Mafanikio ya kudumu katika kitu chochote yanahitaji gharama na kujitoa kuhakikisha yanajijenga na kuimarika. Mafanikio kwenye kitu chochote yanahitaji mfumo bora unaoeleweka na kukubaliwa na watu. Mafanikio ya kudumu kwenye jambo lolote lazima yalenge kwenye utatuzi wa migogoro na changamoto zinazowakabili watu au jamii. Hivyo basi mafanikio kwenye jambo lolote lazima yawe na mfumo bora unaoeleweka na wenye tija kwa jamii.

Sekta ya maliasili inahitaji kujipanga sana kwenye jambo hili endapo tunataka mafanikio ya kudumu kwenye maliasili zetu. Tunatakiwa kuiangalia mara kwa mara mifumo ya utalwala, usimamizi na utoaji wa faida kwa jamii. Kwa namna yoyote tunayotaka jamii ishiriki kikamilifu kwenye uhifadhi wa maliasili tunapaswa kuwa na mfumo ambao unaeleweka na unaonufaisha jamii nzima kwenye ushiriki wao, mifumo yetu tuliuo nayo inapaswa kuwa ya wazi na jamii inapaswa kujulishwa kuhusu utendaji na usimamizi wa maliasili hizo.

Tunaweza kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali lakini kama hakuna mfumo bora wa kuhakikisha jamii inanufaika na rasilimali hizo, mafanikio kwenye ukuaji na usimamizi wa rasilimali hizo utakuwa mgumu sana. Kwa mfano tujifunze kwa nchi zenye utajiri wa mafuta, au gesi au rasilimali nyingine kama madini, kunapokosekana mfumo wa wazi na unaolenga kuwanufaisha wazawa, hali ya usimamizi na uendeshaji wa rasilimali hizo unakuwa mgumu sana, tujifunze kwenye jambo hili, angalia nchi nyingi za Afrika, kama vile Sudani, Kongo, na nchi za Magharibi mwa Afrika kama vile Nigeria zina migogoro isiyoisha kutokana na kufanya mambo bila kuishirikisha jamii, au kuwa na mfumo wa kinyonyaji ambao wazawa hawafaidiki na rasilimali za nchi yao.

Suala la kuieleimisha jamii ili ishiriki kwenye uhifadhi wa wanyamapori na rasilimali nyingine sio la kuwaambia tu kuhusu uzuri na jinsi wanavyotakiwa kushiriki kwenye uhifadhi. Jamii inatakiwa kuelewa utendaji kazi, uwajibikaji, vyanzo vya mapato, kiasi cha mapato hayo, mikataba ya umiliki na uendeshaji wa huduma mbali mbali kwenye maeneo husika, makubaliano yaliyofikiwa; lakini kubwa zaidi ni ushiriki wa jamii kwenye masuala hayo ya rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao. Pia kila kinachoendelea kwenye uwekezaji kinatakiwa kuwekwa kwenye taarifa na wananchi wanapaswa kusomewa au kusoma taarifa hiyo. Kila kitu kinatakiwa kufanyika kwa weledi na uzalendao wa hali ya juu sana.

Uongozi na usimamizi wa rasilimali za nchi unatakiwa kuangaliwa kwa makini sana, kwa miaka kadhaa iliyopita tunasikia kashfa nyingi sana zinazowakabili watendaji, wasimamizi na maofisa kwenye vitengo na idara mbali mbali za sekta ya maliasili na utalii. Tunasikia huyu kafanya hivi na vile huyu kala rushwa, mara huyu kahongwa nk. Kweli inasikitisha sana na inavunja moyo kwa watu wanaopewa dhamana ya kusimamia mali ya umma, wao wanaitumia kama mali binafsi kwa maslahi yao wenyewe. Sasa fikiria katika hali kama hii unaweza kumshawishi mwananchi kushiriki kwenye uhifadhi wa malisili hizo ambazo yeye mwenyewe hajawahi kuona faida inayotokana na uwepo wa maliasili hizo, wala hajawahi kushirikishwa kwenye maamuzi na pia hajui hata mapato yanayoingia kwenye kijiji chake kutokana na maliasili hizo.

Kama ilivyoelezwa kwenye sheria ya uhifadhi wa Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009  kifungu cha 98, na kwenye Sera ya wanyamapori Tanzania ya mwaka 1998 kifungu cha 3.2.5 kwamba mamlaka husika zinazosimamia masuala ya wanyamapori zinatakiwa kutoa elimu ya uhifadhi kwa umma, jambo hili linatakiwa kufanyika kwa mbinu na ubunifu wa hali ya juu sana. Ili kuhakikisha jamii inaelewa kinaga ubaga kuhusu maliasili na uhifadhi wa wanyamapori, pia jamii inatakiwa kujulishwa kwa uwazi kabisa namna inavyonufaika na uwekeza wowote unaotokea kwenye maeneo yao. Endapo jambo hili litafanyika suala la jamii kushiriki katika uhifadhi wa malisili utafanyika kwa mafanikio makubwa na utakuwa wa kudumu.

Mafanikio ya kudumu kwenye uhifadhi wa malisili tulizo nazo unahitaji juhudi kubwa kusimamia kwenye kila hatua, pia itahitajika kuboresha na hata kuondoa mifumo ya uongozi na usimamizi ambayo haina tija kwa taifa, itahitajika uongozi, usimamizi na watalamu wazalendo kwenye malisili hizi. Pia utayari wa kufanya maamuzi magumu na yenye tija kwa uwazi. Na kuweka mifumo bora inayotoa urahisi wa jamii kushiriki kwenye uhifadhi na kufaidika na maliasili za nchi yao kwa kufanya hivi tutatengeneza mfumo bora na wa kudumu ambao utakuwa na mafaniko makubwa sana.

Mwisho, nimalizie kwa kusema wanaotakiwa kusimamia maliasili za nchi yetu ni watanzania wenyewe, hivyo tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha hili linafanikiwa, inaonekana kama tuna uhaba wa viongozi wazalendo, sasa kama watakosekana watanzania wenye sifa na wazalendo wa kusimamia rasilimali za nchi tutafanya nini? Au tutaajiri wageni waje kusimamia maliasili zetu. Hatua za haraka tunazoweza kuchukua hapa ni kubadilika na kubadili mfumo wa uongozi, usimamizi na hata maisha yetu wenyewe. Tunapambana kuokoa tembo na faru, lakini tunasahau kuwa hawa wanyama hawana shida wenye shida ni sisi wenyewe, hivyo tupambane kuokoa uzalendo tunaoupoteza, hili ni jambo linalowezekana kabisa.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255683 862 481/+255742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaam.net/wildlifetanzania