Katika kipindi hiki ambacho dunia inashuhudia mauaji makubwa ya wanaymapori na uharibifu mkubwa wa mazingira asilia hatua mbali mbali zimechukuliwa hadi sasa, vikundi vingi vimeinuka na kuanza kampeni mbali mbali za kuhifadhi wanyamapori na mazingira yao, serikali za nchi na umoja wa mataifa umefanya vikao vingi sana, watalaamu wa masuala ya sayansi ya wanyamapori, pamoja na sayansi ya jamii na mazingira wameandika kila walichojua kuhusu wanyamapori na mazingira yao.
Mtandao wa intaneti umesheheni taarifa mbali mbali zinazohusu mikasa wanayokutana nayo viumbe hai hawa ambao Mungu amewaweka waishi kwenye dunia moja na wanadamu. Tafiti za kitalaamu zimefanyika nyingi sana na zinaendelea kufanyinga, mikakati na mipango mingi ya nchi mbali mbali imewekwa na kuandaliwa kulinda na kuhifadhi wanyamapori hawa. Sheria nyingi sana za uhifadhi na udhibiti wa wanyamapori zimetungwa kitaifa na kiamataifa. Nchi nyingi zimeingia makubaliano na kuweka saini kukubali kwa pamoja kufanya kazi ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yao.
Lakini kila hatua tunayochukua kukabiliana na halii hii kwenye nchi zetu ndipo tunapogundua na kujua ni kwa kiasi gani tatizo lilivyo kubwa na inaonyesha ni kwa namna gani tumechelewa hadi kufikia hatua ambayo nchi moja pekee haiwezi kukabiliana na tatizo la ujangili na kulimaliaza. Kila kukicha nchi zetu, wahisani na wadau wa maliasili na mazingira kwa ujumla wanatumia mamilioni ya dola za kimarekani kudhibiti ujangili katika nafasi mbali mbali, kama vile porini, mjini, vijijini, na hata kwa njia ya mitandao ya intaneti.
Mfumo wetu wa maisha tunaoishi hapa duniani ni mfumo ambao unatulazimu kwa namna moja ama nyingine kushirikiana na kuhusiana na wanyamapori, pia hata mazingira tuliyonayo kutegemeana na sehemu na jamii, maisha yetu yanategemea kwa kiasi fulani mazingira asilia ambayo ni muhimu sana kwa maisha ya mimea na wanyamapori. Watu wanahitaji maji safi na salama, wanahitaji chakula, wnahitaji nishati mbali mbali kwa matumizi yao ya lazima kama vile kuni, mkaa , gesi na madini mengine.
Bajeti ya nchi zetu kwa kiasi kikubwa inategemea mapato ya maliasili zilizopo kwenye nchi husika, ili kuwe na maisha na shughuli nyingi za kimaendeleo ziendelee kuwepo na watu wapate huduma muhimu kama vile shule, afya, barabara na maji inahitajika mamilioni ya fedha nyingi ili miradi hii ya maendeleo iendelee kuwepo kwenye jamii. Mamilioni ya fedha za kuanzisha na kujenga miradi ya aina hiyo inatoka wapi? Kwa hakika kuna sehemu zinatoka, achilia mbali misaada ya wahisani, achalia mbali kodi zinazokusanywa kutoka kwenye miradi na kwa wafanyabiashara au kwenye shughuli za uzalishaji zinazoendelea, kwa hakika zinatoka kenye sekta ya maliasili na utalii.
Kwa jinsi tunavyozidi kutumia fedha nyingi sana kwenye kuwahifadhi wanyamapori na maliasili kwa ujumla, ni ishara tosha kutuonyesha jinsi ambavyo tatizo lilivyo kubwa na linaendelea kuwa kubwa na kutugharimu sio tu fedha bali hata maisha yetu wenyewe yanakuwa hatarini kutokana na usimamizi na ulinzi wa maliasili zetu.
Kuna njia moja ya uhikika ya kutusaidia kupunguza kama sio kumaliza kabisa tatizo la ujangili kwenye nchi zetu; ”kuna msemo wa wahenga walisema umoja ni nguvu na utengeno ni dhaifu”. Kwa kuwa tatizo hili limeenea na kutulemea juhudi binafsi pekee hazitoshi, zinahitajika mbinu na uzoefu wa watu mbali mbali, wadau wa masuala haya ya wanyamapori, nchi zote duniani,vikundi vya itikadi mbali mbali kusimama na kuunga mkono juhudi zote za kupambana na ujangili ili kutunza wanyamapori na mazingira yao.
Amini nakuambia, nguvu zote tunazotumia kupambana na ujangili wa wanyamapori wetu, ili kuhifadhi maliasili zetu, sio tu kwasababu tunataka tuwaone wanyamapori na mimiea ikiendelea kuwepo, bali tunataka kuona maisha ya binadamu yakiendelea kuwepo na kuwa bora kwa sababu ya uwepo wa mazingira safi na salama yanayofaa kuishi kwa wanyama na binadamu.
Kama wanyamapori na mimea itashindwa kuishi kwasababu ya uharibifu wa mazingira, tujue kabisa anayefuata hapo ni binadamu kushindwa kuishi kwa sababu ya uharibifu wa mazingira hayo.
Asante sana kwa kusoma makala hii.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania