Misingi ndio kila kitu kwenye safari yoyote ya maendeleo, kila kitu kwenye maisha kina misingi yake. Ujenzi imara unaanza na misingi imara, na ujenzi mbaya ni matokeo ya misingi mibaya. Hivyo basi misingi ndio inayotoa mwelekeo wa kitu chochote. Kama wahifadhi na watalaamu wa mambo haya tuanatakiwa kuilewa misingi ya kazi zetu na misingi ya sekta tunayoisimamia. Hii ni pamoja na kuelewa sera na sheria za uanzishwaji na usimamizi wa sekta hiyo na manufaa yake kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Kwenye sekta ya maliasili na utalii kuna misingi ambayo iliwekwa na kuandikwa kwenye sera na katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Ibara ya 27 (1) na (2) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatoa wajibu kwa kila mwananchi na serikali kulinda na kusimamia maliasili za nchi yetu kwa ustawi wa taifa letu. Hivyo kwa kuwa wajibu wetu kama raia wa nchi ya Tanzania ni kwamba tunahusika moja kwa moja kwenye kulinda na kusimamia maliasili za nchi, ikiwemo wanyamapori, misitu na maliasili nyingine za nchi. Hii ndio misingi ambayo ipo wazi kabisa.
Pia kwa upande mwingine sera ya wanyamapori ya mwaka 1998 imeelekeza kuwa mapato yanaotokana na uwepo wa maliasili yanatakiwa yawanufaishe jamii hasa jamii ambazo zipo kando kando ya hifadhi za wanyamapori. Kwenye majarida na ripoti mbali mbali inaonyesha kuwa jamii zinazoishi kando kando ya rasilimali hizi hazinufaiki ipasavyo kutokana na uwepo wa rasilimali hizo.
Pamoja na kwamba serikali ilitenga maeneo ya hifadhi ya jamii WMA ambayo yanasimamiwa na wanajamii wenyewe nje ya maeneo ya hifadhi za taifa, maeneo haya tangu yaanzishwe yamekuwa na matokeo yasiyoridhisha kwa sehemu nyingi. Maeneo haya ya hifadhi ya jamii yalitegemewa kuwa ndio chachu ya maendeleo kwa jamii hizi yamekuwa na migogoro na usimamizi mbovu ambao hauna tija kwa jamii.
Kwa kuwa tuna nafasi kubwa sana ya kufanikiwa kwenye sekta hii, serikali na mashirika ya umma, wadau wengine wa mazingira na watu wenye nia ya kweli kwenye uhifadhi wa wanyamapori hapa Tanzania, kurudi kwenye misngi ya mwanzo na kuangalia sheria za usimamizi wa maliasili ndio jambo muhimu zaidi kwa sasa ili mwananchi wa kawaida aweze kunufaika, na mwanajamii akinufaika atakuwa tayari kulinda, kutetea na kushiriki kikamilifu kwenye uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine muhimu.
Nimalizie kwa kusema kila mmoja akirudi kwenye nafasi yake tutafika mbali sana. Kila mtu afanye kwa nafasi yake kwa mujibu wa sheria za nchi. Tutaendelea kuwa nchi bora zaidi duniani kwa utalii endapo tutazingatia misingi hii muhimu yenye faida kwa pande zote. Usimamizi mzuri, uadilifu, uwajibikaji na uzalendo kwenye maliasili zetu ndio njia pekee itakayotufanya kubakia kuwa nchi muhimu na bora kwa utalii duniani.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania