Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambayo tutaangazia mambo yanayotokea kwenye maeno mengi hapa nchini. Kuna jambo nataka kulielezea hapa na jambo hili ni kuhusu wafugaji na uhifadhi wa wanyamapori. Kumekua na changamoto nyingi sana kwa wafugaji na hata wadau wa mazingira na wahifadhi wa wanyamapori. Mahusiano mengi kati ya wafuaji na mamlaka za hifadhi za wanyamapori sio mzuri kwa kipindi kirefu kidogo. Tumeshuhudia migogoro ya mara kwa mara hasa kwa wafugaji wanaoishi kando ya maeneo ya hifadhi ya wanyamapori.

Kimsingi wanyamapori wana maeneo yao yaliyotengwa kwa muda mrefu, hivyo hata wafugaji wana maeneo yao ambayo yametengwa. Lakini kwa muda kumekuwa na mwingiliano wa wanyamapori na wafugaji kwa sababu wafugaji wengi hupenda kuishi na mifugo yao karibu na maeneo ya hifadhi za wanyamapori, hii yote ni kwa ajili ya malisho ya mifugo yao, kwa sababu ya ukaribu huu, wanyamapori kama vile simba, fisi, mbwa mwitu, chui wamekuwa wakileta usumbufu na hasara kubwa sana kwa wafugaji walio karibu na hifadhi za wanyamapori, kwani wanyamapori hawa huvmia mifugo ya wafugaji wakiwa malishoni na wakati mwingine wakati wanyama wapo kwenye maboma yao ya asili, wakati wa usiku.

Ukiachilia mbali wanyama wengine wanaosumbua lakini wanyama wanaokula nyama wanavamia sana mifugo ya wafugaji na kusababisha hasara kubwa kwa watu hawa. Hivyo kwa kiasi kikubwa mfugaji huyu anapowaona wanyamapori kama simba, fisi na wengine wanaokula nyama anaona kama adui yao, na hivyo huwauwa kwa njia mbali mbali, ikiwa ni kwa kuwawinda kuwawekea sumu na njia njingine za kuwatokomeza. Aidha tafiti nyingi kuhusu wanyama wanao kula nyama zinaonyesha wanauliwa sana kwa sababu za kulipiza kisasi, na sababu nyingine za kitamaduni.

Na kwa kuwa wafugaji hawaoni faida za moja kwa moja zinazoletwa na wanyama hao wanaokula mifugo yake hawaoni shida kuwaua. Hata baada ya kutoa elimu ya uhifadhi wa wanyamapori bado kumekuwa na changamoto hii kwa maeneo mengi. Ikumbukwe pia kwa kiasi ikubwa jamii hizi za kifugaji hazijapata elimu ya darasani, hivyo kukosekana kwa elimu kwenye jamii hizi za kifugaji kumekua na changamoto ya kuelimisha jamii hii kwani wengi hawajasoma, na kwasababu hiyo jamii hizi zinaendekeza miala na desturi zilizopitwa na wakati kama vile ili uoe na kuwa na sauti kwenye jamii lazima uue simba au tembo.

Haya ni mambo yanayotokea kwa wafugaji wengi wanaoishi kando kando ya hifadhi na makazi ya wanyamapori. Na kwa kuwa serikali hajajipanga vizuri kutatua changamoto hii na kuwafanya wafugaji waone faida za uwepo wa wanyamapori kwenye maeneo yao, tatizo hili limekuwa likiendelea, wakati mwingine naona serikali ikitumia nguvu nyingi sana za kisheria kukabiliana na jambo hili, lakini tujiulize hawa wafugaji ambao wapo kwenye maeneo haya wananufaikaje na hao simba na wanyama wengine tunaowatete na kuwahifahi?

Pamoja na juhudui za serikali kwenye utatuzi wa jambo hili,  kumekuwa na miradi mbali mbali ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira ambayo inafanya kazi sehemu hizi zenye changamoto hii, ambapo wanajitahidi kuelimimisha na kuwa karibu na jamii hizi za kifugaji ili waweze kuona faida za wanyama hawa. Kwa sababu ya vipaumbele kuwa vingi na vinavyo hitaji fedha, manufaa yanayotolewa moja kwa moja kwa jamii hizi ni kidogo sana, hata mashirika makubwa ya serikali kama vile TANAPA wanajua jambo hili lilivyo changamoto kwao.

Aidha tunatakiwa kutatua changamoto hii kwa kushirikiana na kushirikisha wadau wengine kenye sekta hii, tunatakiwa kuwa na mfumo mzuri na wa wazi unaoeleweka kwa ajili ya kunufaisha wafugaji na watu wengine wanaoishi kando ya hifadhi. Pia kiasi ambacho kinatolewa kwenye jamii kama faida ya moja kwa moja kutokanana uwepo wa wanyamapori kinatakiwa kuongezeka ili kwenda sawa na mahitaji ya jamii, kwani kwa sasa kiasi ni kidogo sana ukilinganisha na mapato ya jumla ya utalii kwenye hifadhi za wanyamapori jambo jingine serikali itoe fursa kwa mashirika mazuri kwenye uhifadhi wa wanyamapori yaweze kuanzishwa hapa Tanzania, sio tu mashirika yanayotoa elimu pekee lakini yanayotoa faida kubwa kwa jamii za watu wanaoishi karibu na hifadhi za wanyamapori.

Kwa upande mwingine wafugaji wanatakiwa kuelewa mipaka ya maeneo yao ya malisho, pia wanatakiwa wazijue sheria za uhifadhi wa wanyamapori, sheria ya ardhi na sheria nyingie zinazosimamia sekta hii, jambo hili litawafanya waamue kuchukua hatua stahiki ili kuepuka migogoro isiyoisha ya wanyamapori. Pia wanaweza kutafuta msaada wa kisheria na wa kitalaamu pale ambapo wanahisi kuonewa na kunyimwa haki zao.

Naamini umepata picha fulani kwenye makala hii kuhusu mahusiano ya wafugaji na wanyamapori. Endelea kujifunza na kila siku! Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania