Habari msomaji wa mtandao wetu wa wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambayo leo tunajifunza njia bora ya kutoa elimu ya uhifadhi kwa watanzania na umma kwa ujumla. Kuna njia nyingi za utoaji wa elimu kwa jamii hasa kupitia mikutano, semina, matangazo mbali mbali, vipeperushi na njia ya usomaji wa vitabu kuhusu uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake. Kila njia ina umuhimu wake na ina matokeo mazuri yanayotarajiwa.

Jambo la utoaji wa elimu kwa jamii ni jambo kubwa na la msingi sana kwenye uhifadhi wa maliasili za nchi. Ndio maana hata tulipokuwa kwenye shule zetu za msingi tulikuwa tunafundishwa kuhusu utunzaji wa maliasili na mazingira, utunzaji na utambuzi wa viumbe hai mbali mbali, hii ni njia ya kuweka kwenye akili za watu umuhimu wa mazingira na maliasili zake. Elimu ya kujitambua na kutambua mazingira imekuwa na msaada mkubwa sana kwa watu, kwa sababu mtu akishajitambua atayaelewa na mazingira yake vizuri. Kwa namna nyingine ni kwamba kama kweli mtu amejitambua ameelimika lazima atakuwa msitari wa mbele kwenye utunzaji wa maliasili na viumbe hai. Huwezi kusema umeelimika wakati unaharibu misitu, unajihusisha na vitendo vya ujangili na kuharibu mazingira na vyanzo vya maji.

Kuna makala moja niliandika siku chache zilizopita kuhusu serikali na wadau wa utalii wapunguze gharama za kutembelea hifadhi, makala hii inaeleza kwa kina faida na dhamira ya kupunguza gharama za watu kutembelea hifadhi za wanyama. Watu watatembelea au kwenda kutalii sio kwa ajili ya kujifurahisha na kuona wanyamapori pekee, lakini watapata somo muhimu sana ambalo litabadilisha fikra zao, somo la uhifadhi na endapo watakuwa na nafasi ya kuingia mara kwa mara kwenye mbuga za wanyama, hii itakuwa ni nafasi yao ya kuutana na wataalamu wa masuala mbali mbali ya uhifadhi wa wanyamapori na watawapa elimu nzuri ya uhifadhi.

Ninaamini katika njia hii sana, kuwapa watu nafasi ya kutalii mara kwa mara ndio njia bora zaidi ya kutuoa elimu ya uhifadhi kwa jamii. Kwa utafiti wangu na kupitia makala ninazoandika naona watu wengi sana wanapenda kutalii, lakini tukiangalia kiuhalisia ni ngumu kumudu gharama za kutembelea hifadhi za wanyama. Kwa sababu sio watanzania wote wana magari, sio wote wanaweza kulipia magari ya kitalii kwa ajili ya kwenda kutalii. Hivyo ingekuwa nafuu endapo gharama zingeshushwa au utafutwe utaratibu mwingine wa kuwafanya watu wengi wapate fursa ya kutembelea hifadhi za wanyama kwa gharama nafuu.

Nafahamu jambo hili la kushusha gharama za kutembelea hifadhi za wanyama linaweza kupokelewa kwa hisia tofauti na wadau wa utalii hasa wenye makampuni ya kibiashara wanaofanya kazi ndani ya hifadhi zetu. Lakini hizi ni maliasili ambazo kila mtu anatakiwa kunufaika, kuzijua, na kuzihifadhi kama inavyotamkwa kwenye sheria na katiba ya nchi yetu. Ukiangalia kati ya wageni wanaokuja Tanzania na wazawa wenyewe ukiwauliza kuhusu hifadhi na wanyamapori wa Tanzania utaona moja kwa moja yule mgeni anafahamu mambo mengi ya hifadhi zetu kuliko watazania wengine. Hili sio jambo ambalo nalipenda sana, watanzania wanatakiwa kujua maliasili zao kwa undani zaidi na kuweza kuzitangaza. Hivyo serikali na wadau wengine wanaonufaika kibiashara kutokan na utalii wakae pamoja na kuja na mpango mzuri unaofanya kazi kwa ajili ya watanzania kutembelea hifadhi zao.

Kama tuna dhamira ya dhati kutoa elimu ya uhifadhi, na kuwafanya watanzania watambue na kuzilinda maliasili zao kwa uzalendo, kitu kikubwa kinachotakiwa kufanyika ni kuwafanya watanzania kuona kabisa uwepo wa rasilimali hizo ni kwa ajili yao na watoto wao. Na jambo hili litafanyika kwa sio kwa kuwapa watu fedha ili kuonyesha kwamba maliasili hizi ni kwa ajili yao. Tuwape fursa zenye nafuu kabisa kutembelea hifadhi za wanyama hata kwa kipindi maalumu, jambo hili likifanyika kwa muda mrefu, hakika tutakuwa na matokeo mazuri. Pia serikali ifikirie kuwa na magari yake kwa ajili ya kuwapeleka hifdhini watanzania kwa gharama nafuu kabisa.

Kupitia njia hii ya kupeleka watu hifadhini tutatengeneza kwenye akili na mioyo ya watanzania upendo, uzalendo wa rasilimali za nchi yetu. Naamini hivi siku zote watu wakifundishwa kuhusu wanyamapori watawapenda na wakiwapenda watawalinda, na hili ndio lengo letu jamii nzima ya kitanzania itambue na kuzilinda maliasili zao, uzalendo unatengenezwa, na hivi ndio tunaweza kuutengeneza, tufikiria jambo hili na tuone namna ambayo tunaweza kutengeneza mazingira mazuri ya watanzania kushriki kwenye maliasili hizi hasa wanyamapori.

Asante sana kwa kusoma makala hii, endelea kujifunza kupitia makala hizi, karibu sana pia washirikishe wengine makala hii na maarifa haya. Nakutakia wakati mzuri na maandalizi mazuri ya kipindi hiki unapofikiria kwenda kutalii au kutembelea kivutio chochote; nitafurahi endapo utanijulisha unapendelea kwenda kutalii wapi msimu huu wa sikukuu na likizo yako, niandikia hapa chini.

Ahsanete sana.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania