Habari msomaji wa mtandao wa wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambayo tunajadili na kujifunza kitu kimoja ambacho kitatusaidia kubadili mitazamo na jinsi tunavyochukulia mambo. Makala hii fupi nimeandika kutokana na hali yetu watanania tunavyotazama maisha na vitu tulivyo navyo. Leo tunazungumzia utalii na kutembelea hifadhi za wanyama, vivutio vya mambo ya kale, fukwe na sehemu nyingine zenye kuleta hisia nzuri na kukupa fahari na asili ya mambo. Nitajadili kidogo kuhusu utamaduni ambao tunauona kwa wenzetu lakini sisi hatuufanyii kazi sana.
Utamaduni unatengenezwa, kitu chochote ambacho kimekubaliwa na watu wengi huwa wanakifanya hata kama kina gharama kiasi gani. Utamaduni unatengenezwaje? Kitu kikiruhusiwa kwa muda mrefu kwenye jamii, watu watakikubali, na wakikikubali watakifanya na wakiifanya ndio utamaduni wenyewe huo. Utamaduni ni kufanya kile kinachokubaliwa na kuthaminiwa na jamii hiyo mara kwa mara. Hata kama kitu ni kibaya kama kikikubaliwa na watu na sheria ikikikubali kitu hicho kinaanza kupata kibali kwa watu na watu wanaanza kuona kuwa ni jambo la kawaida na kuanza kufanya.
Kwa nini naongea haya, kuna kitu natamani kijengeke na kifanyike kuwa sehemu ya maisha yetu kama watanzania. Utamaduni unapotawala mahali unakuwa ni sehemu ya maisha ya jamii hiyo. Kuna vitu vizuri ambavyo tunaweza kuiga kutoka kwa wenetu wa magharibi au wazungu. Na moja kati ya vitu hivyo ambavyo tunaweza kuiga ni utamaduni wao wa kutembelea vivutio. Ukiangalia wanavyopangilia maisha yao utaona kabisa kutembelea vivutio na sehemu mbali mbali duniani imekuwa kama sehemu ya maisha yao. Huwa wanaamini katika kujifunza kwa namna hii. Kutembea ni kujifunza, na pia kujifunza ni kupata mawazo mapya na nguvu mpya ya kuendelea kuboresha maisha ili yawe bora zaidi.
Hivyo jambo hili la kutembelea hifadhi na vivutio mbali mbali sio jambo linaweza kufanyika kwa haraka, litachukua muda hadi kufikia idadi nzuri ya watanzania wanaotembelea hifadhi na vivutio. Ingawa kuna utamaduni huo kwa baadhi ya watu wachache, tunatakiwa kuwafundisha na kuwapa kila uwezekano wa wao kutembelea hifadhi za wanyama na kutalii sehemu mbali mbali kwa madhumuni mbali mbali. Na endapo tutachukua hatua ndogo kila siku kwa ajili ya kuelimisha jambo hili kwa watanzania matokeo yatakuwa mazuri na watu watakuwa na hamasa ya kuchukua hatua, hatimaye tutakuwa tumejijengea utamaduni mzuri ambao hautaondolewa na kuachwa kwa vizazi vingi vijavyo.
Jambo hili linaanza na mtu moja mmoja kuanza kuchukua hatua kutengeneza utamaduni huu, kisha ataifundisha familia yake au marafiki zake na kila mtu atakuwa ni balozi kwenye jamii yake. Hivyo ndivyo mabadiliko makubwa yanavyotokea. Kama unafamilia anza na familia yako kuwapeleka hifadhini, mbugani, sehemu za makumbusho, au kwenye fukwe za bahari nenda na familia yako, ili uwajengee wanafamilia utamaduni wa kuthamini na kujali maliasili za nchi yao wenyewe.
Ahsanete sana.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania