Habari ndugu zangu Watanzania, hongera kwa kupata siku ya leo tena, katika siku chache za nyuma nilipata tangazo moja zuri sana ambalo lilinifikirisha na kunipa wazo la kuandika makala hii. Nilifikiria mambo mengi sana na vitu vingi sana kuhusu suala la utalii wa ndani. Kama kuna vitu napenda nione vinafanyika sana katika nchi yangu ya Tanzania ni kuona watanzania wameamka kwenye suala la utalii wa ndani. Tunaposema utalii wa ndani tuna maanisha kuwa wageni au watalii wanaotakiwa kutembelea vivutio mbali mbali tulivyo navyo ni watanzania wenyewe hasa wazawa, hili ndio jambo ninalolipenda sana kuliona likifanyika hapa Tanzania.

Watanzania, hatuwezi kusingizia kwamba hatuna sehemu ya kwenda kutalii au sehemu za kwenda kutembelea vivutio. Nchi yetu imejaa tele, nchi yetu imebarikiwa nchi yetu ina vivutio vyote, vya kihistoria na vya kiasili. Huu ndio urithi wetu watanzania ambao tunatakiwa kuuenzi, kuutunza na kuutumia. Ndugu zangu hili ni jambo ambalo kila mtanzania analiweza, hatuhitaji ufadhili kwenye jambo kama hili, tunahitaji kuchukua hatua madhubuti na zinazostahili ili kufanya jambo hili muhimu kwenye maisha yetu na nchi yetu. Tutembelee Hifadhi na mbga za wanyama, tutembelee fukwe za bahari, tutembelee sehemu za kihistoria, tuitembelee Tanzania yetu wenyewe.

Kwa kiasi kikubwa tupo hapa tulipo kutokanana na misingi tuliyojenga au kujengewa, na ambayo tunaendelea kuifuata kila siku. Mali ni zetu wenyewe, wanyama ni wetu wenyewe, misitu ni yetu wenyewe, nchi ni yetu wenyewe, lakini kwa nini watu kutoka nje ndio wafurahie vitu tulivyo navyo kuliko sisi wenyewe, kwanini tuwategemee watalii wa nje kukuza pato la ndani, kwanini wazungu. Kuna watu wengine hufikiri kuwa mambo yanayohusu utalii na kutembelea hifadhi za wanyamapori au vivutio vingine ni mambo ya wazungu tu. Yani hata kama atamwona jirani yake anapanga kwenda kutembelea hifadhi za wanyama au sehemu nyingine ya vivutio anashangaa na anaweza kumkatisha tamaa na kumwambia mambo hayo ni ya wazungu, mtalii utakuwa wewe, achana na mambo hayo, hivi una fedha za kuchezea eeh, mambo hayo huyawezi waachie wazungu! nk

Kweli kabisa utamaduni tulionao kwenye mambo ya utalii hausaidii hata kidogo kukuza utalii wa ndani. Tunatakiwa kubadilika kabisa kwenye jambo hili, tunatakiwa tuachane na mambo yasiyo na tija kwenye maisha yetu na taifa letu. Tuingie kwenye utalii, tuwe watalii sisi wenyewe. Tuache kusubiri wazungu ndio tuwaone watalii, sisi wenyewe ni watalii na hatua ya kwanza ni kuanza kufanya hivyo kwa vitendao kabisa, tujenge utamaduni huu mzuri kwa gharama yoyote. Tunahitaji kujivunia vya kwetu, hapa hapa Tanzania kuna vitu vingi ambavyo wengi wanataka kuviona nje ya nchi, nikwambie tu kwamba kuna vitu vingi hujaona na vinapatikana hapa hapa Tanzania.

Tuanze kwa hatua chache kufanyia kazi jambo hili, tuhakikishe tunawaachia watoto wetu utamaduni ulio bora zaidi kuliko tulio nao sasa, tuwaachie utamaduni wa kupenda vya kwao, kupenda maliasili zao, kupenda vitu vilivyozalishwa hapa hapa kwetu, hili ni jambo linaloweza kufanywa na kila mzazi, kila mtanzania, watanzania nitengeneeeni kizazi cha watu wazalendo tu, hilo tu ndio ombi langu. Baba, mama, kaka, dada, kijana, mjomba, shangazi, nitengenezeeni kizazi cha kizalendo, kizazi kinachothamini kutalii nyumbani, na kutangaza utalii wa nyumbani. Kwa miaka mingi ijayo watoto wetu na vitukuu vyetu watatushukuru sana kwa jambo hili.

Mitazamo yetu inatakiwa kubadilika na kuanza kuitanzama Tanzania kwa jicho tofauti kidogo, watoto wanapokuuliza ni sehemu gani nzuri sana hapa duniani mwambie ni Tanzania, akikuuliza ni nchi gani nzuri sana hapa duniani mwambie Tanzania, akikwambia ni nchi gani yenye vitu vizuri mwambie Tanzania, akikuuliza ni nchi gani yenye watu wazuri duniani mwambie Tanzania. Kwa kufanya hivyo utamjengea mtoto kwenye akili yake kwamba hakuna nchi bora na nzuri hapa duniani kama Tanzania.Na atayaishi hayo na kuwekeza Tanzania, ataishangilia Tanzania, ataitanzaza Tanzania na ataipenda Tanzania.

Asante sana kwa kusoma makala hii, kama una maswali, ushauri hata mapendekezo karibu sana.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255683 862 481/+255742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaam.net/wildlifetanzania