Kwa kadri tunavyoendelea mbele na maisha kwenye kila eneo gharama zinaongezeka na hii ni kutokakna na sababu nyingi ambazo zinatulazimu kufanya hivyo. Kimsingi kuna baadhi ya mambo hayatakiwi kuwa tishio endapo kungekuwa na nidhamu na utunzaji wa maliasili tulizopewa na Mungu. Kila siku changamoto zinapotokea na kwenye maisha yetu huwa tunatakiwa kutumia njia nzuri na bora kutatua. Kama vile mwanamahesabu Albert Eistain alivyowahi kusema tatizo linapotokea huwezi kulitatua kwa kiwango kile kile cha ufahamu kilichofanya tatizo hilo, bali inahitajika aina nyingine ya ufahamu wa juu ili kutatua tatizo hilo. Tatizo linapotokea linatakiwa kutatuliwa kwa ngazi nyingine ya ufahamu ya juu zaidi ya hilo tatizo.
Gharama za maisha hazipandi tu kwa sababu zinatakiwa kupanda, hapana, gharama za maisha zinapanda kwa sababu ya maamuzi yetu wenyewe na vitendo vyetu tunavyofanya kila siku. Kwa mfano gharama za uhifadhi wa maliasili zetu zimepanda sana ukilinganisha na gharama za zamani na hii imetokanana na matendo yetu wenyewe binadamu. Kwa sasa serikali na dunia inatumia fedha nyingi sana kuwekeza kwenye kuhakikisha uhifadhi wa viumbe hai na maliasili nyingine unaendelea kuwepo na kuwanufaisha wengine na pia kuhakikisha mazingira na huduma nyingine muhumu za uwepo wa maliasili.
Hapa nimejaribu kuelezea baadhi ya sababu ambazo zinapelekea kuongezeka kwa gharama za uhifadhi kwenye maliasili zetu. Hizi ni sababu ambazo zitaendelea kuwepo na kupanda kila siku endapo hatutabadilika hasa mitazamo yetu kuhusu maliasili na uhifadhi wake. Pia ikumbukwe kuwa sababu hizi sio tu za Tanzania ni sababa ambazo zipo kila sehemu ambazo zina wanyamapori lakini zinatofautiana kiwango, sababu hizi ni kama ifuatavyo;
- Kuendelea kwa vitendo vya kijangili
Kuendelea kwa vitendo vya kijangili kwenye maliasili zetu kumesababisha gharama za utunzaji na uhifadhi wa maliasili kuwa na gharama kubwa kuliko ilivyozoeleka. Katika pembe ya Afirika mashariki na Afrika magharibi na kusini mwa jangwa la sahara kumekuwa na historia ya kusikitisha kuhusu ujangili wa wanyamapori wakubwa kama vile tembo, faru na wanyamapori wengine, jambo hili limesababisha serikali nyingi sana za nchi za Afrika kutumia nguvu nyingi sana na rasilimali nyingi sana za fedha na watu ili kukabiliana na hali hii ya ujangili kwenye maliasili zetu. Kwasababu ya kushamiri kwa vitendo hivyo viovu yameibuka mashrika mengi sana kwenye eneo hili la uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine.
- Mabadiliko ya tabia nchi
Katika ukanda wa Afrika na sehemu nyingine duniani tunaathirika na mabadiliko ya tabia nchi ambayo kwa kiasi ikubwa yamesababishwa na shughuli za kibinadamu kama vile moshi wa viwandani, ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira imechangia kubadiliko kwa hali ya hewa na majira ya mwaka, ambayo imesababisha njaa, ukame na kukauka kwa vyanzo vingi vya maji. Jambo hili linapelekea mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye makazi na mazingira ya wanyamapori. Kwa mfano kukauka kwa vyanzo vikuu vya maji, kama mito na mabwawa makubwa jambo hili linasababisha gharama za kuhifadhi na kuendeleza maliasili kuwa kuwa na gharama kubwa. Hivyo serikali na mashirikia ya kimataifa kuingilia kati hali hii na kusababisha mabilioni ya fedha kunusuru hali hii, kama vile ukarabati wa mabwawa ya maji kwa ajili ya wanyama na pia usimamizi wa shughuli hiyo unagharimu fedha nyingi sana.
- Elimu
Sehemu nyingi ambapo hakuna elimu ya msingi na utambuzi, watu wanatakiwa kujifunza kuelewa umuhimu wa maliasili zao. Jamii nyingi zinazoishi pembembezoni mwa hifadhi za wanyamapori wamekuwa na uelewa mdogo wa faida za wanyamapori kwenye maeneo yao. Kutokana na hali hii kumekuwa na uharibifu wa mazingira na uuaji wa wanyamapori kwenye maeneo haya, na kama kuna jamii za kifugaji ndio kabisaa. Aidha kufuatana na hali hiyo serikali na mashirka ya kimataifa yamekuwa yanatoa elimu ya uhifadhi sambamba na faida zitokanazo na uwepo wa wanyamapori kwenye maeneo yao. Ukiangalia nguvu na gharama inayowekezwa kwenye jamii ili kupata elimu hii ya uhifadhi ni kubwa hivyo kusababisha uhifadhi kuwa na gharama kubwa sana.
- Umasikini
Gharama za uhifadhi zitaendelea kupanda kwa sababu jamii hizi ambazo hukaa karibu na hifadhi hazina maisha mazuri, jamii hizi nyingi ni maskini na zinakabiliwa na njaa kutokana na kukosa chakula cha kutosha kwa ajili ya maisha yao a kila siku, pia kutokuwa na shughuli mbadala za kuingia kipato, jamii hizi ambazo mwazo zilikuwa zinajihusisha na shughuli za ujangili kwa ajili ya mahitaji ya nyumbani, serikali inapokataza shughuli hizi kwenye za ujangili jamii hizi zinzendelea kuwa na mazingira magumu, jambo hili linasababisha migogoro isiyoisha na kushamiri kwa ujangili mkubwa kwenye maeneo ya hifadhi ili kujipatia kipato. Kuokanana hali hii hali ya usalama ya uhifadhi wa maliasili unakuwa mgumu kwa sababu sio majangili tu wanaotaka kuingia kuua tembo bali hata jamii hutegemea maeneo haya kwa ajili ya kuendesha maisha yao ya kila siku.
Kuna vitu vingi sana ambavyo vinachangia sana kukua kwa gharama za uhifadhi, kuna wakati nafikiria kama kungekuwa hakuna ujangili kwenye maliasili zetu, nchi nyingi za Afrika zingekuwa zimepiga hatua kubwa sana kwenye maeneo mengine ya maendeleo na faida nyingi zinatokana na uwepo wa wanyamapori zingekuwa na uwezo mkubwa wa kutawanywa sehemu nyingine ili kuinua maendeleo ya jamii kiuchumi na maeneo mengine muhimu. Kwa jinsi mambo yanavyoenda utafikiri tunalipia uwepo wa wanyamapori na maliasili ulizopewa na Mungu katika nchi zetu. Tunazalisha fedha nyingi kutokana na uwepo wa wanyamapori lakini hapo hapo tunazitumia fedha hizo nyingi kwa ajili ya kuhakikisha maliasili hizo zinaendelea kuwepo. Tena wakati mwingine gharama za uhifadhi zinakuwa kubwa kuliko faida tunazopata au tunazotegemea kupata.
Kati ya sababu nilizotaja hapo juu kwamba zinasababisha gharama za uhifadhi kuwa juu na kuendelea kupanda ni ujangili. Ujangili unasababisha gharama kubwa kwenye hifadhi zetu, endapo ujangili utapungua au utaondoka tutakuwa na gharama kidogo na manufaa makubwa kutokana na uwepo wa maliasili. Fikiria wakati mwingine tuanaingia gharama za kutumia mpaka ndege kufanya doria kwenye hifadhi zetu. Maeneo yetu na mazingira yetu yakitunzwa vizuri, maliasili zikihifadhiwa na kila mtu, ujangili ukiondoka tutapunguza gharama za kuhifadhi maliasili zetu, na pia tutapunguza hatari za askari wanyamapori wanofanya dori kwenye maliasili zetu.
Asante sana kwa kusoma makala hii, mshirikishe mwenzako makala hii. Nakutakia mapumziko mazuri ya sikukuu na mwaka mpya.
Shiriki pamoja nasi kupiga vita ujangili kwenye maliasili zetu.
Ahsanete sana.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569