Habari za siku ndugu msomaji wa makala za wanyamapori. Ni matumaini yangu umzima wa afya kabisa na kama unasumbuliwa na maradhi au msongo wa mawazo basi mwenyezi Mungu akuepushe na matatizo hayo. Ila pia tujitahidi kufanya mazoezi kwani maradhi mengi yanatokana na sisi wenyewe kutokuwa na tabia ya kufanya mazoezi na hatimae miili yetu kuwa dhaifu hasa tunapo shambuliwa na vimelea vya magonjwa.

Leo ni siku nyingine tena tunaingia darasani kujifunza mambo machache kuhusu wanyamapori na mazingira yao huku tukiangazia zaidi uelekeo wa wanyama hao hususani hapa nchini kwetu Tanzania. Katika makala za hivi karibuni nimekuwa nikiwaelezea sana wanyama jamii ya swala. Ni ukweli katika kundi hili kuna wanyama wengi sana na wana hitaji umakini mkubwa sana katika kuwatambua na ndiyo maana nimekuwa nikitumia muda mwingi sana kuwaelezea.

Basi kama ilivo kawaida leo tena nakuletea swala mwingine katika makala hii. Hivyo nakusihi uwe na mimi  mwanzo mpaka mwisho wa makala hii.

Katika makala ya leo tutamjua mnyama ajulikanae kwa jina la “NGURUNGURU” au MBUZI MAWE. Kwa lugha ya kingereza mnyama huyu hujulikana kama “Klipspringer”

UTANGULIZI

Ngurunguru ni wanyama jamii ya swala ambao wana sifa mbalimbali za kipekee tofauti na swala wengine. Wanyama hawa ni miongoni mwa swala wenye maumbo madogo sana na hupatikana bara la Afrika tu. Hapa nchini kwetu tumebahatika kuwa na wanyama hawa wengi tu na tunajivunia kuwa na wanyama hawa. Ni wanyama ambao ukifika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti utaweza kuwaona kiurahisi sana.

Wanyama hawa wenye kuvutia wana sifa nyingi sana ambazo zimewafanya kuweza kuishi katika mazingira wanayoishi hasa ukichunguza vizuri wanyama hawa ni miongoni mwa swala wanaoishi katika mazingira magumu sana tofauti na swala wengine.

SIFA NA TABIA ZA NGURUNGURU

Ngurunguru wana manyoa yenye rangi mbali mbali ambapo ukiwachunguza vizuri utaona wana manyoa ya rangi ya njano inayoelekea kuwa kama kahawai au wakati mwigine rangi ya kijivu inayoshabihiana na manjano.

Sehemu ya tumboni kwa chini, kidevu, mdomoni na sehemu za ndani ya masikio wanyama hawa wana rangi nyeupe.

Wana pua nyeusi, kwato nyeusi na sehemu za ncha ya masikio yao wana rangi nyeusi. Ukiwachunguza kwa umakini wanyama hawa utagundua wana matezi yenye rangi nyeusi ambayo yanaonekana pembezoni mwa macho yao.

Tofauti na swala wengine, ngurunguru wana manyoa mengi na yenye umbo kama la chengachenga ambayo ukiyashika hujikunja na kuwa kama rasta. Manyoa haya pia huwa na vitu kama matundu kutokana na jinsi yalivo jipangilia katika miili ya wanyama hawa.

Tofauti na wanyama wengine jamii ya swala, ngurunguru ni wanyama ambao hutembea kwa kutumia ncha za kwato. Hii ni kutokana na mazingira wanayoishi wanyama hawa kitu ambacho kinawasaidia kutembea kwenye maeneo yenye mmawe.

Katika jamii nyingi ni dume pekee ndo huwa na pembe ambazo pia huwa ni fupi na zilizokaa mbalimbali zenye miduara sehemu ya kikonyo. Japo katika baadhi ya spishi chache za wanyama hawa hasa zile zipatikanazo nchi za Tanzania, Uganda na Ethiopia majike yanaonekana kuwa na pembe pia.

Ngurunguru ni wanyama wenye uwezo wa kuona zaidi majira ya usiku. Hutumia muda mwingi wa mchana kupumzika na kipindi cha usiku hufanya shughuli zao hasa chakula na kuhakikisha wanamaliza kula au shughuli zao majira ya usiku mwingi kabla hapajaanza kupambazuka.

Ni miongoni mwa wanyama ambao huishi kwa uaminifu sana kwenye mahusiano. Dume huwa na jike mmoja tu na huishi sehemu moja kwa muda wote hadi pale mmoja wapo atakapo kufa. Unapofika muda wa kula basi mmoja atasimama kuangalia maadui huku mwenzie anakula kisha baada ya kushiba nae atafanya kazi alokuwa anafanya mwenzake kisha nae ale mpaka ashibe.

Wanapo hisi kuna hatari wanyama hawa huwa wana wasiliana kupitia sauti ifananayo ya filimbi au ile ya tarumbeta. Sauti hii hutoka kupitia njia ya pua.

Kutokana na wivu wao wa mahusiano, wanyama hawa huishi kwa kujitenga na ni mara chache sana kukuta kundi kubwa la wanyama hawa.

Dume la ngurunguru huweka mipaka katika himaya yake kwa kutumia njia mbalimbali kama kusambaza kinyesi kwenye mawe katika eneo lake au kuweka maji maji yatokayo kwenye atezi yaliyopo kwenye macho sehemu zenye majani.

KIMO, UREFU NA UZITO WA NGURUNGURU

Kimo=ngurunguru huwa na kimo cha sentimita 43 – 60.

Urefu= wanyama hawa huwa na urefu wa  futi 2.5 – 3.8 huku mkia ukiwa na urefu wan chi 3 – 5.

Uzito=huwa na wastani wa uzito wa kilogramu 8 – 18.

MAZINGIRA

Hupendelea maeneo yenye miamba yenye uoto wa asili wenye majani mafupi mafupi na wakati mwingine katika maeneo yenye kuta za mito. Miongoni mwa sifa zinazo wafanya wanyama hawa kuishi maeneo yenye mawe mawe ni kwato zao ngumu na zenye uwezo wa kuvumilia sehemu ngumu wanazoishi.

CHAKULA

Hawa ni wanyama walao majani na hupendelea kula nyasi, majani, matunda na maranyingi hupendelea majani yenye maji maji mengi sana kwasababu mazingira wanayoishi Wanyama hawa hunywa na maji kidogo sana. Majani ambayo wanapendelea sana ni yale ambayo huwa yanaanza kuota mara tu msimu wa mvua unapoanza. Hutumia miguu ya nyuma kusimama endapo majani yapo juu zaidi na wana uwezo wakupanda miti hadi mita tano kama majani yapo juu zaidi.

Kipindi cha uhaba wa chakula wanyama hawa hulazimika kushuka maeneo ya tambarare kwa ajili ya kutafuta chakula na maji.

KUZALIANA

Kabla ya kupandana dume huanza kupindisha shingo yake na kung’ong’a kidogo kidogo. Maranyingi wanyama hawa hupandana kuanzia mwezi wa nane hadi mwezi wa tisa. Hata baada ya kupandana tofauti na zilivo jamii nyingi za swala, ngurunguru dume huendelea kukaa na jike wake mpaka mtoto anapo zaliwa na kumtunza.

Jike hubeba mimba kwa muda wa miezi sita na baada ya hapo huzaa mtoto mmoja tu. Mara tu baada ya kuzaliwa mtoto hubaki mafichoni hapo sehemu ya miamba au majani kwa muda wa miezi mitatu. Mama hurudi mara tatu hadi mara nne kwa siku ili kuweza kumnyonyesha mtoto. Kazi ya dume ni kumlinda mama na mtoto kwa kuwafukuza ngurunguru wengine au kuwafanya maadui wasisogee karibu na alipo mama na mtoto.

Mtoto huendelea kunyonya hadi afikishapo miezi minne wakati mwingine hadi miezi mitano. Ngurunguru huweza kuzaa afikishapo umri wa miezi saba nakuendelea. Kama mtoto alozaliwa ni wakiume basi huwa pamoja na mama na baba kwa muda wa miezi sita kisha hufukuzwa. Lakini kwa upande wa mtoto wa kike huendelea kukaa na baba na mama hadi muda wa miezi kumi na moja.

Maisha ya ngurunguru katika mazingira asili hukadiriwa kuwa ni miaka 15 japo inasemekana kama anafugwa kwenye bustani za wanyamapori anaweza kuzidi umri huo na kufika hadi miaka 18.

MAADUI WA NGURUNGURU

Katika mazingira asili wanyama hawa wana maadui wengi tu. Maadui hawa kwa mfumo wa kiikolojia tunasema ni lazima wawepo ili kuweza kusawazisha idadi ya wanyama hawa katika mazingira hayo. Endapo maadui hawa hawato kuwepo basi idadi ya wanyama hawa itazidi kiasi kwamba mazingira hayatatosha kutokana na idadi kuwa kubwa. Maadui wa wanyama hawa ni Chui, Fisi, Mondo, Mbweha, Pakapori, Simbamangu, Nyani na Tai.

Huku tukimzungumzia binaadamu kama adui wa nje ambae hana mchango kwenye ikolojia ya wanya hawa hasa kutokana na suala la ujangili.

UHIFADHI

Ngurunguru bado ni wanyama ambao hawajawa hatarini kutoweka duniani kutokana na taarifa zilizo tolewa na shirika la umoja wa mataifa linalo husika na uhifadhi wa maumbileasili (International Union for Conservation of Nature – IUCN). Hii ni kutokana na kuwepo kwa idadi ya kuridhisha ya wanyama hawa na ulinzi hata kwenye Hifadhi za Taifa kama ilivotajwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ni eneo la urithi wa dunia.

Japo kuna taarifa ambazo zinaonesha kuja spishi moja ya wanyama hawa ambayo inapatikana magharibi mwa Afrika ambao wanaitwa ngurunguru wa magharibi wapo kwenye hatari kubwa sana ya kutoweka duniani. Hivyo endapo hawata chukua hatua madhubuti mapema wanyama hawa watatoweka kabisa na itabaki kuwa historia tu katika maeneo hayo.

CHANGAMOTO NA TISHIO KWA NGURUNGURU

Ni jambo la kumshukuru Mungu sana kwani hadi sasa wanyama hawa hawajaripotiwa kuwa na matishio makubwa sana. Hizi ni taarifa zilizo tolewa na IUCN. Shirika hili linasema wanyama hawa bado hawajakumbwa na matatizo sana kwani mazingira ambayo wanaishi yanaonekana hayana thamani kubwa sana kwa binaadamu kitu ambacho kinafanya yasivamiwe sana kwa shughuli za kibinaadamu.

Kitu cha pili ambacho kinasaidia wanyama hawa kuwa kwenye hali tulivu ni tabia ya wanyama hawa kuchagua kuishi sehemu zenye miamba ambazo huwa ni vigumu sana kugombania chakula na mifugo au wanyama wengine walao majani kwani wanakuwa hawana uwezo wa kufika maeneo hayo kutokana na asili ya miamba migumu katika maeneo hayo.

Japo baadhi ya maeneo kero kubwa inayosumbua maisha ya wanyama hawa ni ujangili kitu ambacho kimefanya hata wale wa magharibi mwa Afrika kuingizwa kwenye kundi la wanyama walio hatarini kutoweka duniani kutokana na suala la ujangili.

MUHIMU

Kwa upande wa Afrika magharibi ambao ngurunguru wao wapo hatarini kutoweka wanahitaji kutafuta mbinu mbadala ili kunusuru wanyama hawa. Njia moja wapo ni kuanzisha bustani za wanyamapori ili kuwazalisha wanyama hawa na endapo idadi itaridhisha basi wanaweza kuwaachia tena katika hifadhi zao za taifa. Hili litasaidia sana kurudisha tumaini la uwepo wa wanyama hawa katika maeneo yao.

Suala la pili linalenga hata kwetu pia hapa Tanzania. Japo bado tuna idadi kubwa ya wanyama hawa hasa maeneo ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ila tunahitaji kuimarisha ulinzi wa wanyamapori kutokana na ujangili kwa kuongeza idadi ya askari wa wanyamapori. Hii itasaidia kuongeza doria ya askari hawa katika eneo kubwa kwani ni wazi kwamba askari waliopo ni wachache kitu ambacho ni vigumu kufika kwenye kila eneo la hifadhi zetu.

Ushirikishaji wa jamii katika uhifadhi wa wanyamapori ni kitu muhimu sana na nimekuwa nikikiongelea kwenye makala mbali mbali kwani ndio msingi wa kutambua majangili walipo na maficho yao kwani majangili tunaishinao kwnye makazi yetu. Hivyo jamii ipewe kipaumbele sana katika kuimarisha na kutekeleza dhana ya uhifadhi hapa nchini kwetu.

HITIMISHO

Wanyama hawa wana faida kubwa sana katika mazingira wanayoishi na kwa upande wa pato la taifa kwa ujumla. Kuna watu wanalipa pesa nyingi kwa ajili ya kuja kumuona ngurunguru hapa nchini kupitia sekta ya utalii nakufanya nchi iingize pesa nying sana kutokana na watalii hao. Mbali na suala la utalii, mashirika mbali mbali yanafanya tafiti kupitia wanyama hawa na kulipa pesa nyingi kutokana na tafiti hizo, hivyo hizi ni sababu tosha kwanini tunatakiwa kuwalinda wanyama hawa.

Kabla ya kumtegemea mtu kutoka nje aje kutusaidia kutunza rasilimali zetu za wanyamapori tulizo jaaliwa basi sisi ndio tuwe wakwanza kuonesha mfano katoka kuwatunza wanyama hawa. Kumbka kuna nchi duniani zinatamani hata wangekuwa na ngurunguru 10 tu lakini hawana uwezo wa kuwa na wanyama hawa kutokana na kukosekana kwa baadhi ya mahitaji ya wanyama hawa katika nchi zao.

Unapo muona mnyama anaishi sehemu Fulani basi moja kwa moja ujue kuna mahitaji maalumu ambayo yana mfanya mnyama yule kuishi katika maeneo yale na si sehemu nyingine. Hivyo ni lazima uyatunze mazingira yale kwa ajili ya kumfanya mnyama huyo aendelee kuwepo katika maeneo hayo. Usawa wa ikolojia ni kitu muhimu sana kwenye maisha ya viumbe hai kwani mabadiliko ya ikolojia yanaweza kusababisha viumbe hai jamii fulani kutoweka kabisa katika eneo hilo.

Hivyo kabla na sisi hatuja kumbwa na tatizo la kuwapoteza ngurunguru wetu hapa nchini basi tushikamane pamoja kuwanusuru wanyama hawa ili waweze kuendelea kuishi na kuonywa na vizazi vijavyo. Ni dhambi kubwa sana mbele za Mungu endapo viumbe hawa wata towekea mikononi mwetu kwani waliopita walifanikiwa kuwatunza na ndio maana sisi tumewakuta, sasa kwanini sisi tushindwe kuwatunza kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Hongera na pongezi za kipekee kwa mamlaka mbali mbali kama TANAPA, TAWA,TAWIRI, NCCA na WWF bila kuwasahau WCS kwa kazi kubwa sana mnayo fanya kunusuru maisha ya viumbe hawa na mazingira yao.

Ahsanteni

Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori tuwasiliane kupitia

Sadick Omary

Simu= 0714 116963/ 0765 057969/ 0785 813286

Email= swideeq.so@gmail.com

Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifetanzania

.”I’M THE METALLIC LEGEND”