Habari za leo msomaji wa mandao huu, karibu kwenye barua yetu ya leo, kila jumapili nimepanga kukuandikia barua moja ya wazi, barua hii ni ya wazi hivyo inamfaa kila mtu kuisoma. Kwenye barua hii niliyoipa kichwa “hadi sasa umepanda miti mingapi” ni barua ambayo ipo kwenye mfumo wa swali hivyo nategemea utakaposoma hadi mwisho unaweza kutushirikisha chini ya barua hii kwamba ulishapanda miti mingapi hadi unafikia umri huo ulio nao. Nikifafanua kidogo hapa kwenye kichwa cha barua hii ni kwamba umeshapanda miti mingapi, au umeshaotesha miti mingapi ndicho ninacho maanisha kwenye barua hii. Karibu tujifunze pamoja na tuchukue hatua mara moja.

Miti ni muhimu sana kwenye mazingira yetu na mazingira ya viumbe hai wengine. Ndio maana kabla ya sisi kuja hapa duniani miti ilikuwepo na Mungu alihakikisha mazingira yote yanayofaa kwa binadamu kuishi yanakuwa tayari ndio tukaletwa hapa duniani. Umuhimu wa miti ni mkubwa sana tukianza kuzitaja faida za miti au misitu ni nyingi mno. Mungu alijua tunahitaji hewa ya Oksijeni ili tuendelee kuishi hapa duniani hivyo akamua kupanda miti ya kila aina ili itoe hewa ya kutusaidia kuishi hapa duniani. Na mfumo aliouweka Mungu kwenye uumbaji ni wa ajabu sana, sisi binadamu na viumbe hai wengine tuna uhusiano wa wazi kabisa na mimea au miti, ndio maana miti inatoa hewa ya oksijeni ambayo tunaitumia na binadamu na sisi tunatoa hewa ya Cabondioxide ambayo hutumiwa na mimea.

Nafikiri kila mtu anajua umuhimu wa hewa ya oksijeni kwenye maisha yake. Binadamu hawezi kuishi hata kwa lisaa limoja bila hewa ya oksijeni. Nimeona na imeripotiwa mara nyingi sana kwenye vituo mbali mbali na kwenye magazeti na kwenye vitabu mbali mbali jinsi watu wanavyokufa haraka kwa kukosa hewa ya oksijeni. Madaktari wanaelewa na wanajua vizuri mgojwa anapokosa hewa hii hawezi kuendelea kuishi kwa dakika chache zijazo. Watalaamu na wanasayansi wamejitahidi kutengeneza hewa hii ambayo husaidia kuokoa maisha ya watu pale wanapokuwa kwenye hali mbaya na wanahitaji hewa hii, lakini gharama ya hewa hii iliyotengenezwa ni kubwa sana na sio ile ya asili.

Na pia maelfu na mamilioni ya wanyama na viumbe hai wanaotumia oksijeni wamepoteza maisha kwa sababu ya uharibifu wa misitu na ukataji wa miti, uchomaji wa moto na uchafuzi wa mazingira asilia ya wanyama na viumbe hai hawa. Ilisha wahi kuripotiwa katika moja ya bahari za huko Marekani idadi kubwa sana ya samaki na viumbe wengine wa baharini walikufa kwa kukosa hewa ya oksijeni baada ya meli kubwa ya mafuta kuvujisha mafuta hayo kwenye bahari na kuzuia hewa ya oksijeni isiwafikia samaki na viumbe hai waliokuwa baharini. Matokeo yake ile kampuni iliyokuwa inasafirisha mafuta yale walilipa faini kubwa sana za mamilioni ya dola za kimarekani kwa uharibifu na uuaji walioufanya pamoja na kusafisha mafuta yaliyotapakaa kwenye bahari hiyo.

Hivyo basi kwa umuhimu huu wa hewa ya oksijeni, tunaweza kusema hivi ni bora ukakosa fedha kuliko kukosa hewa ya oksijeni, na kwasababu hiyo tukiangalia kwa jicho la mbali tunaweza kurudi kwenye chanzo cha hewa ya oksijeni na tunaweza kusema hivi ni bora ukakosa pesa kuliko kukosa miti au misitu au mimea. Kwa mantiki hii misitu na mimiea hazipaswi kuharibiwa kwa sababu za kuichumi, au kwa sababu tumeishiwa fedha za maendeleo, au kwasababu tunahitaji fedha za haraka za ujenzi au ukandarasi. Uwepo wa misitu au miti unatakiwa kuangaliwa kwanza si kama kitu kinacholeta fedha nzuri, bali kama kitu kinachosababisha maisha hapa duniani yaweze kuendelea.

Kwa kusema hivyo simaanishi tusitumie misitu tuliyonayo kutengeneza fedha za maendeleo, hapana, misitu inatakiwa itoe faida hizo, lakini mtazamo wetu wa kwanza unapoona miti na misitu unawaza fedha tu, hii haitatupeleka mbali, tunatakiwa kuwa na mtazamo wa mbali zaidi unaovuka na kuvunja kabisa matamanio ya fedha, na kuifanya kuwa na sehemu ya kusababisha maisha ya viumbe hai wanaendelea kuwepo hapa duniani. Tuna wajibu wa kuifanya dunia kuwa sehemu bora kabisa ya kuishi. Tunapofikia wakati wa kuondoka hapa duniani tunatakiwa kuiacha dunia kwenye hali nzuri na bora sana kuliko tulivyoikuta, hatutakiwi kuwaachia watoto wetu na vizazi vijavyo dunia iliyochoka, yenye ukame na njaa kutokana na kutowajibika kwetu.

Kwenye mwanzo wa barua hii nilikuuliza swali, hadi sasa umepanda miti mingapi? Nafkiri baada ya kusoma barua hii hadi hapa utakuwa unaelewa umuhimu wa kuwa na miti na kupanda miti, pia umeelewa kwanini ni hatari kukata na kuchoma misitu. Najua kwa kiasi kikubwa jamii yetu haina utaratibu wa kupanda miti, ilia tunajua vizuri jinsi ya kukata miti, kuharibu badala ya kutengeneza. Sisi binadamu Mungu katupa uwezo na upeo wa kipekee ndio maana alitupa hii dunia na mazingira yake akatuambia tuyalinde na kuyatunza; nafikiri ulishasikia msemo wa wahenga wakisema “tunza mazingira ili yakutunze”.

Kuna watu wana miaka 30, 40, wengine 50, wengine 70 na wengine 80 na wengine wana miaka 100 waliyoishi hapa duniani, lakini waulize taratibu wamepanda miti mingapi hadi kufikia umri huo na ni miti mingapi ambayo ipo hai, utashangaa, kama hutastaajabu. Fikiria hivi tena, hawa watu hadi wanafikia umri kama huu wameharibu miti mingapi, wamekata miti mingapi wameua viumbe hai wangapi? Halafu wanataka kuondoka hapa duniani na kutuachia dunia isiyo na miti, na yenye ukame, unatudhulumu ndugu yangu, unakidhulumu kizazi kijacho, wewe huna fadhila, huna huruma, unajiangalia wewe mwenyewe. Kuna mtu mmoja aliwahi kusema ukiona mtu ana kaa kwenye kivuli leo ujue kuna mtu alipanda miti mika mingi ya nyuma. Wewe unataka kuondoka hapa duniani umekaa kwenye vivuli wala hukuchomwa na jua na pia ulipata hewa safi kutoka kwenye miti hiyo waliopanda wenzako kwa jasho na damu, na tena mingine uliiharibu wala hata hukukumbuka kupanda mingine, unavyofanya sio kabisa.

Kama bado ni mzima, Unaweza kubadilisha mambo na pia unaweza kuweka historia mpya, haijalishi miaka uliyonayo, haijalishi haukuwahi kuapanda miti hata mmoja kwenye maisha yako. Unaweza kuamua kuchukua hatua za makusudi, nenda kapande miti kama kichaa, panda miti mingi kuliko uliyoitumia na kuiharibu, panda miti mingi kuliko umri ulio nao na pia unapoipanda isimamie mpaka itengemae na kuendelea kukua bila usimamizi, kwa sababu haina maana kupanda miti halafu hakuna anayeisimamia. Hata kama hauna eneo la kupanda nenda hata kijijini kwako ukapande miti, nenda kwenye kampeni za upandaji wa miti na hudhuria semina na jifunze kupanda miti au kuotesha miti. Panda miti sio mpaka usubiria kampeni za kupanda miti ndio na wewe uanze kupanda tengeneza msitu wako.

Waache na wengine waje wakae kwenye kivuli cha miti uliyopanda, utakuwa umesaidia sio tu ndugu zako na jamii yako bali hata dunia nzima. ongezeko la watu liendane na ongezeko la upandaji wa miti. Nafikiria kama kila mtu hapa Tanzania kwa idadi tulionayo ya zaidi ya milioni 50, kila mtu angekuwa amepanda miti tangu akiwa na mwaka mmoja, au kila mwaka leo tungekuwa na bustani ya misitu na hali nzuri zaidi ya hewa na mazingira yetu yangekuwa bora zaidi, na mvua na majira ya mwaka yangekuwa hayapishani wala kubadilika, kwa ufupi kusingekuwa na njaa.

Nakushukuru kwa kusoama makala hii, mshirikishe na mwingine maarifa haya ili kwa pamoja tuchukue hatua za mara moja na tupande miti, panda miti mingi kuliko umri wako. Waambie na wafundishe watoto wako jambo hili. Panda miti hata kama hakuna anayekuona na kukusifia, endelea mbele panda miti zaidi.

Ahsante sana

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania