Mpendwa msomaji wa makala hizi za wanyamapori karibu katika makala hii inayohusu kugawanyika kwa mazingira ya asili yaan Habitat Fragmentation. Neno mazingira ya asili maana yake ni ardhi ambayo inahifadhi aina mbalimbali za mineo, Wanyama, wadudu n.k kabla ya kuharibiwa au kubadilishwa matumizi yake kugawanyika kwa mazingira ya asili ni kitendo cha eneo kubwa la mazingira ya asili kubadilishwa na kuwa vipande vidogovidogo vilivyojitenga. Vipande hivi huwa kila kimoja na mandhari tofauti ukilinganisha na lile la asili.
Kugawanyika kwa mazingira ya asili hujumuisha upotevu wa mazingira pamoja na mabadiliko katika muundo wa mazingira. Mchakato huu husababisha sehemu ambazo hutenganisha kipande kimoja na kingine kuongezaka kwa viwango vya mwanga, joto, kasi ya upepo na pia hali ya unyevu
Uhusiano wa kugawanyika kwa mazingira ya asili na wanyamapori.
Kugawanyika kwa mazingira ya asili imekuwa ni tishio kubwa hapa duniani linalopelekea upotevu wa viumbehai (Wu 2013). Wanyamapori wengi wana mazingira yao ya asili ambayo hutumia kufanyia shughuli zao za kila siku lakini kutokana na kugawanyika kwa mazingira ya asili hupelekea kupungua kwa ukubwa na ubora wa makazi na maeneo ya chakula na pia maeneo ya kuzaliana. Hifadhi nyingi nchini zinakabiliwa na tatizo la kugawanyika kwa mazingira ya asili kwa sababu ya shughuli za binadamu ndani na karibu na hifadhi. Hivyo mchakato huu huleta athari nyingi katika shughuli za kiuhifadhi. Mchakato huu unaathiri zaidi spishi ambazo hutegeemea maeneo makubwa kwa ajili ya kustawi kama Wanyama wakubwa kama tembo na ndege na wanyama kama nyumbu wanaohama kwa misimu hivyo hukabiliwa na changamoto ya kupungua kwa uwezo wa kufikia rasilimali.
Sababu za kugawanyika kwa mazingira ya asili katika maeneo ya hifadhi.
- Shughuli za binadamu
Ujenzi wa Barabara, reli, na miundombinu mbalimbali katika maeneo ya hifadhi au karibu na hifadhi huweza kusababisha kugawanyika kwa mazingira ya asili kwa kuvunja maeneo ya asili na kuzuia au kuathiri shughuli za wanyamapori.
Uvamizi wa ardhi,
uvamizi wa ardhi unaofanywa na binadamu kama vile ujenzi holela wa makazi karibu na maeneo ya hifadhi na shughuli za kibiashara husababisha kupunguza eneo la asili la wanyamapori na kusababisha kugawanyika kwa mazingira ya asili
- Mabadiliko ya tabia ya nchi
Mabadiliko ya tabia ya nchi yanaweza kusababisha kugawanyika kwa eneo la asili , kwa mfano ongezeko la joto au ukame katika misitu linaweza kusababisha kupunguza eneo la msitu kwani baadhi ya miti hufa na kuacha uwazi kati ya sehemu moja na nyingine hivyo msitu unakuwa umegawanyika.
- Mito
Mito husababishwa kugawanyika kwa mazingira ya asili katika hifadhi kwa kuwa kama kizuizi cha kijiografia ambapo hugawanya ardhi na kuwa kama mipaka kati ya sehemu moja na nyingine hivyo kuzuia shughuli mbalimbali za wanyamapori.
Athari za kugawanyika kwa mazingira ya asili kwa wanyamapori.
- Upungufu wa eneo la makazi
Kugawanyika kwa mazingira ya asili kunaweza sababisha upungufu wa maeneo ya makazi ya wanyamapori. Hali hii hutokea pale ambapo eneo la wanyamapori la asili liliweza kuwamudu wote kupata makazi na mahitaji yao muhimu kama chakula, maji na maeneo ya kuzaliana lakini kutokana na kugawanyika kwa eneo. Wanyamapori hawa wanakuwa wanakabiliwa na upungufu wa eneo la makazi kwani ukubwa wa eneo lao unakuwa umepungua na wanashindwa kupata mahitaji yao muhimu.
- Kujitenga kwa vinasaba (Genetic isolation)
Kugawanyika kwa maeneo ya asili kunasababisha wanyamapori waliokuwa katika kundi moja kubwa ,kuwa katika vikundi vidigovidogo katika maeneo yao yaliyogawanyika. Hii hupunguza mtiririko wa vinasaba kati ya vikundi kwa kuwa mgawanyiko huu huzuia harakati za wanyama, na pia hupunguza mtiririko wa vinasaba na kuongeza urithi wa vinasaba (inbreeding) ambao unaweza sababisha spishi zitakazozaliwa kuwa na udhaifu katika afya zao.
- Athari za kwenye mipaka (Edge effect)
Maeneo ambayo yametengana hutengeneza mipaka kati ya eneo moja na jingine kwa mfano eneo lilikuwa ni moja na kubwa lakini likatenganishwa kwa kujenga barabara , huwa ni mipaka kati ya eneo moja na jingine .Katika maeneo haya ya mipaka huwa na hali tofauti kabisa za kimazingira ukilinganisha na ilivyokuwa kabla ya eneo kugawanywa. Maeneo haya huwa na joto kali sana, upepo unaovuma kwa kasi kubwa, na rahisi kwa mimea vamizi kuvamia na kustawi kwa wingi na pia huwa kuna ongezeko la shughuli za kibinadamu hivyo huendelea kuvuruga makazi ya wanyama na kusababisha waende mbali na maeneo haya ili kuepuka kupata athari .
- Upoteaji wa huduma za mifumo ya Ikolojia (ecological services).
Mifumo ya ikolojia yenye afya na ambayo haijagawanyika hutoa huduma mbalimbali kama vile kusafisha maji, uthibiti wa hali ya hewa, rutuba ya udongo na kuthibiti mafuriko. Kugawanyika kwa mazingira ya asili huhatarisha huduma hizi, hivyo huathiri viumbe hai na binadamu wanaotegemea huduma hizi.
- Ongezeko la migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Wakati makazi ya wanyamapori yanapogawanyika, Wanyama wanaweza kuvamia katika makazi ya binadamu kutafuta mahitaji yao kwani eneo lao la makazi linakuwa linashindwa kuwapatia mahitaji yao ya muhimu, hivyo hii huleta migogoro baina ya binadamu na wanyamapori. SOMA; Zijue Sababu Saba (7) Zinazopelekea Migogoro Baina ya Binadamu na Wanyamapori Kutoisha
- Mabadiliko katika mifumo ya uhamaji wa wanyamapoi.
Kugawanyika kwa mazingira ya asili ya wanyamapori kunaweza kusababisha kuathiri harakati za asili za uhamaji wa wanyamapori. Hii ni muhimu hasa kwa spishi za wanyamapori wanaotegemea makazi makubwa yenye kuungana kwa ajili ya harakati za kila msimu za kuhama, kutafuta chakula au kwa ajili ya kuzaliana. SOMA Zifahamu Tabia za Spishi za Ndege Wanaohama Kutoka Nchi Moja Kwenda Nchi Nyingine
- Kupungua kwa idadi ya wanyamapori.
Spishi zinazotegemea makazi makubwa na yaliyounganika zinakabiliwa na athari ya kupungua kwa idadi au kutoweka kwa eneo lao pindi makazi yanapogawanyika, sababu kuu ni wanyama wanakosa maeneo mazuri ya kupata chakula na sehemu ya kuzaliana hivyo hushindwa kuzaliana vizuri na hupelekea idadi kupungua. Lakini pia pale wanapokosa eneo kubwa ambalo litaweza kuwatosha wote, hukaa kwa mafungu madogomadogo hivyo inakuwa rahisi kwao kuathiriwa na matukio ya kiholela ya ujangili au wanashindwa kustahimili athari za mazingira hivyo kupelekea idadi kupungua. Sii hivyo tu pia sehemu ambazo huwa ni mipaka baina ya eneo moja na jingine huwa na mimea mbalimbali ambayo hufa wakati ugawanyaji wa mazingira unapokuwa unafanyika, mfano katika ujenzi wa barabara katika hifadhi mimea mingi hung’olewa au hukanyagwa au hukatwa ili kuweka mazingira vizuri kwa ajili ya ujenzi wa barabara . SOMA Kilio Kisichoisha Ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi
Ujumbe wangu kwa jamii
Ninakusihi msomaji wangu kuchukua hatua katika kuzuia na kudhibiti athari hizi katika hifadhi zetu wa kuhakikisha unafuata sheria zote za hifadhi husika, kuwaelimisha ndugu na jamaa zetu waishio karibu na hifadhi kwamba waridhike na maeneo yao na wasiingile maeneo ya hifadhi kwani wakifanya hivyo wanaenda kuligawa eneo la hifadhi ambapo mwisho inaweza waletea wao wenyewe athari kama vile kuvamiwa na wanyama na kuharibiwa makazi yao. Lakini pia ulinzi wa mazingira ni jukumu letu sote hivyo tuchukue hatua ya kuhifadhi mazingira ya hifadhi zetu na wanyamapori wetu.
Asante
Mwandishi wa Makala
Monica Charles Mahilane
+255 652 267 935
mahilanemonica49@gmail.com