Habari msomaji wa makala hizi za mtandao wa wildlife Tanzania, karibu sana kwenye makala hii ambayo nimeiandaa ili tuwe na tafakari kidogo kwenye maliasili zetu. Kuna mambo mengi sana ambayo yanafanyika ambayo yanatishia kuendelea kuwepo kwa wanyamapori na rasilimali zetu. Kwenye makala hii kama nilivyoandika kwenye kichwa cha habari uadilifu na uzalendo kwenye sekta ya maliasili. Najua kabisa kwa zama hizi kama kuna kitu kinaendelea kuwa adimu basi ni uadilifu na uzalendo, uadilifu umekuwa wa kutafuta na hauonekani kwa watu wengi. Hii ni kutokana na matendo yasiyo ya kizalendo kuendelea kushamiri hasa kwenye maliasili zetu.

Watu wengi tumekuwa tukiimba uadilifu na uzalendo, tumekuwa tukidai na kuwalalamikia viongozi wetu kuwa hawana uadilifu kwenye mali za umma. Watu pamoja na kwamba wanaapa kuwa watakuwa waadilifu kwenye kulinda na kutunza rasilimali za nchi bado kumekuwa na mianya mingi ya ubadhirifu, rushwa na kukosekana kwa uzalendo kwenye sehemu nyingi za rasilimali za nchi yetu. Watu waliopewa dhamana ya usimamizi wa maliasili hizi wanafanya mambo kwa maslahi binafsi bila kufikiri kizazi kijacho kitafaidikaje na rasilimali hizo.

Naendelea kuona juhudi na mchango mkubwa wa wazee wetu ambao walikuwa ni wazalendo wakaamua kuhifadhi maliasili tunazoziona leo kwa maslahi ya kizazi hiki, ni jambo ambalo sisi wa kizazi hiki tunatakiwa kufanya na kuhakikisha maliasili zetu zinawafikia kizazi kingine. Ili kufanikisha jambo hili hatuna budi kufanya kazi kubwa kujizuia sisi wenyewe na kufuta sheria za uhifadhi wa maliasili zetu. Tunahitaji kuwa waadilifu na wazalendo ili kufikia malengo ya kuhakikisha wanyamapori na rasilimali nyingine zinawafikia na kuwanufaisha vizazi vijavyo.

Suala hili la kuwa waadilifu na wazalendo halitakiwi kuwa la viongozi tu wanaopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za nchi yetu, bali inatakiwa kuwa ni vitu vya msingi vinavyotakiwa kuonekana kwenye maisha yetu ya kila siku, ukiwa muadilifu na mzalendo utakuwa na nafasi kubwa sana ya kuona mapungufu yaliyopo na kuyakemea na pia utasimama kwenye ukweli na haki siku zote. Hivyo kabla ya kuangalia wengine tujiangalie sisi wenyewe kweli tuna uadilifu na uzalendo kwenye maliasili za nchi. Fikiria ukipewa wewe nafasi ya kuwa kiongozi au msimamizi wa rasilimali za nchi utakuwa mwadilifu na mzalendo hata kama utashawishiwa kwa kiasi gani?.

Tusipojifunza kuwa waadilifu na wazalendo kwenye kutetea maliasili na kutunza maliasili hizi, hakika tutawaridhisha watoto na vizazi vijavyo nchi iliyochoka isiyo na maliasili za kutosha. Tunatakiwa kuacha nchi yetu imejaa neema, imejaa misitu na maliasili zake zote muhimu. Watu wenye hekima popote duniani hata kwenye historia huwa wanaishi maisha yao kwa kufikiria kizazi kijacho kitanufaikaje au kitapata faida gani kutokana na maisha yao wanayoishi kila siku, hivyo walikuwa na nafasi ya kufanya maamuzi magumu ili kuhakikisha kizazi kijacho kinafurahia na kuwakumbuka kama wazalendo na watu waliosimamia vizuri rasilimali za nchi bila ubinafsi na uchoyo.

Tuna wajibu wa kuwaridhisha watoto na vizazi vijavyo misingi ya maisha ambyo ni uadilifu na uzalendo hasa kwenye uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine muhimu. Wakivikuta vitu hivi hakika maisha yatakuwa na thamani kwa kila kiumbe hai. Tufanyie kazi kwa bidii na kuweka mipango ya kuishi maisha ya uadilifu na uzalendo sio kwa ajili yetu wenyewe bali kwa ajili   wengine wengi ambao hawajazaliwa, timiza jukumu hili kwenye kipindi cha maisha yako hapa duniani na uiachiea dunia urithi na lulu za thamani kama hizi za uzalendo na uadilifu, hakika hata kama utakufa utaendelea kuishi wenye mamia na maelfu ya mioyo ya watu. Na watoto na nchi yako watakushukuru kwa kuwa raia wa nchi yao.

Ahsanete sana.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania