Habari ndugu msomaji wa makala za Wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambayo tunazungumzia kazi kubwa inayohitajika ili kuweka mtazamo chanya wenye matokeo chanya kwa jamii zetu. Baada ya kufundishwa, baada ya kujifunza, baada ya kuona, baada ya kukubali na kuridhia kinachofuata ni matokeo, na hapa matokeo yanaweza kuwa hasi au chanya. Lakini namini kwa juhudi na mbinu nzuri matokeo lazima yawe chanya.SOMA HAPA Jamii Itaendelea Kuthamini Kuheshimu Na Kulinda Kile Kinachowaletea Faida

Baada ya shughuli pevu ya uanzishwaji wa maeneo ya hifadhi ya jamii, vijiji viliridhia kila jambo na kila hatua nasasa vinasubiri matokeo ya uwepo wa rasilimali na matokeo wanayotarajia. Kwa kweli sio jambo jepesi hata kidogo kuanzisha na kutegemea matokeo mazuri kwa mara moja kwenye jambo kubwa kama la kuanzisha asasi za wanyamapori na maeneo yao mengine muhimu.

Baada ya kuandika makala ya jana na juzi zinazohusu masuala ya WMA au maeneo ya hifadhi ya jamii nimegundua kuna mambo mengi ambayo watanzania wengi hawayafahamu kwenye uanzishwaji wa maeneo haya. Wengi wanafikiri maeneo haya ni ya TANAPA, wengine wanafikiri ni kwa ajili ya baadaye ili yaje kuwa hifadhi au mapori ya akiba. Sio kweli kabisa maeneo haya ni maeneo yaliyowekwa mahususi kwa ajili ya jamii kuyasimamia na kupata faida kutokana na uwepo wa maliasili zilizopo kwenye maeneo haya.

Kama kichwa cha habari hapo juu kinavyoeleza kuwa kazi kubwa bado inahitajika ili kuyafanya maeneo haya kuwa yenye manufaa kwa jamii. Maeneo haya yanahitaji kufanyiwa utafiti na upembuzi yakinifu, yanahitajika kutangazwa ili kuyafanya yajulikane kwa wawekezaji na wafanyabiashara. Hili ndilo jambo kubwa kabisa kwa uanzishwaji wa maeneo haya ambapo jamii inatakiwa kupata faida za kiuchumi na mapato ya fedha kutokana na miradi ya kibiashara iliyopo kwenye maeneo hayo.

Kwenye hatua za uanzishwaji wa maeneo haya ya hifadhi ya jamii kuna hatua ya sita na ya saba ambapo hatua ya sita inasema baada ya kuitangaza na kuifanya WMA kutambulikana kisheria na jamii kupata kibali cha kutumia wanyamapori hatua ya sita ni kushirikiana na wawekezaji ili kuandaa miradi ya kibiashara yenye tija kwa jamii, hili ndilo jambo la msingi na muhimu ili maeneo haya yawe na mapato kwa jamii. Lakini hatua ya mwisho au ya saba katika hatua za uanzishwaji wa maeneo haya ni ufuatiliaji, haitoshi tu kuwa na WMA inafaa sana kukawa na utaratibu wa wazi na unaojulikana wa kufuatilia maendeleo na changamoto zinazoikabili WMA hizi, na jambo hili linatakiwa kufanyika kwa kutumia watalaamu, washauri na watu wenye weledi kwenye maeneo haya.

Hivyo basi wale viongozi na wasimamizi wa maeneo haya ya hifadhi ya jamii kazi kubwa sana ipo mbele yenu kuhakikisha WMAs zinaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa jamii, ili maeneo haya na rasilimali zilizopo humu zilete mtazamo chanya wa uhifadhi na utunzaji endelevu wa maeneo haya. Hivyo basi inahitajika kazi mipango, kazi ,mipango, kazi mipango hadi kieleweke.

Ahsante sana

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania