Habari msomaji wa wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo tutaangazia jcho letu kwenye mahusiano ya wakulima na wanyamapori au wanyama wanaoharibu mazao ya wakulima. Kama tunavyojua Tanzania inategemea kwa kiasi kikubwa kuendesha uchumi wake kupitia sekta ya kilimo, sekta hii imekuwa ndio uti wa mgogo kwa watanzania wengi, karibia asilimia 80 ya watanzania wote ni wakulima. Kuna wanaolima kilimo kikubwa kwa ajili ya biashara na kuna wanao lima kawaida kwa ajili ya chakula na matumizi mengine madogo madogo, lakini yote katika yote maisha yao yanategemea kilimo cha mazao hasa mazao ya chakula.
Tanzania ina eneo kubwa sana kwa ajili ya shughuli mbali mbali za uzalishaji, kama vile kilimo, hifadhi ya misitu, mdini, maji, hifadhi ya wanyamapori maji, na hifadhi ya maeneo oevu. Kwa mujibu wa tafiti mbali mbali, maeneo yanayofaa kwa kilimo cha kawaida ni makubwa sana, na pia hata maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ni makubwa sana. Hivyo kulingana na sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012, tulikuwa watanzania zaidi ya milioni 45. Ukilinganisha na eneo la ardhi ya nchi yetu lenye ukubwa wa kilomita za mraba zaidi ya 945,000. Bado Tanzania inaonekana kuwa na eneo kubwa sana kwa ajili ya kila shughuli za uzalishaji na maendeleo.
Aidha kulingana na ukubwa wa eneo hili la nchi, Tanzania sio nchi ya kusema hakuna maeneo kwa ajili ya kuendesha shughuli fulani za maendeleo, kama vile kilimo cha kawaida na kilimo cha umwagiliaji. Kwa kiasi kikubwa inchi ya Tanzania ilishatenga maeneo mengi na makubwa kwa ajili ya hifadhi ya wanyamapori na misitu, pia maeneo oevu ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya makazi na mazalia ya viumbe hai muhimu kwenye ikolojia ya wanyamapori. Maeneo haya yaliyotengwa ndio yanayotambuliwa kirahisi na watu wengi na yametungiwa sheria za usimamizi na uendeshaji wake.
Msomaji wangu, unajua kuwa unaweza kuwa na eneo kubwa sana lakini usipojua jinsi ya kulitumia utaona kama halitoshi na ni dogo; hapa namaanisha unaweza kuwa na eneo kubwa sana la nchi, lakini eneo hilo lisipopangwa vizuri linaweza lisitohe kwa matumizi ya watu na shuguli zao. Mipango ardhi ni muhimu sana kwani itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa na kupunguza migogoro ya ardhi. Inatakiwa ifikie mahali kila kundi kwenye jamii ya Tanzania waelewe kabisa maeneo yao ya kufanyia shughuli zao za kila siku. Kama ni wafugaji waelewe, kama ni wakulima waelewe maeneo yao, kama ilivyotengwa na kupangwa kwa sekta ningine kama misitu na wanyamapori.
Kuna changamoto kubwa nimeiona kwa wakulima wanaolima mashamba yao karibu na hifadhi za wanyama, kwa eneo la hifadhi ya Ruaha ni kubwa sana na linachukua sehemu nyingi na mikoa kama Iringa, Dodoma, SIngida na Mbeya. Nimeona wakuliama wakipata shida ya wanyamapori aina ya nyani, tembo , tandala, nguruwe na ngiri wanakuja kula mazao ya wakulima hawa wanaolima kwenye maeneo yaliyo karibu na hifadhi za wanyamapori, pia hata ndege wamekuwa ni changamoto kubwa sana kwa wakulima. Unakuta mkulima ameshalima shamba lake na amelipalilia na anatakiwa kukaa hapo kuyalinda mazao yake mpaka yakomae na ayavune bila hivyo anaweza asipate kitu.
Mfano kwa wakulima wa tarafa ya Pawaga na Idodi wanakabiliwa sana na changamoto hii hasa kipindi cha kilimo, kwa tarafa ya Pawaga ambapo wanajishuhulisha sana na kilimo cha mpunga, tembo ndio wamekuwa wanyama waharibifu sana kwenye mashamba ya mpunga, ndege nao hawapo nyuma kwenye uharibifu huu. Kwa hiyo kwa wakulima hawa wanatumia gharama kubwa sana kenye uzalishaji wa chakula. Kwa Idodi nako ni shida kubwa ambapo wamejikita kwenye kilimo cha mahindi na mpunga. Hii ndio changamoto ninayoiona ikijirudia mara kwa mara kwa wakazi wa maeneo haya yaliyokaribu na hifadhi za wanyamapori. Na tafiti zinaonyesha si maeneo haya tu ndio yanachangamoto hii, ni maeneo mengi sana yaliyo karibu na hifadhi za wanyamapori.
Juhudi za serikali kwenye changamoto hii huwa zinaonekana pale ambapo kunatokea matukio ya ushambulizi wa mazao na wanyamapori. Nimeona Askari wa TANAPA wakija na kuwafukuza wanyama hawa, nimeona pia Kikosi cha kuzuia na kupambana na Ujangili (KDU), wakija kuwafukuza wanyama hawa wasumbufu. Nawapongeza kwa kazi yao, lakini nayo inachangaomto kubwa ya kukosa vitendea kazi ya uhakika kama vile magari mazuri na vifaa vingine vya kazi, pia kuna maeneo mengine magari hayapiti na pia maeneo ya mashamba ni makubwa ukiinganisha na idadi na nguvu inayotumika.Pia wamekuwa wakitoa fidia kidogo kwa wanaoripoti maukio hayo.
Ingawa tunweza kujifunza kutokana makosa pia tuchukue hatua nyingine ngumu zaidi kunusuru na kutatua changamoto hizi. Ni kweli kwamba sio kila mara wakulima wanaonewa wakati mwingine ni wakulima ndio wanasababisha matatizo, na wakati mwingine ni maamuzi na sheria tulizounga zinatoa nafasi hii. Kwa mfano kwa watu wanaolima kilimo kikubwa cha mpunga kwenye mashamba makubwa kwenye bonde la Usangu, unakoanzia mto Ruaha Mkuu, wanachangia sana kupungua kwa maji kwenye mo Ruaha na kuathiri maisha ya wanyamapori.
Ningependa serikali ipitie tena sheria zake mara kwa mara kuhusu hali hii, ili kwa pamoja tuweze kutatua tatizo hili, wizara zinazoshirikiana zikikaa pamoja wanaweza kuja na jibu pana na zuri lenye tija kwa miaka mingi ijayo. Wizara kama ya ardhi, wizara ya kilimo, wizara ya maji, wizara ya madini, wizara ya maliasili na utalii, wizara ya mazingira na wizara nyingine zinaweza kukaa kwa pamoja kwenye jambo hili ili kuweka mambo sawa kabisa. Najua ni jambo gumu ndio maana linahitaji maamuzi magumu kulitatua. Naamini hakuna kinachoshindikana kwenye jambo wanapukutana watu wengi.
Ahsante sana
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania