Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu kwenye barua yetu ya leo ambayo nimeamua kuwaandikia kila mtu, kila shirika na kila kampuni ambayo inajihusisha na mambo ya utalii. Barua hizi hza wazi huwa naziandika kila jumapili ambapo lengo kubwa ni kutoa taraarifa kwa jamii ya kitanzania ili kila mtu ajue nini kinaendelea kwenye maliasili zetu, lakini pia barua hizi zina lengo kubwa la kutoa elimu na maarifa kuhusu uhifadhi wa mazingira yetu na mazingira ya wanyamapori. Hivyo naamini kabisa kupitia maandishi haya kila mtu atakayesoma atagundua na kutambua maliasili zilizoko kwenye nchi yetu, na akisha kuzijua ataamua kuchukua hatua kama ni kuzitembelea au kama ni kuona namna ya kunufaika na uwekezaji na fursa nyingine kwenye sekta hii.

Aidha kwa kutambua hilo nimekuwa naandika makala za uhifadhi na utambuzi wa maliasili zetu kila siku nikiamini kuna watu wanasoma na kuchukua hatua. Kama unavyojua Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye watu wengi na itaendelea kuwa na watu wengi hivyo inatakiwa kuwepo na elimu ya mazingira na watu watambue maliasili zilizopo kwenye nchi yao. Baada ya kuandika makala hizi nimegundua kwa kiasi kikubwa watanzania wengi hawajui mambo mengi yanayoendelea kwenye maliasili zao hasa kwenye upande wa wanyamapori na utalii. Nimegundua wengi wanapenda sana wanyamapori, wengi wanapenda kutalii, yani kwenda kutembelea hifadhi za wanyama, na sehemu zenye mvuto lakini wanashindwa pa kuanzia .

Kama nilivyokwisha dokeza hapo juu kwamba barua hii itawalenga zaidi wale wenye makampuni ya utalii, wanaojihusisha na kubeba na kutembeza watu kwenye mbuga za wanyama, lakini pia barua hii itawahusu zaidi mamlaka za usimamizi wa hifadhi zetu kwa kuwa wao ndio wanaoweka utaratibu wa namna ya kutembelea hifadhi, gharama, vigezo na mambo mengine mengi ambayo ni mazuri kwa ajili ya uhifadhi na utunzaji wa maliasili zetu. Hivyo kwa pamoja nimewaandikia barua hii ili muamue kwa pamoja kuhusu kipindi hiki cha sikukuu.

Barua hii ina lengo na mapendekezo kwa wadau hawa wa utalii, kwamba katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu wangepunguza gharama za watu kutembelea hifadhi za wanyama na sehemu nyingine zenye vivutio. Nimekazia wapunguze gharama kwenye kutembelea hifadhi kwa kuwa kutembelea sehemu hizi gharama yake ni kubwa ambayo sio kila mtanzania ataweza kuimudu. Hivyo nashauri na pia naomba kwa namna ambayo mnaona itafaa na kupendeza zaidi kupunguza gharama za kutembelea hifadhi, ikiwa ni pamoja na gharama za usafiri kwa wale wasiokuwa na usafiri, gharama za malazi na kiingilio.

Endapo jambo hili litafanyika litasaidia sana watu ambao wana matamaniao na shauku ya kutembelea hifaadhi za wanyama kutimiza matarajio na matamanio yao ya kutembelea hifadhi za wanyama. Pia endapo jambo hili litafanyika litasaidia sana watu kuthamini na kuona kwa macho yao rasilimali za nchi yao, hii ni njia moja wapo ya kuifanya jamii kuthamini maliasili zao na kuwa tayari kuzihifadhi. Vile vile kama watashusha gharama wazingatie kwa kushusha gharama kwa watanzania pekee, kwa wageni inaweza kubaki hivyo hivyo bila kushusha.

Katika msimu huu wa sikukuu ambapo watu wengi wanakuwa kwenye mapumziko ndio kipindi kizuri kwa wadau wa utalii kutumia fursa hii kutangaza kushusha gharama za kutembelea hifadhi na mbuga za wanyama, pia kipindi hiki watu wengi hutamani kusafiri na kwenda sehemu tofauti ili kufurahia na kujifunza mambo mengine ya maisha. Kipindi hiiki hata wanafunzi wengi huwa wanakuwa likizo nyumbani, wafanyakazi wengi wanakuwa nyumbani hivyo ni nafasi nzuri sana kwa wadu na watu wenye mamlaka kwenye hifadhi zetu kuamua kutumia fursa hii kuzitangaza maliasili zetu kwa watanzania wenyewe.

Aidha napenda kuwashukuru wadau wote wa wa sekta ya utalii kwa kuwa mara kwa mara wamekuwa wakiamasisha watu kutembelea hifadhi na wakati mwingine kupunguza gharama, nawapongeza pia TANAPA kwa kuwa wanatoa fursa mbali mbali kwa gharama  nafuu ili watu watembelee hifadhi za wanyamapori.

Ahsanete sana.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania