Kwaheri mwaka 2017 karibu mwaka 2018, kuna mengi yaliyokuwa yanafanyika hapa duniani katika kipindi hiki cha kuangana na mwaka 2017, kuna watu binafsi waliokuwa wanafanya mamuzi na maazimio ya kubresha maisha yao kwa mwaka mpya wa 2018, kuna makampuni yaliyokuwa yanajipanga namna ya kuongeza faida na kutoa huduma bora kwa wateja wao, lakini pia kuna maazimio na ahadi nyingi zilizokuwa zimeahidiwa kwamba kabla ya mwaka 2017 kuisha zitafanyika. Hivyo mwishoni mwa mwaka ukimuuliza mtu yeyote mipango yake anayotarajia kufanikisha kwa mwaka ujao asilimia karibu 70 watakuwa na mipango mizuri na watakwambia jinsi watakavyoanza mwaka mwingine kwa kishindo. Hivi ndivyo watu wanavyomaliza na kuanza mwaka mwingine sehemu nyingi hapa duniani.

Tukiachana na mambo ya kuanza na kumaliza mwaka, hebu twende kwenye upande wa maliasili zetu hasa hapa barani Afrika, hakuna siku imekuwa nzuri sana kwa wahifadhi wa wanyamapori kama jinsi mwaka 2017 ulivyoisha. Jinsi mwaka 2017 ulivyoisha ni kama vile ujangili umeisha katika bara la Afrika, hasa ujangili wa tembo na faru. Kwa kweli ni kipindi ambacho kilikuwa kinasubiriwa kwa hamu sana na mataifa mengi, watu binafsi na mashirika mengi ya uhifadhi wa wanyamapori katika bara la Afrika na sehemu nyingine duniani. Kilio cha tembo, ujangili na juhudi kubwa inayotumika kupiga vita ujangili wa tembo, kila utafiti ulifanywa, kila serikali ilichunguzwa, kila biashara ilipelelezwa, Afrika yenyewe ilizungukwa na miradi mingi sana ya uhifadhi, kampeni nyingi zimefanyika ili kujua chanzo kikuu cha ujangili, na namna ya kuondoa au kupunguza ujangili wa tembo, taarifa na takwimu zilizokuwa zikitolewa na taasisi mbali mbali za utafiti wa mambo haya ulileta hofu kubwa sana kwenye uhifadhi wa wanyama hawa jambo ambalo lingeachwa bila kufanyiwa kazi tungebaki na historia kwamba tulikuwa na wanyama wanaoitwa tembo kwenye nchi zetu.

Katika kutafuta mchawi nani kwenye vita hivi, kila mtu aliinyooshea nchi ya China kidole kuwa wao ndio wamekuwa msitari wa mbele kusababisha ujangili kushamiri katika bara la Afrika. Nchi ya China ndio yenye masoko makubwa sana na ya muda mrefu yanayonunua meno ya tembo na pembe za faru. Na sio tu walikuwa wanunuzi pia walikuwa na viwanda vya kutengeneza vitu ambavyo hutokana na meno ya tembo na pembe za faru. Hivyo kwa kuwa mahitaji ya soko ni makubwa basi jambo hili lilipelekea kushamiri kwa vitendo vya kijangili kwenye bara la Afrika. Kutokana na taarifa ambazo zipo kwenye gazeti maarufu la National Geographic, inaonyesha uwepo wa biashara hii ya mano ya tembo umesababisha tembo 30,000 kuwawa na majangili kila mwaka kutoka katika bara la Afrika. Hili ni janga kubwa sana ambalo lilikuwa linapelekea kupotea kwa tembo wa Afrika kwa kipindi kifupi sana cha baadaye.

Aidha baada ya kujua kuwa nchi ya china ndio kiini na ndio wanaochochea kwa kiasi kikubwa kuwawa kwa tembo, ilibidi juhudi za makusudi zianze kuchukuliwa serikali, watu binafsi, mashirika na nchi ziliungana na kutoa sauti yao juu ya masoko ya biashara ya meno ya tembo huko China yanakuwa ndio kichocheo cha kuthorotesha juhudi za uhifadhi wa wanyama hawa. Hivyo baada ya kilio cha muda mrefu nchi ya China ikakubali kufunga masoko yake halali ambayo yalikuwa yanafanya biashara hii kwa muda mrefu, katika maazimio ya mapema mwaka 2017, nchi ya china ilikubali kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2017 itafunga kabisa masoko ya meno ya tembo kwenye nchi hiyo, na jambo hili ndilo lililofanyika jana tarehe 31/12/2017. Baada ya kutangaza kufunga masoko yake makubwa na viwanda vyao vilivyokuwa vinazalisha bidhaa za meno ya tembo, hii ikawa ndio taarifa nzuri na yenye matumaini makubwa kwa tembo wa Afrika, maana kutangazwa kufngwa kwa masoko yao ni kama kutangaza mwisho wa ujangili katika bara la Afrika na sehemu nyingine duniani.

Licha ya kuwa biashara ya Kimataifa ya meno ya tembo ilifungwa na kuzuiwa tangu mwaka 1990, lakini bado kuna nchi nyingi ambazo ziliendelea na biashara hiyo ya meno ya tembo kwenye nchi zao, kati ya nchi hizo ni Marekani na China, hivyo nchi hizi ziliamua kuendelea na biashara hii kwenye nchi zao wenyewe. Lakini ilipofika mwaka 2015 Rais wa Marekani Barack Obama na Rais wa China Xi Jinping waliamua kufanya maazimio makubwa na magumu ya kufunga na kuzuia kabisa biashara ya meno ya tembo ndani ya nchi zao. Na hii ilitokana na ongezeko la kupungua kwa idadi ya tembo hasa kwenye bara la Afrika. Baada ya kufanya maamuzi hayo kila mmoja alibaki na jambo moja kubwa la kufanya, ambalo lilikuwa ni utekelezaji wa maazimio yao ya kufunga biashara hiyo haramu. Mnamo mwaka 2016 Marekani ikaamua kuanza utekelezaji wa mazimio waliyokubaliana na China na ilipofika mwezi wa sita mwaka 2016, Marekani ilipitisha sheria ya kufunga kabisa kuuza na kununua ya meno ya tembo kwenye nchi yao isipokuwa yale meno ya zamani kabla ya mwaka 1990 na hivyo ndivyo walivyofanya, na kazi ikwawa imebakia kwa nchi ya China kusimamia na kutekeleza maamuzi na makubaliano yao.

Haikuchukua muda China nayo ikajitokeza hadharani mwanzoni mwa mwaka 2017, na kutangaza kufuata nyayo za nchi ya Marekani kufuta biashara ya meno ya tembo na kufunga kabisa vinu au viwanda vya kutengenezea bidhaa za meno ya tembo, hii ndo jambo lililokuwa likisubiriwa kwa mwaka mzima wa 2017 na ndio jana wakaamua kuvunja ukimnya na kutangaza nia yao na dhamira yao ya kutoendelea na biashara hiyo. Na jana hiyo hiyo walifunga zaidi ya maeneo 67 ambayo yalipewa lessseni ya kuendesha biashara hiyo. Hili ndilo jambo la kishujaa na linapongezwa na watafiti na wahifadhi wengi wa wanyamapori popote duniani.

Sasa tuwaache tembo wetu wapumue, naamini hatua zilizochukuliwa zitaleta auheni kwenye hifadhi za wanyamapori na pia utulivu kwenye maeneo ya wanyamapori. Maana watu walipoteza maisha kwa sababu ya kuuwawa na majangili waliotaka kuua tembo. Hivi ndivyo tunavyotakiwa kushirikiana hapa duniani kwani uwindaji na ujangili wa meno ya tembo ulikuwa ni kwasababu ya watu wachache ambao wanataka kuishi maisha ya anasa na kuonekana matajiri na wenye heshima kwa jamii jambo ambalo sio la msingi wala halina umuhimu wowote.

Tutendelea kujifunza na kufahamishana kuhusu mambo yaha, leo niishie hapa, naamini umepata kujua baadhi ya mambo na utajua juhudi na kazi kubwa inayofanywa na serikali, wadau wa mazingira na wahifadhi kwa ujumla wao ili kuokoa na kupigania uwepo wa wanyamapori kwenye hifadhi zetu. Tukutane kwenye makala ijayo.

Nakutakia Kheri Ya Mwaka Mpya 2 018 Wenye Mafanikio Makubwa.

Asante sana.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania