Habari msomaji wa mtandao huu wa wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambayo tunatafakari kuhusu juhudi zetu kwenye uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine. Juhudi tulizo nazo kwenye uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine zinatakiwa kuthaminiwa na kuungwa mkono na mamlaka za nchi husika. Uungwaji mkono na kuwa na dhamira ya dhati kuhifadhi maliasili zetu ni jambo tunalotakiwa kuliona kutoka kwa wakuu wa nchi na wenye mamlaka ili kazi yetu iwe na mafanikio makubwa na kupata ushirikiano kutoka kwa jamii yetu.
Kuna watu, kuna mashirika na miradi mingi sana ina nia ya dhati kwenye kupambana na uharibifu kwenye maliasili zetu, kuna wanaopambana na majangili wanaoua tembo, kuna wanao pambana na wanaofanya ujangili wa wanyama wengine kama vile swala, twiga, tandala, na wengine wengi. Tuwaunge mkono na kuwapa mazingira mazuri ya kuendelea kufanya mambo makubwa kwenye maliasili zetu.
Kuna watu wengi wamepoteza maisha yao kulinda maliasili za nchi, kuna walio uwawa kwa kupigwa risasi, kuna walioumwa na nyoka, kuna waliopata ajali na kuwa na vilema vya maisha kwa sababu ya kutetea maslahi ya nchi, kutetea tembo wa Afrika waendelee kuwepo, kuna walio liwa na wanyama wakali kwa sababu ya kufanya doria na kuzuia majangili wasiingie kwenye hifadhi za wanyama na kuua wanyamapori wetu. Watu kama hawa ambao wametoa maisha yao kulinda rasilimali za nchi tutawalipa nini, juhudi na uzalendo wao unatakiwa kuthaminiwa.
Niameandika makala hii baada ya kutafakari habari moja iliyoripotiwa kutoka katika nchi ya Zimbabwe kwamba mke wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo anatuhumiwa na kushikiliwa na polisi kwa tuhuama za kuhusika kwenye biashara ya meno ya tembo. Meno hayo yaliyokamatwa katika uwanja wa ndege wa Robert Mugabe yakiwa tayari kusafirihwa kwa biashara kwenda nchi nyingine yame kamatwa. Nilishangaa baada ya kusoma taarifa hiyo ambayo ilinipa maswali mengi sana.
Juhudi za nchi mbalimbali, mashirika na watu binafsi wanapambana kuua kabisa biashara hii haramu ya meno ya tembo, lakini kuna watu wenye nafasi za juu serikalini wanatumia nafasi zao kufanya kinyume kabisa na inavyotarajiwa. Jambo hili linaua kabisa na kuthorotesha juhudi zetu kwenye uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine. Vile vile hii inaonyesha mtandao wa biashara hii unahusisha watu wakuu, na wenye nguvu, ambao wananafasi kubwa kwenye serikali zetu. Jambo hili limetokea Zimbabwe na kuripotiwa kuwa viongozi wa ngazi za juu wanajihusisha na baishara hii haramu ya meno ya tembo, si jambo la ajabu kuwa hata nchi nyingine wanatumia nafasi zao za juu serikalini kujihusisha na Bashara hii haramu. Licha ya vyombo mbali mbali vya kitaifa na kimataifa kupaza sauti kuhusu kutokomezwa kwa bishara hii lakini bado watu wanaendelea kufanya.
Viongozi hawa na serikali zetu walitakiwa kutumia nafasi na mamlaka yao kupambana na biashara hii kwa vitendo, walitakiwa kuunga mkono kwa vitendo kuhusu uhifadhi na kuzua kabisa vitendo vya kijangili kwenye maliasili zetu. Walitakiwa kuwa wazalendo na wawazi, walitakiwa kuwa mfano wa kuigwa kama viongozi wenye dhamira ya dhati kupambana na ujangili.
Kwa mwenendo huu bado wanazidi kufanya vita dhidi ya ujangili kuwa ngumu, kwa sababu hawana dhamira ya kweli kwenye jambo hili. Na hapo sio tu kwamba wanadhorotesha juhudi za wahifadhi kwenye nchi yao, bali hata kwenye mashirika na watu wengine wanaofanya kazi hii hapa duniani. Nawapongeza mamlaka na serikali ya nchi ya Zimbabwe kwa kuripoti jambo hili ambalo litachangia sio tu kuzuia ujangili kwenye nchi yao pekee bali kwenye nchi nyingine zinazokabilia na jambo hili la ujangili, sheria ikifuatwa kwa usahihi nafikiri watampa adhabu inayostahili kwa matendo yake.
Mwisho, nataka serikali zetu na watu wenye nyadhifa na mamlaka za juu wasizidhoroteshe juhudi zetu kwenye uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingie, watuunge mkono, waunge mkono wale wenye juhudi za dhati kwenye kupambana na ujangili na uharibifu wa mazingira. Wanatakiwa kuwa msitari wa mbele kabisa kuongoza mapambano dhidi ya biashara hii haramu. Naamini mamlaka za kiserikali zikiwa na dhamira ya dhati hakuna knachoshindikana, na tutapata matumaini kwa uwepo wa wanyamapori na mazingira yake kuendelea kuwepo kwa vizazi vingi. Pia jambo la namna hii halipaswi kutukatisha tamaa wahifadhi na watu wengine wenye nia njema na maliasili zetu, bali iwe ni jambo ambalo litatupa na kutoa mbinu nzuri zaidi kukabiliana na ujangili na biashara ya meano ya tembo, faru na wanyama wengine.
Ahsanete sana.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania