Kuna vitu kwenye maisha ukivikosa maisha yako yanasimama, na unaweza kufa kwa kuvikosa vitu hivyo. Vitu vya namna hiyo ndio huitwa mahitaji ya msingi na ya lazima kwa binadamu yeyote. Nikitoa kalamu na karatasi nikampa mtu nikamwambia aniandikie mahitaji yake ya msingi anayohitaji ili aishi sidhani kama ataandika anahitaji meno ya tembo na pembe za faru. Meno ya tembo na pembe za faru sio mahitaji ya muhimu na ya msingi kwa binadamu, mtu akikosa meno ya tembo na pembe za faru hawezi kufa wala hawezi kupungukiwa na kitu chochote.
Meno na pembe tuwaachie tembo na faru, wao ndio mahitaji yao ya msingi ili maisha yao yaendelee kuwepo. Ukimnyang’anya tembo meno yake hataendelea kuishi, ukimnyang’anya faru pembe zake hataendelea kuishi, utakuwa umeharibu maisha yao na uhai weo ndio utakuwa umeishia hapo hapo. Mambo mengi ya uharibifu siku zote hufanyika kwa ajili ya maslahi binafsi. Ukangalia wanaoagiza pembe za faru na wanaohitaji meno ya tembo sio kwa ajili ya kunufaisha jamii au kuwasaidia watu wawe na maisha bora, bali ni kwa ajili ya tamaa na ubinafsi, tena anasa. Anasa za watu wachache zinaharibu mfumo mzima wa maisha ya wanyamapori na kuidhulumu dunia urithi wa asili unaotakiwa kutunzwa kuenziwa kwa vizazi vingi vijavyo.
Unapoua faru mmoja au tembo mmoja sio kwamba umeua moja, umeuwa wengi, umeharibu mfumo wa maisha ya wanyamapori. Wanyama hawa wakiwa porini wana umuhimu wao mkubwa ambao hufanya uwepo wa wanayama na viumbe hai wengine uendelee kuwepo. Ujangili huwa hauna macho, ujangili ni kama ugaidi hawaangalii usoni, hawana muda na kukufikiria, tamaa ya fedha na umaarufu vimewafunika na kuwatawala hawana uwezo wa kufikiria kuwa wanafanya jambo baya kwenye maliasili. Hawaangalii kama mnyama huyo ana watoto au hana, wanachoangalia kwa wanyama hawa ni pembe tu, ndio wanaua wanyama hawa wa thamani.
Maisha ya maelfu na mamilioni ya viumbe hai yamekatishwa na kuharibiwa na watu wachache wenye tamaa. Mataifa yanayoagiza pembe za faru na meno ya tembo yanatakiwa kutoa adhabu kali na kuhakikisha kila anayehusika na biashara hiyo haramu anatafutwa na kuchukuliwa hatua kali. Na kwa kuwa Afrika ndio imekuwa sehemu ya kupata malighafi hizo, na sisi ni wakati wa kuungana na kupinga kuzuia na kuua kabisa mitandao yote ya ujangili kwenye bara la Afrika na kwenye hifadhi zetu.
Tusimame kwa pamoja na kuwa sauti kwa wanyama hawa wasioweza kuongea, tuwahifadhi sio tu kwa ajili ya ufahari na kujipatia utajiri kupitia utalii wa picha, lakini pia kwasababu uhifadhi wao ni uhifadhi wa mazingira yote yanayowafanya wawepo. Hivyo wakiwa salama na mazingira yao yatakuwa salama na mazingira yao yakiwa salama na mazingira ya wanyama, mimea na viumbe wengine yatakuwa salama, hivyo hata binadamu atakuwa salama na dunia itakuwa sehemu salama ya kuishi. Kila mmoja wetu anatakiwa kuelewa jambo hili ili kila mtu aweze kutoa ushirikiano wa kuhakikisha wanyamapori hawa wanaendelea kuwepo na wanathaminiwa na jamii nzima.
Shiriki pamoja nasi kupiga vita ujangili kwenye maliasili zetu.
Ahsanete sana.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania