Habari msomaji wa Wildlife Tanzania karibu kwenye makala ya leo, kama nilivyowahi kukuandikia kwenye makala za nyuma kwamba kila Jumapili nitakuwa naandika barua, na barua hii ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu, barua hii haichagui kwamba unapenda mambo ya wanyamapori au haupendi, barua hii haichagui rika, jinsia wala cheo. Barua hii ni kwa watanzania wote. Naweza kusema kama unaishi katika ardhi ya nchi hii barua hii inakuhusu. Barua hizi nimeamua kuaziandika kila siku za jumapili ili watu wajitambue kwenye maeneo ya mazingira yanayowazunguka. Hivyo lengo la barua hii ni kutoa elimu ya kujitambua kwenye upande wa mazingira na pia kutengeneza roho ya uwajibikaji kwenye mambo ya msingi kwenye maisha yetu.
Maisha yetu tunayoishi yanagusa vitu vingi na yanahusisha vitu vingi sana ambavyo vinatuzunguka. Vitu hivi vinavyotuzunguka vipo vya aina nyingi sana kuna viumbe hai na visivyo viumbe hai, kwenye viumbe hai kuna wanyama pamoja na mimea, kwenye wanyama kuna wanyama wa porini na wanyama wa nyumbani au wanyama wa kufugwa, yote haya yapo kwa ajili ya binadamu na kwa ajili ya kufanya maisha ya binadamu yaweze kuwa bora na ya maana hapa duniani. Mazingira yana umuhimu sana kwenye ustawi na ukuaji wa kitu chochote, mazingira ndio yanaamua aina ya maisha na mifumo ya maisha ya watu fulani. Hivyo suala la mazingira ni suala ambalo tunahitaji kulichukulia kwa uzito na kwa umakini mkubwa.
Ninapozungumzia suala la mazingira sio tu suala la kukata miti na kupanda miti, sio tu swala la sheria kali na mipaka ya hifadhi za taifa. Suala la mazingira linagusa sehemu kubwa sana ya maisha yetu. Fikiria mazingira yangekuwa machafu, hakuna utaratibu wowote wa kuondoa uchafu au kufanya usafi kwenye mazingira yetu, nadani hata maisha yetu yangekuwa mafupi sana. Fikiria hewa ya Oksijeni tunayovuta, na hewa ya Kabonidiksaidi tunayotoa ingekuaje kama kungekuwa hakuna utaratibu wa kubadilishana hewa na mimea. Mimea inatoa hewa ya Oxigeni na mimea inahitaji hewa ya kabonidiksidi ili iendelee kukua na kuendeleza. Kwa hiyo mti ambao upo hapo kwako au kwa jirani yako ni muhimu sana kwenye ujenzi wa maisha yetu na maisha ya mimea, maisha ya wanyama na maisha ya mimea tunategemeana na kuhitajiana sana, hii ni kanuni ya ajabu sana.
Mimi ninachosisitiza kwenye makala hii ni sisi kuwa makini na sensitivu sana kwenye mazingira yetu. Mazingira yetu yakiwa safi hata maji yatakuwa safi hatimae wanaotumia maji hayo watakuwa salama pia. Kati ya mambo yanayochangia kuenea kwa magonjwa mengi ya binadamu na wanyama ni maji machafu. Unakuta maji machafu yanatoka kiwandani yanaingia kwenye vyanzo vya maji au kwenye makazi ya wanyamapori, na hivyo wanyamapori bila kujua wanakunywa maji yenye kemikali au sumu kali sana inayotokana na uchafu wa viwandani.
Kwa hiyo ndugu zangu watanzania, tuayatunze mazingira yetu yatutunze, hakuna urithi mzuri tunaoweza kuacha hapa dunini kama kuacha mazingira bora yanayofaa kwa ajili ya vizazi vijavyo. Fekiria gharama za miti iliyoota kando kando ya nyumba yako, au nkwenye shamba lako, miti hiyo inachukuwa miaka mingi sana hadi kufikia hatua kubwa ya kuzaa na kutoa matunda ambayo ni msaada na faida sana kwa maisha yetu. Mti huo unaweza ukawa umekaa na kukua kwa zaidi ya miaka 20 au 30, mtu anakuja anakuja kuukata ni hasira kubwa sana. Hivyo tufikiriae sana tunapotaka kufanya maamuzi ya namna hii.
Hivyo basi mimi na wewe tunawajibu wa kuweka kila kinachotuzunguka nikimaanisha mazingira yetu kuwa salama na masafi wakati wote, hili ni jukumu la kila mtanzania, sio jukumu la kikundi cha watu fulani tu au serikali za mitaa au majiji, ni jukumu letu watanzania. Tunatakiwa tujitambue kwenye eneo hili, maana ni muhimu sana kwenye kwenye maenedeleo na ukuaji wa kila kitu. Fikiria tungekuwa na mazingira mabaya ina maana tusingekuwa na vivutio vizuri kama wanyamapori au hata misitu yetu ambayo ina mchango mkubwa sana kwenye ukuaji wa pato la taifa kupitia maliasili na utalii.
Hivyo kwa utanguilizi tu nataka kila mtanzania aelewe kuwa hii ni barua ya utangulizi tu kukuandaa wewe kwa makala nyingi zijazo zitakazogusa mambo mengi na mambo mbali mbali ya mazingira na wanyamapori. Hivyo mtanzania mwenzangu karibu tuendelee kufanyia kazi kila lililo la muhimu kwenye utunzaji wa mazingira yetu. Nafarijika sana kuona juhudi za watu, serikali , mashirika na hata juhudi za kimataifa kwenye suala la utunzaji wa mazingira yetu.
Nakushukuru sana kwa kusoma makala hii, karibu tuwe pamoja, kwa maoni ushauri na maswali karibu tuwasiliane kwa mawasiliano yaliyopo hapa chini ya makala hii.
Asante kwa kusoma makala hii,
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255683 862 481/+255742 092 569
www.mtalaam.net/wildlifetanzania