mwa wanyama ambao maisha yao nusu majini na nusu nchi kavu. Hujiepusha sana na sehemu za maji ambazo zipo wazi zaidi kwani maeneo hayo huwa sio mazuri kwao hasa kwa upande wa chakula na jinsi ya kujificha dhidi ya maadui zao.

CHAKULA

Nzohe ni miongoni mwa wanyama walao majani kama walivo swala wengine wote. Hupendelea majani yaliyo karibu na mabwawa, kando kando ya mito na hata yale yalio maeneo yenye unyevu nyevu misituni. Wakati mwingine nzohe huonekana wakila mbegu za mimea mbali mbali na magome ya baadhi ya mimea.

KUZALIANA

Kama nilivokwisha sema hapojuu, wanyama hawa majike huishi pekeyao na hukutana na madume pindi tu wanapotaka kuzaliana na baada ya hapo hukaa kwa muda mfupi sana kisha kusambaratika na hii hutokea mara chache sana kukaa pamoja baada ya kupandana. Mara tu baada ya kupandana majike na madume husambaratika na jike hukaa na mimba kwa muda wa miezi minane hadi minane na nusu (takribani siku 240 – 250) na baada ya hapo huzaa mtoto mmoja tu.

Mara nyingi watoto huzaliwa katika maeneo ya mabwawa yaliyo kauka na huishi hapo huku wakinyonya kwa vipindi vifupi kwa takribani mwezi mzima. Watoto huendelea kunyonya na kuwa chini ya uangalizi wa kina mama kwa muda wa miezi minne hadi sita, na baada ya hapo ukaribu kati ya mama na mtoto huanza kupungua na kwa muda mfupi tu mtoto huanza maisha yake huku akiwa kaungana na kundi la watoto wenzie.

Nzohe jike huanza kuzaa afikishapo umri wa miaka 2 wakati dume huanza kupanda majike afikashapo miaka miwili au miwili na nusu. Japo mara nyingi huanza miwili na nusu na kipingi hiki anakuwa hajawa na uwezo wa kupigana na madume wakubwa ili kumiliki kundi la majike.

Umri wa nzohe wa kuishi awapo katika mazingira asili huwa ni miaka 19 – 20. Japo kama anafugwa katika bustani huweza kufikisha miaka 22 – 23.

UHIFADHI

Ni jambo la kumshukuru Mungu bado wanyama hawa wapo wa kutosha hususani hapa nchini kwetu Tanzania na bado hawajaingizwa kwenye kundi la wanyama walio hatarini kutoweka. Kuna baadhi ya nchi kama nilivoanza kudokeza hapo juu wanyama hawa wametoweka kabisa. Yani utazunguka nchi nzima lakini huwezi kumuona Nzohe wala viashiria vyake. Mfano wan chi hiyo ni Togo. Haya kuna baadhi ya nchi wamepetea kwenye baadhi ya maeneo ambayo walikuwa wana onekana mfano nchini Niger. Unajua hii yote ni sababu ya nini?, utapata jibu kwenye changamoto hapo chini.

Kwa sasa takwimu zinaonesha wapo jumla ya Nzohe 170,000 tu bara zima la Afrika na ukumbuke kuwa wanyama hawa wanapatikana barani Afrika tu na si kwingineko duniani. Na kwa idadi hiyo ni asilimia arobaini tu (40%) ya Nzoha ndo wapo katika maeneo Tengefu ya wanyamapori wengine wametawanyika maeneo mbali mbali.

Takwimu pia kwa sasa zinaonesha idadi hii ya Nzohe inapungua siku hadi siku kitu ambacho ni hatari sana mana kinaweza pelekea wanyama hawa kutoweka kabisa.

CHANGAMOTI KWA NZOHE

Changamoto kubwa sana kwa wanyama hawa ni uharibifu wa mazingira ambao hupelekea pia kuharibika kwa mahitaji ya ki ikolojia kwa wanyama hawa. Hali ya kuongezeka kwa uharibifu wa ardhi oevu ambayo huwa ni chanzo kikubwa kwa mahitaji ya Nzohe kumepelekea kwa kiasi kikubwa idadi ya wanyama hawa kupungua na hata mijongeo yaokatika maeneo mbali mbali kwa sasa imepotea kabisa. Hii imepelekea hata makundi ya wanyama hawa kujitenga kwani mazingira yaliyokuwa yakiwakutanisha tayari yamekwisha haribiwa.

Madiliko ya kupungua na kuongezeka kwa maji hasa katika maeneo ya ardh oevu yamepelekea wanyama hawa pia kupungua sana kwani wanakosa hata mazingira ya kujificha au kuwakimbia maadui zao kwani tumeona hapo huu wanyama hawa ni hodari sana katika kuogelea sasa kama maji yanakuwa yamepungua basi ni rahisi kukamatwa na maadui zao.

Ujangili ulio kithiri kwa wanyama hawa. Nzohe wamekuwa wakiwindwa sana na majangili hasa kutokana na mahitaji ya nyamapori na kuongezeka kwa biashara haramu ya nyama za porini. Hii huwafanya watu kuingia katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori na kuwinda wanyama kiholela bila kujali jinsia au afya ya mnyama.

Uchomaji moto wa maeneo kiholela kitu ambacho kina punguza maeneo ya kuishi kwa wanyama hawa na hivyo kuishia kuuwawa na majangili au maadui zao kama simba, chui na fisi.

SULUHISHO LA CHANGAMOTO KWA NZOHE

Usimamizi mzuri na ufuatiliaji wa utekelezaji wa uhifadhi wa maeneo yenye ardhi oevu. Tumeona hapo juu wanyama hawa bila maji hawawezi kuishi hata kidogo ukilinganisha na jamii nyingine za swala.. Hivyo serikali kupitia sera na sheria za hifadhi za wanyamapori pamoja na Wizara husika zihakikishe utekelezaji wa sheria hiyo unafuatwa vizuri bila kupepesa macho. Kwa kufanya hivyo itasaidia sana kupunguza dhurba ya uharibifu wa mazingira ambapo ni kitu hatarishi kwa Nzohe.

Uandaaji mzuri wa mikakati ya utekelezaji wa sera za kupambana na ujangili nchini hasa kwa kutoa mafunzo ya uzalendo na kujitolea kwa askari wa wanyamapori. Ikiwezekana kuongeza hata idadi ya askari hawa kwani kwa uhalisia askari waliyopo hawatoshi kabisa ukilinganisha na maeneo ya hifadhi za wanyamapori yalivyo makubwa.

Kupambana na uchomaji hovyo wa misitu na hasa karibu na maeneo oevu kwani kunapelekea sana kuharibu ikolojia ya wanyama hawa na hatimae kusababisha kuhama baadhi ya maeneo.

HITIMISHO

Tusidanganyike na idadi iliyopo kwa sasa ya Nzohe kwani ni idadi ndogo sana endapo changamoto zilizo tajwa hapo juu hazita tafutiwa ufumbuzi wa haraka. Hebu fikiria kama kwa siku wana uwawa Nzohe 10 maana yake kwa mwaka mzima tunapotenza nzohe 3650. Bado wengine wanakufa kwa magonjwa na wengine huliwa na wanyama walao nyama kama usawa wa ikolojia.

Kwaiyo kwa haraka haraka tunaweza ona kwa mwaka tunapoteza asilimia 2% ya Nzohe kitu ambacho ni hatari sana ndugu zangu. Nalia na mamlaka husika kuendeleza uzalendo wa uhifadhi wa wanyama hawa kwani hadi sasa kwakweli tunaona matunda ya kazi ya mamlaka mbali mbali hapa nchini na nje ya nchi na bila wao sijui tungekuwa wapi hususani kwenye suala la maliasili tulizojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

 

Pongezi sawa kwa Dr. Hamis Kingwangalla kwa mwanzo mzuri aloanza nao katika kusimamia sheria za maliasili na kwakweli tunakuomba kuendelea na kasi hiyi hiyo ili nidhamu ya uhifadhi maliasili irudishe hadhi yake. Nyuma ya Dr.Kingwangalla wakiwepo TANAPA, TAWA,NCAA na TAWIRI kwa pamoja tunalo jukumu la kuhakikisha tunapambana na kusimamia kwa hali na mali uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yao ili vizazi vijavyo viweze kushuhudia kile tulichopewa na mwenyezimungu kama ufahari wetu hapa nchini.

AHSANTENI….

Kwa mengi na ushauri zaidi juu ya wanyamapori au mchango wowote kuhusu makala hizi basi wasiliana mwandishi kupitia

Sadick Omary

Simu= 0714116963 / 0765057969 / 0785813286

Email= swideeq.so@gmail.com

Au tembelea = www.mtaalamu.net/wildlifetanzania

.I’M THE METALLIC LEGEND”….