Tanganyika ilipata uhuru wake rasmi tarehe 9/12/1961, baadaye kidogo wakaungana na Zanzibar mnamo tarehe 26/4/1964 na kutengenezwa jina jipya la Tanzania, hapa ndipo jina la Tanzania lilipozaliwa. Kweli ukirudi kwenye historia ya nchi hii, kuna visa vingi sana, kuna historia ya mashujaa wengi, kuna harakati na mambo ambayo yaliwalazimu kuyafanya ili wawe na nchi huru iliyo na watu huru na watu wawajibikaji, uwajibikaji ilikuwa ndio nguzo kuu kwenye uhuru tulioupata. Jambo la uzalendo na kuheshimiana lilitiliwa mkazo na waliliishi bila kusubiri nani aanze. Napongeza sana juhudi hizi zilizozaa matunda hadi leo tuna nchi huru, yenye watu huru na yenye utulivu.
Tumefikia miaka 56 tu tangu tuwe huru, miaka hii sio mingi sana, bado nchi yetu ni changa na hapa nazungumzia umri wa nchi yetu. Ukiangalia nchi nyingine duniani zina historia ndefu na zina umri mkubwa sana hadi miaka 200, 100 nk. Kwa kuwa bado tuna uwezo mkubwa sana wa kukua kwa kasi na kufikia mafanikio makubwa tunatakiwa tuangalie vitu tulivyo navyo. Kwa mfano sehemu kubwa sana ya rasilimali zetu bado hazijatumika, ukianzia na ardhi, madini, wanyama, na hata misitu. Tuna akiba nzuri sana na ya kutosha ili kuitumia kwa vizazi vingi vijavyo.
Tukiangalia nchi nyingine za ulaya, waliamua kufanya maamuzi ambayo hadi leo wanayajutia na kati ya vitu walivyofanya ni kuharibu rasilimali zao muhimu, kama vile misitu, maeneo ya wanyamapori na hivyo kusababisha mazingira mengi ya asili kutoweka, zipo sababu nyingi sana ikiwemo ni ukuaji wa miji, ongezeko la watu, uanzishwaji wa viwanda kwenye maeneo ambayo ni muhimu kwa makazi ya wanyama na mimea.
Hivyo sisi tunatakiwa kuwa na hekima na uzalendo kwenye matumizi ya rasilimali zetu, tunatakiwa kuwa msitari wa mbele ili kuboresha na kuangalia kila penye nyufa na kuziziba haraka iwezekanavyo. Tunatakiwa tujifunze kutokana na makosa yao, ili kuboresha maisha yetu na nchi yetu. Tuhakikishe kuna mpango wa utekelezaji unaotekelezeka ili kuinufaisha jamii kutokana na uwepo wa wanyamapori na rasilimali nyingine kwenye maeneo yao.
Nawapongeza wazalendo wote walioifikisha nchi yetu hapa ikiwa na rasilimali zote muhimi, hawakuwa wabinafsi, hawakuharibu misitu au kutumia kitu chochote cha umma kwa maslahi binafsi, kwa miaka hii 56 ya uhuru, bado tunaweza kuiona Tanzania kuwa ni sehemu nzuri na iliyobaki na asili yake. Juhudi hizi ndizo zinazotakiwa kuigwa na kuziendeleza zaidi kwa kizazi hiki na tuwaridhishe watoto, wajukuu na vitukuu nchi iliyojaa unono wa rasilimali muhimu.
Ahsante sana
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania