Kuna mtu aliuliza swali kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na  changamoto ambazo zinaletwa na utoaji wa rushwa kwenye maeneo yanayohusu maliasili. Rushwa ni mbaya sana hakuna sehemu ambayo rushwa itatolewa halafu watu na rasilimali zilizoko hapo zikawa salama. Kwa namna nyingine mtu anayetoa rushwa na anayepokea rushwa wanakubaliana kuharibu sio tu heshima zao bali hata vitu wanavyopokea.  Rushwa haijawahi kumwacha mtu salama. Wala haijawahi kuacha kitu salama. Kwenye rushwa kuna uharibifu, kuna ubinafsi na maslahi binafsi.

Rushwa inaua uzalendo, maana kama unapokea rushwa hakuna uzalendo. Tukija kwenye sekta ya maliasili na utalii, matendo mengi ya ujangili ni kwa sababu ya uwepo wa rushwa baina ya watu. Ni mara chache sana ujangili unafanyika bila kuwepo kwa rushwa, rushwa inapindisha ukweli na ni adui wa haki. Kuenea na kustawi kwa ujangili kwenye maliasili zetu chanzo kikubwa ni kuwepo kwa mianya mingi ya utoaji wa rushwa kwenye ngazi mbali mbali ili anayekuja kufanya ujangili au kuharibu maliasili asichukuliwe hatua zozote.

Watu wengi waliokamatwa kwa vitendo vya kijangili wameshindwa kufikishwa mahakamani kwasababu ya kuwepo kwa rushwa, rushwa inaharibu sana kupatikana kwa haki kwenye maeneo mengi, rushwa imechelewesha maendeleo ya wengi, rushwa imefanya wengi wenye sifa ya kupata kazi kukosa kazi, rushwa imefanya wasio na sifa wala uwezo kupata kazi, rushwa imeharibu kabisa misingi ya utu na usawa kwenye jamii yetu, rushwa imepofusha macho ya viongozi ambao walikuwa na macho ya kutazama mbele, rushwa imechangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa matabaka katika jamii zetu, rushwa imeua uwezo wa watu wengi waliokuwa na uwezo. Rushwa ni mbaya na haifai kwenye jamii yoyote.

Tunapofikiria kuwepo kwa manufaa ya uwepo wa wanyamapori karibu na makazi ya watu, tunapotaka wanyamapori wawe na faida kwa jamii, tunapotaka jamii iwe na usimamizi wa maliasili zilizopo kwenye maeneo yao, tunatakiwa kujua kwanini hatufanikiwi kama tunavyotaka, kwanini hatufkii lengo letu, kwanini jamii hainufaiki, ukiangalia maeneo mengi yenye migogoro ya aina hii utajua tu au watu wataanza kulalamikia viongozi kutokuwa waadilifu kwenye usimamizi wa maliasili zao, kutokuwepo kwa usawa na uwazi kwenye mambo haya kumesababisha matatizo yasiyoisha. Kamwe hatuwezi kufanikiwa kwenye malengo yetu makubwa ya kunufaisha jamii na kupunguza migogoro bila kushughulikia suala la rushwa kwenye maliasili zetu.

Mara nyingi kukosekana kwa uwajibikaji, kutofuata sheria ndio mambo yanayochangia kila hali ya uwepo wa rushwa kwenye maliasili zetu. Jamii inatakiwa kushirikishwa kwenye mambo yote muhimu ya usimamizi wa rasilimali, kuziba mianya yote ya rushwa, pia kuweka watu walioshughudiwa wema na watu wengi, wenye uzalendo na wanaofanya kazi. Suala sio kuweka kila mtu, hapana bali ni kuweka watu na mfumo ambao utazuia watu kupokea na kutoa rushwa kwenye maeneo yetu.

Ndugu msomaji wa makala hii, suala la rushwa lipo kila mahali, lina madhara makubwa sana sio kwenye sekta ya wanyamapori pekee, bali kila sekta inakumbana na changamoto hii. Hii ndio sababu hakuna matokeo makubwa kwenye sekta nyingi zinazoandamwa na masuala ya rushwa. Ufanisi unapotea, ubora unaisha na viwango vinalegezwa na kushushwa. Hakuna aliyetamani kuwa na fedha nyingi akaridhika, hakuna aliyewahi kupokea rushwa nzuri, rushwa haina uzuri na ubaya, rushwa ni mbaya moja kwa moja,inakemewa kila mahali, kwenye dini, kwenye serikali, kwenye biashara, kwenye familia, kwenye kila eneo la maisha rushwa inakemewa, lakini cha ajabu hicho kinachokemewa ndio kinafanywa sana wakati mwingine hata na hao wanaoikemea na kuwaambia wengine wasifanye hivyo, inashangaza.

Kuwa miongoni mwa wachache, usikubali rushwa kuwa sehemu ya maisha yako, usikubali kwa namna yoyote ile kujihusisha na masuala ya rushwa kwenye eneo lolote la maisha yako, kuwa mwanga, hata kama wenzako wote wamezimika, endelea kunga’aa , ishi maisha ya kizalendo, toa mchango wako kwa jamii yako, ishi maisha ya wema na tengeneza misingi iliyoharibika. Endelea kusimama hata kama umebaki peke yako.

Ahsanete sana.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania