Leo tena nimekuandalia makala nzuri yenye kuvutia ambayo inamuhusu mnyama jamii ya swala ambae kwa hakika wengi wetu hatumfahamu na kama tunamfahamu basi huwa tunamchanganya na jamii nyingine sa swala. Jambo la kustajaabisha nikwamba idadi kubwa ya wanyama ambao nitakuelezea katika makala hii wanapatikana hapa nchini Tanzania na hasa katika eneo moja hivi ambalo hata wewe huwezi kuamini kutokana na eneo hilo kuwa na shughuli nyingi za kijamii lakini bado wanyama hao wameendelea kuwepo katika eneo hilo.

Turudi nyuma kidogo angalau tujikumbushe kidogo kuhusu jamii za Wanya hawa waitwao swala kwani kuna aina nyingi sana za swala ambazo wengi wetu hatuzijui. Wapo baadhi wanawafahamu swala paa tu kuwa ndio swala kumbe kuna swala wengi tu katiika hifadhi zetu za taifa na maeneo mengine ya hifadhi za wanyamapori. Miongoni mwa swala wapatikanao hapa nchini ni pofu, nyamera, swala paa, tandala wakubwa, tandala wadogo, mbuzi mawe, swala tomi, kuro na wengine wengi tu.

Katika makala ya leo tutamjua swala aitwae SHESHE kwa jina lingine ni PUKU. Hivyo nakusihi uwe Pamoja nami katika makala hii mwanzo mpaka mwisho ili uweze kujifunza mambo mengi kuhusu mnyama Puku kwa Nyanja mbali mbali kama sifa za mnyama huyu, tabia, kuzaliana kwao, maeneo wanayo patikana wanyama hawa bila, uhifadhi wao na changamoto wanazo kutananazo wanyama hawa katika mazingira yao asilia.

UTANGULUZI

Sheshe ni wanyama jamii ya swala ambao wanapatikana barani Afrika tu na si kwingineko. Ni swala wenye umbo la kawaida ambao wanavutia sana kuwatazama. Wanyama hawa kwa asilimia kubwa wanapatikana katika maeneo tengefu ya hifadhi za wanyamapori na maeneo mengine yaliyopo chini ya usimamizi wa maliasili sehemu mbali mbali. Mbali na kuwa wanyama hawa wanapatikana barani Afrika tu, lakini ukweli ni kwamba wanapatikana katika nchi chache sana barani Afrika na hasa katika nchi zilizopo kusina mwa jangwa la Sahara.

Sheshe wana sifa kemkem ambazo zinavutia hasa kutokana na maumbile na namna rangi zilivyo pangika katika miili yao. Zipo changamoto mbali mbali wanazo kutananazo wanyama hawa ambazo kwa zaidi ya asilimia 85 ni shughuli za kibinaadamu na kupelekea idadi ya wanyama hawa kupungua katika maeneo yao asilia. Pamoja na chnangamoto hizo lakini mamlaka mbali mbali zinapambana ili kuhakikisha wanyama hawa wanaendelea kuwepo katika hifahi zetu za taifa na maeneo mengine tengefu ya hifadhi za wanyamapori bila kusahau na maeneo ya misitu.

Nijambo la kujivunia kuwa na wanyama hawa hawa Hapa nchini Tanzania na kwa takwimu za tafiti mbali mbali zinaonesha kuwa idadi kubwa ya wanyama hawa wanapatikana hapa nchini. Ikumbukwe kuwa wanyama hawa wapo hatarini kutoweka duniani hivyo inahitajika nguvu kubwa sana kuhakikisha wanyama hawa wanaendelea kuwepo na idadi yao kuongezeka kama ilivyokuwa happo awali.

SIFA NA TABIA ZA SHESHE

Sheshe ni wanyama wenye maumbile ya kawaida wenye rangi ya udongo au dhahabu huku sehemu ya tumboni wakiwa na rangi nyeupe inaypo ng’aa au kuonekana kama imepauka. Manyoa ya wanyama hawa yanakadiriwa kuwa na urefu wa 32 mm.

Wana miduara myeupe kwenye macho na rangi nyeupe sehemu ya shingoni na sehemu ya mdomo wa juu japo sifa hii pia unaweza kuikuta kwenye baadhi ya jamii nyingine za swala. Sheshe wanakosa alama usoni na miguuni kama zilivyo jamii nyingi za wanyama aina ya swala.

Sehemu ya nyuma ya masikio yao wana rangi ya dhahabu huku ncha za masikio zikiwa na rangi nyeusi.

Mikia yao ina manyoa marefu kuelekea nchani na manyoa haya hayajachambuka. Hii ni moja kati ya sifa kubwa ambayo inawatofautisha sheshe na jamii nyingine za swala ambazo zinafanana kwa kiasi kikubwa sana sehemu ya mikiani.

Maranyingi hupendelea kufanya shughuli zao majira ya jioni wakati jua linaanza kuzama japo kuna wengine huendelea kula hata wakati wa usiku.

Sheshe wanapo pata mshituko hukimbia umbali mfupi kisha husimama na kuangalia ni nini kimetokea katika eneo hilo. Mawasiliano hufanyika kwa njia ya sauti itokayo kama mluzi au filimbi.

Madume tu ndo huwa na pembe ambazo huwa nene na zenye miduara kwa chini ambapo kadri zinavyo elekea juu miduara ile huenda inapotea. Pembe hizi huwa na wastani wa urefu kati ya sentimita 40 japo kuna ambao pembe hurefuka hadi kufikia urefu wa sentimita 52.

Majike na Watoto huwa wanaishi kwenye kundi ambalo wanawezakuwa kati ya 6-20 na wakati mwingine idadi inaweza kuzidi hapo.

Madume huishi kwa kujitenga na maranyingi dume mtawala wa himaya ambayo inakuwa na majike huwa na monekano wa shingo kubwa kuliko madume wengine lakini kwa Pamoja wote wana matezi sehemu ya shingoni. Dume mtawala hutumia matezi hayo kusambaza harufu katika mipaka ya himaya yake ili kuzuia madume wenguine wasiingie katika himaya hiyo.

Mbali na usambazaji wa harufu kwenye mipaka, madume pia hutioa sauti zenye mfanano wa filimbi au miluzi ili kuwatishia madume wengine wasisogee katika himaya zao na hutoa sauti hii mara tatu hadi nne kila baada ya dakika 30. Sauti hii pia hutumika katika kuvutia majike hasa unapokaribia msimu wa kuzaliana japo tafiti zinaonesha kuwa wanyama hawa huzaliana karibu kila majira yote ya mwaka.

KIMO, UREFU NA UZITO WA SHESHE

Kimo; Sheshe mkubwa hufikia kimo cha sentimita 90.

Urefu; Wanyama hawa huwa na urefu wa wastani kati ya sentimita 126-160 huku mikia yao ikiwa na urefu wa sentimita 30.

Uzito; Uzito hutofautiana kati ya madume na majike. Madume wakubwa huwa na uzito kati ya kilogramu 67-91 huku majike wakiwa na uzito kati ya kilogramu 48-78.

MAENEO WAPATIKANAYO SHESHE

Mwanzo wa makala hii hapo juu niligusia kidogo tu maeneo ambayo unaweza kuwakuta wanyama hawa hasa katika mazingira yao asilia. Sheshe wanapatikana bara la Afrika tu na si kwingineko. Lakini pia ni nnchi chache sana hapa barani Afrika ambazo zinajivunia uwepo wa wanyama hawa huku Tanzania tukiwa tunaonmgoza kwa idadi kubwa ya wanyama hawa.

Nchi wanazo patikana wanyama haw ani Tanzania, Angola, Namibia, Botswana, Malawi, Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo na Zambia. Kwa taarifa zaidi kuhusu idadi ya wanyama haw abasi fatilia makala hii hadi kwenye sehemu ya uhifadhi utajifunza mengi kuhusu hali ya wanyama hawa hapa nchini na kwingineko barani Afrika.

MAZINGIRA

Sheshe wanapatikana sana kwenye maeneo yenye majani mengi, Savana na kwenye maeno ya mito ambayo yamekuwa na mafuriko madogo madogo ya mara kwa mara. Mabadiliko ya hali ya hewa (jotoridi na misimu ya mvua) huchochea wanyama hawa hukama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Mfano kipindi cha mvua wanyama hawa hupendelea sana kwenda maeneo yenye miinuko ambayo inakadiriwa kuwa na urefu wa mita 900 hadi 1550 kutoka usawa wa bahari.

Kipindi cha kiangazi wanyama hawa hupendelea kwenda kwenye maeneo yenye vyanzo vya maji ya kutosha ambayo maranyingi yapo chini kidogo kulinganisha na miinuko ambayo huwa wanakwenda kipindi cha majira ya mvua.

CHAKULA

Kama walivyo swala wengine, chakula pekee cha wanyama haw ani majani na wana uwezo wakula majani ya aina mbali mbali. Mjani au mimea wanayo pendelea wanyama haw ani ile yenye kiwango kikubwa cha protini ghafi na yenye uwezo wa kuishi hadi myaka miwili. Sheshe hutumia muda wao mwingi kwenye kula kuliko shughuli nyingine.

KUZALIANA

Sheshe huzaliana majira yote yam waka japo maranyingi majike hubeba mimba kipindi cha mwisho cha mvua kubwa za mwanzoni msimu wa mvua. Majike wote huwa chini ya dume mtawala wa himaya na dume mmoja huweza kupanda majike wote kwenye kundi. Japo baadhi ya tafiti zimefanyika na kuhakiki kuwa majike huchagua madume wayatakayo wenyewe. Mara chache sana dume mtawala huvumilia uwepo wa madume wengine endapo tu hawatoonesha hali ya kuhitaji kuwapanda majike katika himaya yake.

Baada ya kupandwa, jike hubeba mimba kwa muda wa miezi 8 na huzaa mtoto mmoja tu. Huwa ni ngumu sana kuwaona watoto wa sheshe kwasababu ni wazuri kwenye kujificha kwasababu majike huwa hawana matunzo mazuri sana kwa watoto na kulazimika kuwaacha wenyewe mafichoni kisha kurudi kuwanyonyesha kwa vipindi mbali mbali. Uwepo wa majani marefu husaidia sana watoto kujificha lakini pia chakula cha kutosha kwaajili ya kina mama wanao nyonyhesha. Mtoto hunyonya kwa muda wa miezi 6 na huwa tayari kuzaliana wafikishapo umri wa miezi 12 hadi 14. Ndama ambao tayari wameshakuwa hutoka mafichoni kisha kujiunga na kundi la kina mama ili kuendelea na maisha ya kila siku.

Umri wa kuisha kwa sheshe ni kati ya myaka 17-18 wawapo katika mazingira yao asilia japo umri wa kuishi unaweza kuongezeka kama wanafugwa katika bustani za ufugaji wanyamapori.

UMUHIMU WA SHESHE

Umuhimu wa wanyama hawa tunaweza kuugawanya katika maeneo mawili tofauti.

Kwanza kabisa ni upande wa ikolojia; Sheshe ni wanyama walao majani hivyo husaidia sana kwenye urekebishaji wa uotaji wa majani katika mazingira kutokana na namna wanavyokula kwenye maeneo mbali mbali. Lakini pia husaidia kufanya idadi ya wanyama walao nyama iendelee kuwa ya kuridhisha kwani huwawinda kama chakula.

Pili wanyama hawa wana faida kubwa sana kwa binaadamu kwani sheshe ni miongoni mwa wanyama wawindwao kama kitoweo hasa kwa kufuata sheria na kanuni za vibali vya uwindaji. Watu hupata nyama lakini pia baadhi ya sehemu za wanyama hawa kama ngozi, pembe na kwato hutumika kama mapambo. Faida nyingine apatayo binaadamu kutokana na wanyama haw ani upande wa utalii. Wageni mbali mbali wanatembelea maeneo ya hifadhi za wanyamapori kwaajili ya kuwaona wanyama hawa hivyo kuwa kivutio kizuri tu cha utalii na kupelekea taifa kuingiza fedha nyingi za kigeni kupitia utalii. Wenyeji pia ambao wanaishi pembezoni mwa hifadhi za taifa na maeneo mengine tengefu ya hifadhi za wanyamapori pia hunufaika kupiotia shughuli za kitalii zinazo endlea katika maeneo yao.

UHIFADHI

Katika maeneo ambayo huwa nasisitiza sana kusoma kwa umakini ndugu msomaji wa makala hizi basi huwa ni sehemu hii ya uhifadhi kwani hapo ndo tunapata mwanga na ufahamu zaidi kuhusu wanyamapori hususani hapa nchini kwetu Tanzania na kujua uelekeo wa wanyama hawa. Hivyo nakuomba usome kipengele hiki kwa umakini zaidi.

Kutokana na taarifa za shirika la umoja wa mataifa la uhifadhi wa maumbileasili (International Union for Conservation of Nature- IUCN), idadi ya wanyama hawa inakadiriwa kuwa 130,000 tu na wanazidi kupungua sana hali ambayo imepelekea wanyama hawa waingizwe kwenye kundi la wanyama lililo karibia kwenye hatari ya wanyama wanao karibia kutoweka duniani.

Katika idadi hiyo, hapa nchini Tanznia tunajivunia kuwa na idadi kubwa ya wanyama hawa ukilinganisha nan chi nyingine. Tafiti zinaonesha kuwa Tanzania ina jumla ya sheshe 54,600 ikifuatiwa na Zambia ambayo ina sheshe wapatao 21,000. Idadi ilobaki wanapatikana katika nchi nyingijne kama ambavyo nimeziorodhesha hapo juu kwenye kipengele cha maeneo wapatikanayo sheshe. Mfano nchini Botswana tafiti zinaonesha kuwa idadi ya sheshe kwa nchi nzima hawafiki hata 100 na idadi inazidi kupungua siku baada ya siku. Hali ikiendelea hivi basi wanyama hawa watatoweka kabisa nchini Botswana.

Hapa nchini Tanzania wanyama hawa wanapatikana kwa wingi katika bonde la Kilombero. Asilimia 75 ya wanyama jamii ya sheshe duniani wanapatikana katika pori tengefu la hifadhi ya wanyamapori la Kilombero ambalo lipo chini ya mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori hapa nchini (Tanzania Wildlife Management Authoritty-TAWA). Japo tunaongoza kwakuwa na idadi kubwa ya wanyama hawa kuliko nchi nyingine, bado idadi ya wanyama hawa inazidi kupungua kutokana na changamoto mbali mbali ambazo tutazielezea kwenye vipengele vinavyo fuata.

MAADUI ASILIA WA SHESHE

Katika mazingira asilia ya wanyama hawa, madui wakubwa ni simba na chui. Mbali na simba na chui adui mkubwa kabisa ambe sio asilia nah ana mchango kwenye ikolojia kwa wanyhama haw ani binaadamu. Shughuli za binaadamu zimekuwa mwiba wenye uchungu sana kwenye ustawi wa uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini na kwingineko duniani kote.

CHANGAMOTO ZINAZO WAPATA SHESHE KATIKA MAZINGIRA YAO

Kama walivyo wanyama wenguine jamii swala, sheshe wanakumbwa na changamoto nyingi sana ambazo zinapelekea idadi yao kupungua kwa kasi katika maeneo wapatikanayo. Changamoto zote hizo kwa zaidi ya asilimia 95 zinatokana na shughuli za kubinaadamu ambae kama nilivo dokeza hapo juu kuwa ndo mwiba mkubwa kwa wanyama hawa. Miongoni mwa changamoto ni kama ifuatavyo;

Ujangili; wanyama hawa wamekuwa wakiwindwa sana na watu kama vitoweo hali inayo changia kupungua kwa kasi sana katika maeneo wapatikanayo sheshe. Biashara haramu ya wanyamapori na bidhaa zao zinapelekea sheshe kuwindwa sana. Kama nilivotangulia kueleza hapo juu, nchini Botswana wanyama hawa hawafiki hata 100.Hivyo kama kasi ya ujangili dhidi ya wanyama hawa itazidi kuongezeka basi hata hapa nchini Tanzania tunaweza kuwapoteza kabisa wanyama hawa.Ujangili sio tatizo kwa sheshe tu bali hata kwa jamii nyingine za swala zimekuwa zikikumbwa na tatizo hili hali ambayo inasababisha taifa kupitia mamlaka za usimamizi wa maeneo tengefu ya wanyamapori kupoteza fedha nyingi sana kupambana na ujangili.

Uharibifu wa mazingira; kwa kiasi kikubwa sana uharibifu wa mazingira umepelekea sheshe kupungua katika maeneo mbali mbali. Hii ni kutokana na watu kuharibu maeneo yenye malisho ya wanyama haw ana kugeuza kuwa makazi. Uhaba wa chakula unasababisha wanyama hawa kuhama lakini pia mazingira yao tulivu ya kujificha n ahata kuzaliana pia yanapo haribiwa wanyama hawa hulazimikakuhama katika eneo hilo. Tukumbuke kuwa moja kati ya wanyama jamii ya swala ambao huwahi zaidi kuathirika na uharibifu wa mazingira basi sheshe huwezio kuwakosa katika kundi hilo.

Uingizaji wa mifugo kwenye mapori tengefu ya wanyamapori; kumekuwa na tabia ya wafugaji wengi kuingiza mifugo kwenye maeneo ya wanyamapori kwani kuna uwepo wa majani mazuri kwaajili ya kulishia mifugo yao. Hali hii inasababisha uwepo wa kugombania chakula kati ya sheshe au wanyamapori kwa ujumla na mifugo. Changamoto ya upatikanaji wa chakula katika maeneo ya wanyamapori inapozidi basis heshe hulazimika kuhama maeneo hayo na hatimae wafugaji wanazidi kuharibu maeneo hayo. Hii hupelekea hata mabadiliko ya kiikolpojia katika eneo hilo kwasababu ya uharibifu wa asilia iliyo kuwepo katika maeneo hayo.

Usimamizi mbovu wa vibali vya uwindaji; usimamizi duni wa vibali na shughuli za uwindaji wa wanyamapori unaonekana kuwa pia sababu ya kupungua kwa wanyama sheshe katika maeneo mbali mbali. Baadhi ya makampuni ambayo yana leseni na vibali vya uwindaji yamekuwa yakikiuka taratibu za uwindaji ama kwa kuwinda idadi kubwa zaidi au kuwinda sheshe ambao bado hawajafikia umri wa kuwindwa. Mamlaka za usimamizi wa vibali hivyo zinapo legalega kusimamia kwa madhubuti shughuli za uwindaji basi athari yake ni kupungua kwa idadi ya wanyama hawa kwenye maeneo tengefu ya hifadhi za wanyamapori.

NINI KIFANYIKE ILI KUHAKIKISHA SHESHE WANAENDELEA KUWEPO NCHINI TANZANIA NA IDADI YAO IONGEZEKE

Kutokomeza ujangili; serikali kupitia mamlaka za usimamizi wa wanyamapori na maliasili haina budi kutafuta mbunu mpya na za kisasa katika kupambana na majangili ambo wamekuwa wabinafsi katika kuliibia taifa hasa kwa upande huu wa wanyamapori. Mbali na matumizi ya mbinu mpya, serikali pia haina budi kutoa vibali vya ajira kwa mamlaka husika ili kuongeza idadi ya askari wa ulinzi katika hifadhi za wanyamapori ili iwepo doria muda wote na yenye askari wa kutosha ambao wanaweza kusambaa kwenye kila pembe ya hifadhi husika. Wataalamu pia wa uhifadhi waajiriwe ili kuchagiza utoaji wa elimu kwa jamii zinazo zunguka maeneo ya hifadhi na watu waweze kujua umuhimu wa uhifadhi wanyamapori. Kupitia elimu hii basi niwazi kwamba jamii zitashirikiana na mamlaka husika katika kufichua majangili na maficho yao na kuisaidia serikali kuokoa fedha nyingi ambazo inapoteza kila mwaka katioka kupambana na tatizo la ujangili hapa nchini.

Kuzuiya uanzishwaji holela wa makazi; serikali ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania kupitia wizara ya ardhi na makazi kwa kushirikiana na wizara ya maliasili na utalii haina budi kupambana na wale wote wanao anzisha makazi katika maeneo yaliypo tengwa kwaajili ya uhifadhi wa wanyamapori. Ziwepo sheria kali ambazo zitasaidia kutoa adhabu kali kwa wote wenye kukiuka mamlaka za wanyamapori kwa kuanzisha makazi katika maeneo hayo. Jamii nyingi zinazoishi pembezini mwa hifadhi zimekuwa na tabia ya kupanua maeneo yao ama kwa kuongeza eneo la makazi au mashamba hali ambayo inapelekea uharibifu wa mazingira na kusababisha sheshe kuhama katika maeneo hayo.

Usimamizi yakinifu wa vibali vya uwindaji; kama nilivyotangulia kusema hapo juu kuwa usimamizi wa vibali vya uwindaji unasuasua hivyo mamlaka zihakikishe zinasimamia kwa ukaribu zaidi kwa kampuni zote ambazo zina vibali na kujihusisha kwenye uwindaji ili kufuata utaratibu mzuri wa uwindaji. Pawepo na msimamizi kutoka mamlaka husika kila muda ambao kampuni inaingia katika shughuli za uwindaji ili kutokomeza tabia ya makampuni kuwinda idadi kubwa ya wanyama tofauti na kibali kitakavyo. Lakini pia hata maeneo mengine ambayo hayaruhusiwi kuwinda katika mapori hayo kwani kwa kawaida mapori ya akiba shughuli mbali mbali hugawanywa kutokana na maeneo.

Utengaji wa maeneo maalumu ya malisho ya mifugo; kupitia wizara ya mifugo, serikali ihakikishe yanapatikana maeneo sahihi ya wafugaji kwaajili ya malisho ya mifugo yao. Hatuia hii itasaidia kupunguza wimbi la uingizaji mifugo katika hifadhi za wanyamapori na kuchochea upatikanaji mzuri wa chakula kwa sheshe na wanyama wengine walao majani. Tunayo maeneo mengi sana tena yenye ardhi yenye rutuba ambayo yana chakula cha kutosha kwaajili ya mifugo, hivyo kwakuwa serikali ina mamlaka inaweza kuamua kutenga maeneo mbali mbali hasa kwa kuzingatia mikoa au sehemu zenye idadi kubwa ya mifugo ili kuepika migogoro ambayo imekuwa ikijiotokeza baina ya mamlaka za hifadhi za wanyamapori na jamii zinazo zizunguka hifadhi hizio.

Kuanzisha mitaala ya elimu ya uhifadhi mashuleni; moja kati ya vipengele ambavyo huwa naandika kwa msisitizo katika makala hizi basi kipengele hiki pia kimo katioka vipengele hivyo. Wizara ya elimu iangalie namka ambayo itaweza kuanzisha mitaala ya elimu ya uhifadhi kuanzia ngazi ya msingi ikiwezekana mpaka sekondari ili wanafunzi wajifunze kuhusu uhifadhi na umuhimu wa kuwatunza wanyamapori kwa maendeleo ya taifa. Hatua hii itasaidia kuzalisha mbalozi wengi katika jamii zetu ambao watakuwa na ki una ari ya kuona thamani ya wanyamapori lakini pia watasaidia kutoa elimu kwa watu wengine kuhusu umuhimu wa kuwalinda wanyamapori hapa nchini.

Utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa jamii; mamlaka za hifadhi za wanyamapori zihakikishe zinazidi kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa uhifadhi ili kusaidia kupunguza tatizo la ujangili. Zipo idara mbali mbali katika kila mamlaka ambazo kwa kushirikiana wanaweza kutoa elimu na ikamfikia kila mtu kuhusu shughuli za uhifadhi lakini pia faida tunayopata kama taifa kutokana na ubhifadhi. Lakini pia miradi mbali mbali inayo fadhiliwa na mamlaka za wanyamapori hapa nchini haina budi kufahamika ili jamii zijue kwa undanikazi kubwa inayofanywa na mamlaka hizo.

HITIMISHO

Sheshe ni wanyama ambao wanavutia sana kuwatazama hasa wanapokuwa katika mazingira yao asilia na wafanyapo shughulizao katoka mazingira ambayo hayana usumbufu. Ni wanyama ambao wanaathiriwa kwa kiasi kikubwa sana na haraka zaidi kutokana na uharibifu wa mazingira. Jukumu la uhuifadhi wa wanyamapori ni jukumu la kila mtanzania kwani faida zote zipatikanavyo na uhifadhi hutunufaisha wanachi wote kwa ujumla.

Idadi ya wanyama hawa inapungua kwa kasi sana na kuna baadhi ya nchi kama tulivyoona hawafiki hata 100. Tanzania tunatakiwa kujivunia sana kwakuwa na idadi kubwa ya wanyama hawa kuliko ncho yoyote ile japo bado pia tunakumbwa na changamoto mbali mbali katika uhifadhi wa wanyama hawa. Moja kati ya changamoto kubwa tumeona ni shughuli za binaadamu ambazo ndo zimekuwa zikipelekea kupungua kwa idadi ya wanyama hawa.

Ushirikiano kati ya taasisi mbali mbali hapa nchini na kwingineko barani Afrika unaweza kuwa chachu ya ongezeko na uhifadhi wa wanyama haw ana kupelekea idadi yao kuongezeka na kurudi kama ilivyokua hapo zamani. Ili kulitekeleza hili taasisi mbali mbali zinazo jihusisha na uhifadhi wa wanyamapori hazina budi kuandaa sera madhubuti ambazo zitapelekea hamasa kubwa kwenye suala zima za uhifadhi wa wanyamapori.

Pongezi za dhati kwa mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori nchini (TAWA) kwa kazi kubwa sana wanayo ifanya ya usimamizi wa pori la Kilombero na kuhakikisha wanyama hawa wanaendelea kusalia katioka pori hilo tena kwa wingi. Lakini pia nizipongeze mamlaka nyingine kwa usimamizi mzuri wa rasilimali zetu hasa wanyamapori kwani Pamoja na changamoto mbali mbali mnazo kutananazo lakini bado hamjakata tamaa. Nasi kama watanzania hatuna budi kushirikiana na mamlaka husika na taasisi nyingine ili kuhakikisha uhifadhi wa wanyamapori unastati kwa kizazi chetu na vizazi vijavyo.

Makala nyingine kuhusu wanyama jamii ya swala unaweza kusoma hapa.Zijue Sifa Za Wanyama Jamii Ya Swala

……….. MWISHO ………

Ili kujifunza mengi zaidi kuhusu wanyamapori na uhifadhi kwa ujumla basi usisite kuwasiliana nami kupitia

Sadick Omary Hamisi

Simu=0714116963/0765057969

Email=swideeq.so@gmail.com

Istagram=wildlife_articles_tanzania

Facebook=Envirocare and Wildlife Conservatio au Sadicq Omary Kashushu

Au tembelea tovuti yetu= www.wildlifetanzania.home.blog

………… “I’M THE METALLIC LEGEND”…………