Biashara yoyote ili iendelee kudumu na kufanikiwa lazima kuwe na pande mbili, upande wa kwanza ni wateja au wanunuzi wa bidhaa na upande wa pili ni wauzaji wa bidhaa hiyo, upande mmoja ukikosekana hapo upande wa pili hauwezi kusimama na kuendelea kwa sababu kila upande unategemea uwepo wa upande mwingine. Kwa lugha ya kibiashara tunazungumza ili biashara iwe endelevu lazima kuwa na wateja au wanunuza au soko na pia kuwe na wauzaji au upatikanaji wa bidhaa ambayo inahitajika na wateja. Hivyo ndivyo ilivyo kwenye biashara yoyote hapa duniani, haijalishi biashara hiyo ni halali au sio halali,  uwepo wa pande mbili ndio unaowasukuma watu kufanya biashara hata katika mazingira magumu na hatarishi.

Katika barua ya leo nitazungumzia kwa uchache jambo hili ili kwa namna moja au nyingine iweze kutusaidia kufikia lengo la kandika barua hii. Lakini barua hii nimeiadika kutokana na matukio yaliyotokea siku chache zilizopita kwenye upande wa maliasili zetu, pale ambapo nchi ya China iliporidhia kufunga masoko yake ya ndani ya biashara ya meno ya tembo. Hapo ndipo nilipopata wazo hili baada ya kusoma majarida na habari mbali mbali kutoka kwa watalaamu wa masula ya wanyamapori, wahifadhi, watu binafsi, mashirika makubwa ya uhiafdhi wa wanyamapori na mazingira, na pia hata kauli za viongozi wakubwa duniani kuhusiana na uamuzi wa China kufungia na kuzuia biashara ya meno ya tembo kwwenye nchi iyo.

Ukweli ni kwamba endapo China ingeendelea na biashara hii hata kama ilikuwa inafanyika kihalali katika nchi yao, bado hali ingekuwa mbaya sana kwa upande wa maliasili zetu kama vile tembo, kwa sababu endpo soko lipo basi kwa namna yoyote ili iwe halali au isiwe halali lazima kungekuwa na uhitaji wa bidhaa kwa ajili ya kufanya soko liendelee, na jambo hilo ndio lingepelekea kupotea na kuuwawa kwa tembo hasa kwa bara la Afrika. Hivyo baaada ya kufungwa kwa viwanda na vinu vya kutengenezea bidhaa za meno ya tembo na masoko mengi kumeleta ahueni kwa wapenzi wengi wa wanyamapori uhifadhi na mazingira. Jambo hili la ufungwa kwa biashra hii kumeleta faraja na matumaini makubwa sana kwa tembo wa Afrika, na kwa kufanya hivyo biashara hii itasimamisha uwindaji na uuaji wa tembo hivyo kwa kiasi kikubwa kuna matumaini ya kupungua au kuisha kwa ujangili wa tembo.

Hayo ndio mambo makubwa yaliyotokea ndani ya siku chache tangu mwaka huu kuanza. Wataalamu wa mambo wanasema mwaka 2018 umeanza vizuri kwa upande wa wanyamapori kama tembo na wengine kama vile faru. Kuna link nitaziweka hapa ili ufungue na kusoma baadhi ya makala nilizoandika kuhusu uamuzi wa China kusimamisha biashara ya meno ya tembo. Makala hiyo inaeleza pia hatua za nchi ya Marekani kuanza kuchukua hatua hizo mapema mwaka 2016, baada ya hapo ndipo China nayo ikafuata nyayo za Marekani.

SOMA MAKALA HII KUJUA ZAIDI; Tumaini Kubwa Kwa Tembo Wa Afrika

Kwenye barua hii nimeelezea kusimamishwa na kufungwa kwa masoko ya biashara ya meno ya tembo huko China kunavyoleta matumaini ya kupungua au kuisha kwa ujangili kwa bara la Afrika. Lakini nataka niende mbali kidogo kugusia wanyamapori wengine na wanaofanya biashara haramu kwamba endapo kutakuwa na watu wanahitaji bidhaa hizi basi biashara haitaisha. Ndio maana biashara ya madawa ya kulevya ni ngumu kuisha kwasababu bado masoko na watu wanazitumia, endapo kungekosekana wateja basi biashara hiyo isingeweza kuendelea. Hivyo hivyo kwa bishara nyingine kama vile za usafirishaji wa miti au mimea ambao ipo hatarini kutoweka au wanyama au hata wadudu. Njia nzuri ya kufunga biashara haramu zote ni kufunga masoko yake.

Aidha, bila kufanya hivyo tutatumia nguvu nyingi sana na rasilimali nyingi sana kama vile fedha kupambana na ujangili kwenye hifadhi zetu. Pia kumekua na janga kubwa sana kwenye uhifadhi wa maliasili zetu ambalo linadhorotesha juhudi kubwa za kupambana na ujangili na kuwafanya watu na jamii zinazoishi kwndo ya maeneo ya hifadhi kushindwa kuona na kupata faida, janga hili ni rushwa,  rushwa imedhoofisha sana jitihada na nguvu za watu wengi kupambana na ujangili, maendeleo mengi yamekwama kwa sababu ya kukosekana kwa haki na usawa, wanajamii wanashindwa kuona faida kutokana na maliasili zao kwasababu ya uwepo wa rushwa kwenye maeneo yao na ngazi za juu. Hivyo naamini kufungwa kwa masoko haya ya meno ya tembo kutapunguza pia uwepo wa rushwa kwenye maliasili zetu.

Hivyo, naipongeza sana Nchi ya China kwa uamuzi wa busara walioufanya kufunga masoko ya biashara ya meno ya tembo. Pia napongeza jitihada za serikali zetu, mashirika na watu binafsi kwa juhudi kubwa waliyokuwa nayo kuhakikisha dunia inatambua kuwa ujangili wa tembo na viumbe hai wengine unaleta madhara sio tu kwa tembo kupungua bali kwenye makazi na usawa wa kolojia ambayo inajumuisha mamlioni ya viumbe hai ambayo na binadamu yupo ndani yake.

Asante sana kwa kusoma makala hii, karibu kwa makala nyingine.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania