Kila kitu kilichoumbwa na Mungu hapa duniani kina makusudi maalumu, maana yake kipo ili vitu vingine viweze kwenda, maisha ya viumbe hai yametengenezwa kwa namna ya ajabu sana, ni muunganiko unaogusa vitu vingi. Hii ikiwa na maana kwamba maisha yetu kama binadamu yameshikiliwa na kuunganishwa na vitu vingi sana, na vitu vyote hivyo katika uhalisia wake vinaendeshwa kwa sheria za asili, iwe ni binadamu, mimea, wanyama au ndege wanaendesha maisha yao kwa kufuata kanuni na sheria za asili. Ujinga ni kutokujua kwamba maisha yetu hayategemei wala kuesndeshwa kwa sheria za asili. Misingi ya mafanikio na ustawi wa kudumu kwenye jambo lolote ni kujua sheria husika na kuzifuata, na hapa sheria ndio misingi yenyewe, maisha yetu yamejengwa tuyaishi kwenye misingi, maisha ya wanyama, mimea, ndege na samaki yamejengwa wayaishi kwenye misingi.

Kwasababu tunategemeana kwenye mazingira na kwenye maisha hatutakiwi kufanya vitu vya kibinafsi visivyo na msaada kwa wengine. Mambo mengi ya uharibifu yametokea na yanaendelea kutokea duniani kwa sababu ya ubinafsi na kufanya mambo bila kuwafikiria wengine watanufaikaje au watasaidikaje. Kwa mfano kumwibia mtu mwingine mali zake, hapo utanufaika wewe kwa muda mfupi lakini kibaya zaidi umeharibu maisha ya mtu uliyemwibia na kumrudisha nyuma, pia itakupelekea kupigwa na hata kwenda jela endapo utakamatwa hivyo mfumo mzima wa maisha yako umeharibika, kama ni baba au mama ndie ameiba na alikuwa na familia, fikiria watoto wataanza kuhangaika na kukosa malezi na misaada ya wazazi ya karibu na hapo watoto huanza kufanya vitu ambavyo vinaweza kuwa hatari tena kwenye maisha yao, hivyo maisha ya jamii nzima yanakosa uasalama na amani kwa tendo moja.

Kwa mfano nilioutoa hapo juu ni kuhusu binadamu na binadamu mwenzake, sasa kwenye aya hii tuingie ndani kidogo kwenye somo la makala hii. Kwanza kabisa naamini maisha ya mwituni kwa asilimia mia moja yanaendeshwa kwa sheria na kanuni za asili, yani mimea na wanyama wote wanategemeana na maisha yanaenda bila shida. Lakini kikiingia kitu kingine kikafanya kitu ambacho sio cha kawaida katikati ya mfumo wa maisha wa asili basi mambo yanaaza kupoteza uelekeo na kila kitu kinakosa utulivu kwenye mazingira yao.

Kwa mfano shughuli nyingi za kibinadamu zinazofanyika kando kando ya vyanzo vya maji au karibu na maeneo ya makazi ya viumbe hai wengine mara nyingi haziachi salama sehemu hizo. Uzoefu unaonyesha wazi sehemu nyingi sana kwenye nchi yetu nan chi nyingine anapoingia binadamu kujihusisha na shughuli zake kwenye maeneo oevu au maeneo muhimu ya wanyamapori athari za matokeo yake huwa ni mbaya kwa pande zote. Ingawa kwa haraka haraka mtu anaweza kuona yeye ndiye amenufaika kwa kupata alichokusudia lakini madhara yake ni makubwa kimfumo na kiikologia. Fikiria mtu anapokata miti au anavyofyeka shamba kwa kukata miti mingi ya asili ili tu apate sehemu ya kupanda mazao yake, fikiria wachoma mkaa, fikiria wanaochimba madini sehemu muhimu zenye makazi na mazalia ya muhimu ya viumbe hai au mbuga za wanyama. Mtu anaweza kuona anapata manufaa makubwa anapofanya jambo hilo, lakini hajui anafanya jambo la kibinafsi bila kufikiria miaka mingi ijayo na vizazi vijavyo vitaishije hapa duniani. Vile vile anafanya jambao ambalo likishaharibika ni ngumu sana kurudisha kwenye hali yake ya mwanzo.

Tarehe 30/9/2017, ilikuwa ni siku ya Tumbusi duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka. Katika sherehe zilizofanyika katika Kijiji cha Tungamalenga mkoani Iringa, nilijifunza mengi kutoka kwa wengi walioongea. Sherehe hizi ziliandalliwa na Shirika lisilo la kiserikali la kijamii la kuhifandhi wanyamapori (Wildlife Conservation Society, WCS) ambao ndio watafiti wakuu wa ndege huyu aitwaye Tumbusi kwa Ukanda wa Nyanda za juu Kusini, yani tafiti zao kuhusu Tumbusi huzifanyia kwenye hifadhi za Kusini mwa Tanzania. Katika sherehe hizo ambazo zilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, wadau mbali mbali walipewa nafasi ya kumwelezea ndege huyu aitwaye Tumbusi walielezea vizuri sana lakini ilionekena wengi hawamfahamu ndegu huyu mashuhuri aitwaye Tumbusi, hata hivyo bila kuwaacha nyuma wanafunzi wa shule za Sekondari na misingi walipewa nafasi ya kuwasilisha ujumbe wao kwa njia nyimbo.

Nilijifunza mengi kweli siku hiyo. Lengo kuu la kufanyika kwa hayo yote ni kutengeneza kwenye akili za watu kuwa ndege huyu ni muhimu sana kwenye mazingira yetu ya hifadhi za wanyama lakini pia hata kwenye mazingira yetu hivyo kwa uelewa huo tushirikiane kwenye uhifadhi wa ndege huyu. Kati ya mengi niliyojifunza napenda niyaweke hapa ili kila moja aweze kuelewa umuhimu wa ndegeu huyu kwenye ikologia ya wanyama na usalama wa maisha ya biandamu kama nilivyodokeza mwanzoni mwa makala hii kwamaba kwenye maisha tunategemeana sana.

Ndege huyu aitwaye Tumbusi ni miongoni mwa ndege jamii ya Tai wanaokuala sana mizoga, kwa tafiti mbali mbali za nje na ndani ya nchi ni kwamba kuna zaidi ya aina 22 za Tumbusi duniani nao wamegawanyika kulingana na maeneo wanayopatikana. Kwa upanda wa Tanzania kuna baadhi ya tafiti zilifanyika katika hifadhi za Kaskazini mwa Tanzania yani Serengeti, na sasa nguvu imehamia Kusini, na matokeo ya utafiti yanaonyesha hifadhi ya taifa ya Ruaha ina aina nne za Tumbusi ambao ni Tumbusi mgongo mweupe, Tumbusi kichwa cheupe, Tumbusi mdogo au Tumbusi kapu chini, na Tumbusi Rupple’s. Hizo ni aina za Tumbusi wanaopatikana katika hifadhi ya taifa ya Ruaha na maeneo ya Asasi ya kijamii ya Mbomipa.

Tumbusi wamekuwa na faida nyingi sana kiikologia na kimazingira pia, hii ni kutokana na uwezo wao wa kula mizoga inayojifia yenyewe au hata inayouliwa na wanyama kama simba au majangili. Hii ni nzuri sana kwani husaidia sana kutokuenea kwa magonjwa yanayokuwa kwenye mzoga, kwa tafiti za kibaolojia zinaonyesha kuwa wanyamapori wanaokufa wakiwa na ugojwa kama kimeta au kichaa cha mbwa endapo mizoga yao italiwa na Tumbusi vijidudu vyote vya kimeta au kichaa cha mbwa vilivyoliwa na Tumbusi vinafia vyote ndani ya tumbo la Tumbusi, ambalo ni tumbo la ajabu sana lina tindikali kali sana ambayo inaweza kuua vimelea vyote vya magojwa  vilivyokuwa kwenye mzoga kama vile kimeta na kichaa cha mbwa na magojwa mengine bila kuyaeneza zaidi. Lakini nzuri zaidi ni kwamba pamoja na kwamba ndege huyu atakula mizoga hiyo yenye vimelea vya magonjwa hawezi kuathirika au kupata madhara yoyote, ataendelea kuwa salama kabisa.

Tofauti na wanyama wengine wanaokula mizoga kama vile Bweha na Mbwa ambao hawana uwezo wa kuua vimelea vya magojwa ya kimeta na kichaa cha mbwa, hivyo wanapotoa vinyesi vyao husababisha kusambaa kwa ugojwa wa kimeta na kichaa cha mbwa kwa wingi kwenye mazingira yetu, ambayo hupelekea wanyama wa kufugwa kama vile ng’ombe na mbwa kupata maambukizi hivyo kusababisha kusambaa kwa kimeta na kichaa cha mbwa kwa mbwa, na endapo mbwa mwenye kichaa atang’ata mtu, mtu huyo mara moja anapata kichaa cha mbwa na mara nyingi hupoteza maisha. Hivyo uwepo wa Tumbusi kwenye maeneo yetu ni muhimu sana kwani yeye ni sabuni ya mazingira.

Kama ilivyokuwa kwenye maadhimisho ya siku ya Tumbusi duniani kauli mbiu ilikuwa ni, “Tumbusi ni Sabuni ya Mazingira” ni sabuni kwani anakula mizoga yote na kufanya hifadhi na mazingira kuwa masafi na salama kabisa. Pia ni sabuni ya mazingira kwa sababu wana uwezo wa kula mzoga mara tatu ya fisi na bweha hivyo, hula mizoga yote na kubakiza mifupa ikiwa mieupe bila uchafu wowote, hii ndio sababu wanaitwa ni sabuni ya mazingira.

Pamoja na kazi nzuri sana wanayoifanya Tumbusi kwenye hifadhi za wanyama na kwenye mazingira yetu bado watu wengi hawana ufahamu au hawatambui umuhimu wa ndege hawa kwenye mazingira yetu, fikiria kungekua na mizoga kila mahali ingekuaje, fikiria kusingekuwa na tumbusi maambukizi na kuenea kwa magojwa ya kchaa cha mbwa na kimeta ingekuaje, fikiria kungekua na mizoga yenye harufu kali ndani ya hifadhi zetu au kwenye mbuga zetu za wanyama hali ya utalii ingekuaje? Ukiona hali ni nzuri, mazingira yanavutia na hewa ni safi haina harufu usisahau kuwa Tumbusi wamefanya kazi yao. Ukiona hakuna kichaa cha mbwa na kimeta kwenye maeneo ya jamii zetu usisahau kuwa Tumbusi mwenye uwezo wa kuwashuhulikia hao vimelea vya magojwa ya kimeta na kichaa cha mbwa amefanya kazi yake. Maaskari wanyamapori wanajua nini faida ya ndege hawa pale wanapokuwa kwenye doria au kutafuta sehemu ambapo ujangili umefanyika.

Kuna baa kubwa limezuka kwa watu kukosa uelewa na kufanya mambo ya kibinafsi hasa baadhi ya wafugaji, pale ambapo mfugo wake ameliwa na Simba na kuamua kuweka sumu kwenye mzoga wa ngombe huyo na kumtupa porini husababisha mauaji ya kutisha kwa wanyama walao mizoga kama vile Fisi, Bweha, Tumbusi na hata Simba. Hili ni jambo lililotokea kwenye maeneo ya hifadhi ya jamii na ilipelekea kupoteza idadi kubwa sana ya ndege hawa na wanyama wengine wala mizoga. Usiweke sumu kwenye mzoga utauwa na wanyama ambao hawahusiki na tukio la uharibifu.

Pia hata majangili wamekuwa wakiweka sumu kwenye mizoga ili kuwaua ndege hawa ambao hutoa ishara ya uwepo wa ujangili uliofanyika sehemu. Hili ndio changamoto kubwa sana kwenye usalama na uhifadhi wa ndege hawa, jamii na watu wengi hawaoni umuhimu wa ndege hawa hivyo huwaua kwa sababu mbali mbali. Na kusababisha kuharibu mfumo mzima wa ikolojia na maisha ya watu, kama nilivyoanza kwa utangulizi hapo mwanzoni mwa makala hii,kila kitu kwenye mazingira kina nafasi yake kwenye mfumo wa maisha na endapo kimoja kitaharibiwa basi ni ngumu sana kurudisha kwenye hali yake. Uwepo wa tumbusi ni muhimu sana kwenye nafasi ya kila kiumbe hai, sasa unapowaua Tumbusi, sijui wewe unayewaua na kuwawekea sumu unataka ufanye hizo kazi za Tumbusi za kula mizoga?

Nimalizie makala hii kwa kusema, kitu chochote ambacho kipo na hujui kipo kwa sababu gani, tafadhali sana kiache kama kilivyo maana ukianza kuingiza ujuzi wako au uzoefu wako utakiharibu. Nitoe rai kwa jamii na watanzania wenzangu hata kama hujui faida au sababu ya kuwepo kwa baadhi ya viumbe hai, tafadhali usiviue viache viendelee kuishi. Kama Mkuu wa Wilaya alivyolichukulia jambo la kuwawa kwa tumbusi kwa uzito sana na kusema mtu yeyote atakayeua Tumbusi hana tofauti na aliyeua Tembo. Ujangili wa Tembo ni sawa na ujangili wa Tumbusi, akamalizia kusema ukikamatwa unafanya vitendo vyovyote vya kiharibifu kama ujangili na kuweka sumu kwenye mizoga basi ujue hutabaki salama sheria itakapochukua mkondo wake.

Mwisho, nakushukuru sana Rafiki yangu kwa kusoma makala hii ndefu na yenye, naamini umepata mwanga na picha pana kuhusu ndege hawa na jinsi ambavyo wanamchango mkubwa kwa uwepo wa mfumo mzuri wa  ikolojia, lakini pia usalama wa afya zetu dhidi ya magojwa hatari. Kweli kabisa kama kauli mbiu isemavyo “Tumbusi ni sabuni ya mazingira”. Mshirikishe mwingine makala hii apate ufahamu na maarifa uliyoyapata. Pia nakukaribisha endapo unataka kujua zaidi kuhusu Tumbusi, au unamaswali, maoni au ushauri karibu tufanye kazi kwa pamoja ili kuhifadhi maliasili zetu.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania