Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambayo tunajifunza mambo mbali mbali kwenye sekta hii ya wanyamapori. Katika kuendelea kujifunza hatutaweza kujifunza kila kitu kwenye maliasili, kwa sababu unapoongelea maliasili unajumuisha vitu vingi sana. Kila mtu unaposema maliasili anapicha yake inayokuja kichwani, lakini leo kwenye makala hii nataka niweke wazi kipengele cha maliasili ambacho tutakuwa tunajifunza wakati wote. Kama nilivyokudokezea kidogo kuwa dhana ya maliasili ni kubwa na pan asana, inajumuisha vitu vingi asilia ambavyo vipo kwenye ardhi ya Tanzania. Ukweli ni kwamba kila nchi hapa duniani ina maliasili zake, lakini tunatofautiana kwenye uwingi na aina ya maliasili ambazo nchi husika inazo.
Mailiasili ni rasilimali zote asilia zilizopo kwenye rdhi ya nchi husika mfano kama wanyama, ardhi, misitu, madini, gesi, mito, bahari, maziwa, milima, na reasilimali nyingine zote zinazojumuisha ardhi. Kwa ufupi rasilimali ni nyingi sana. Mailasili zilizopo nchini ni muhimu sana kwa maendeleo endelevu ndio maana juhudi kubwa zinahitajika kwenye kuzitambua, kujua umuhimu wake na kuzitunza kwa ajili ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Utambuzi wa rasilimali hizi ni muhimu sana kwa jamii kwasababu bila utambuzi wa rasilimali zilizopo kwenye jamii au eneo fulani hakuwezai kuisaidia jamii hiyo kiuchumi, na kimaendeleo. Kwa kuwa dhana ya maliasili ni kubwa na pana sana, mimi sitakuwa nazungumzia kila maliasili tulizonazo hapa Tanzania, nitajikita zaidi kwa maliasili za wanyamapori na misitu. Nimeamua kujikita kwenye wanyamapori kwa kuwa ndio eneo la taaluma yangu, na misitu kwa kuwa misitu ina nafasi kubwa sana kwenye maenedeleo na uwepo wa wanyamapori. Hivyo huwezi kutenganisha, kwa sababu misitu ina faida kubwa sana kwenye uhifadhi wa wanyamapori. Hivyo ndugu msomaji wa makala za mtandao wako wa Wildlife Tanzania tutakuwa tunajifunza rasilimali zote zinazohusiana na wanyamapori, misitu sambamba na utalii.
Tanzania ina eneo la ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba 945,000 kati ya hizo hekta zaidi ya milioni 48 ni hifadhi ya misitu na hekta milioni 13 kwa ajili ya hifadhi ya ardhi na uhaianuai, pia kuna idadi ya hifadhi za taifa 16, Mapori ya akiba 28, mapori tengefu 44, pia maeneo ya Jumuiya za hifadhi ya jamii (WMAs) zipo zaidi ya 19. Haya yote ni maeneo muhimu sana kwa uhifadhiwa wanyamapori na misitu. Hivyo kwa kutambua utajiri tulio nao serikali ilikuwa na jukumu la kusimamia rasilimali hizi kwa niaba ya wananchi.
Ni muhimu sana kwa serikali kuwa na usimamizi mzuri na wanye tija kwa maliasili zake, kwani nimeona nchi nyingi zikiingia kwenye vita na migogoro isiyoisha kwa sababu ya rasilimali za nchi kutotumika ipasavyo kwa ajili ya wananchi wake. Kukosekana kwa usimamizi mzuri wa rasilimali za taifa kumepelekea machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa nchi nyingi duniani hasa nchi za Afrika. Hivyo ni muhimu tukawaambia wananchi kwa usahihi kuhusu maliasili hizi na jinsi zinzvyoweza kuwasaidia. Tuwaelimishe siku zote ili wafahamu na kushiriki kwenye uhifadhi wa maliasili hizi. Tena tulenge kuwanufaisha wananchi wote kwa rasilimali za nchi hii.
Hivyo naamini kufia hapa umepata maarifa ya kiuelewa juu ya maliasili zetu, na pia utaendelea kujifunza ili kuelewa zaidi kuhusu wanyamapori, misitu na utashiriki kuhifadhi maliasili hizi popote pale ulipo.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania