Habari rafiki, karibu sana kwenye makala ya leo ambayo ni muhimu sana. Pamoja na kwamba nimechelewa kuandika barua hii kwa wakati katika siku ya askari wanyamapori duniani (World Ranger Day) ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 31 Julai, sasa zimeshapita siku kama saba. Lakini sikutaka siku hiyo ipite tu bila mimi kuandika chochote kuhusu watu hawa muhimu kwenye ulinzi na usimamizi wa wanyamapori wetu na maliasili nyingine. Nilitaka kuacha kuandika barua hii ya kuwapongeza na kuwaenzi mashujaa wetu hadi mwakani ila nikashindwa na kuona sio jambo la busara, nimeamua niandike kwa maneno machache  kwa sababu ya juhudi na kazi kubwa wanayoifanya kwenye ulinzi wa maliasili zetu.

Tarehe 31 Julai kila mwaka ni siku yenu askari wa wanyamapori, ni siku ambayo walikutana na kuundwa umoja wao ulioitwa “Shirikisho la Kimataifa la Askari Wanyamapori” (International Ranger Federations), ambayo pamoja na mambo mengine muhimu siku hiyo ni siku ambayo dunia inawaenzi maaskari wanyamapori waliopoteza maisha yao wakiwa kwenye majukumu yao ya kikazi, wakiwa katika ulinzi na usimamizi wa wanyamapori. Pia ni siku ambayo wanaheshimu na kutoa orodha ya maaskari wanyamapori waliouwawa au kupoteza maisha wakiwa kazini hivyo wana kitu kinaitwa  Ranger Roll of Honour, hii ni namna tu ya kuwaenzi mashujaa wetu kwenye uhifadhi wa maliasili zetu. Ukiangalia hiyo linki niliyoweka hapo utaona askari 105 ndio waliopoteza maisha kwa kipindi cham miezi 12 iliyopita wakiwa katika majukumu yao ya kikazi, hayo ni majina tu yaliyowasilishwa kwenye Shirikisho la Askari Wanayamapori Duniani. Inawezekana wapo wengi wamepoteza maisha lakini majina yao hayapo kutokana na kutowasilishwa kwenye shirikisho lao.

Ningependa kuwapongeza sana maaskari wanyamapori popote walipo duniani kwa kazi hii ngumu mnayoifanya kwa moyo na kwa kujitoa sana, maliasili zetu tunazojivunia ambazo ni wanyamapori na memea zisingekuwepo leo bila juhudi zenu za dhati za kuifanya kazi hii kwa weledi mkubwa. Natambua kuishi porini ilivyo changamoto, natambua kuishi mbali na familia kwa muda mrefu ilivyo changamoto, nafahamu hatari za mara kwa mara zilizopo porini hasa hatari ya majangili ambao wanasilaha na vifaa vya kisasa na vizuri kuliko ninyi. Pamoja na hayo yote hamkurudi nyuma hata kidogo, mlitumia kila ujuzi na mbinu mlizofundishwa kuhakikisha usalama kwa wanyamapori wetu.

Kuna siku niliangalia filamu moja inayoelezea maisha na hifadhi ya Virunga iliyopo Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, nilishangaa sana na kujua jinsi askari wanavyopata wakati mgumu kwenye ulinzi na usimamizi wa viumbe hai, ile filamu ilionyesha machafuko ya kivita jinsi yanavyo adhiri uwepo wa wanyamapori, niliona watu na askari wengi sana wa wanyamapori wakiuwawa kwa sababu ya kulinda maliasili za nchi zao. Ni kazi kubwa sana inayofanywa na askari wanyamapori.

Hii ndio sababu kubwa ya kuandika barua hii kwa askari wetu hawa wanaofanya kazi kubwa. Nilikuwa nataka kuacha kuandika barua hii kutokan na siku yenyewe ya askari wanyamapori kupita, lakini nikaamua kuandika tu ili kuwatia moyo na kutambua juhudi wanazofanya kwenye ulinzi na usimamizi wa wanyamapori na mimea yetu. Leo tungekuwa tunaongea stori nyingine kwenye maliasili nzetu, kutokana na ujangili uliokithiri miaka michache ya nyuma, lakini kwa kiasi kikubwa kumekua na hali ya kutia matumaini kwa miaka ya hivi karibuni, hii yote ni kazi nzuri iliyofanywa na askari wetu kwa kushirikiana na mamlaka husika. Hongereni sana mashujaa wetu.

Kwa askari wanyamapori Watanzania nawapongeza kwa kazi yenu bora sana na inayoonekana kwenye ulinzi na usimamizi wa maliasili zetu. Japo maeneo ya kuyalinda na kusimamia katika nchi yetu ni mengi na makubwa bado kazi yenu ya thamani kwenye uhifadhi wa wanyamapori na mimea yetu ni kubwa sana. Tunawashukuru sana kwa moyo wa kizalendo mlio nao, tunawashukuru kwa imani mliyonayo kwenye rasilimali za nchi yetu. Tunawashukuru sana askari wanyamapori Tanzania. Licha ya kutokuwepo kwa vifaa na vitendea kazi vya kutosha bado mmeendelea kufanya kazi hii kwa uaminifu na kwa kujitoa sana. Nimeona maaskari hawana magari ya kufanyia doria, nimeona maaskari hawana silaha za kufanyia doria, nimeona wengine hawana makazi au vituo (ranger post), nimeona wengine hawana mavazi, nimeona upungufu mkubwa mlio nao kwenye kazi yenu. Nimeona waliokosa misharaha yao kwa muda mrefu kutokana na kutokuwepo kwa fungu la kuwasaidia.

Lakini pamoja na upungufu wote huo wanafanya kazi kwa nguvu zao zote, wamejitoa kusaidia nchi yetu, wengine wana vilema sasa, wengine wameshapoteza maisha na kuacha familia zao na wake zao. Kwa siku yenu mnayosherekea kila mwaka nawapongeza kwa juhudi zenu na kwa mioyo ya uzalengo mlio nayo.

Wito kwa serikali, kama mnavyoona hali ya mambo ya utendaji katika sekta ya wanyamapori, inahitaji kuwekeza fedha, vifaa vya kisasa, na mafunzo kwa askari wetu, ili waendelee kufanya kazi zao kwa weledi na kwa viwango vya hali ya juu sana. Pia wadau wengine wa maendeleo, watu binafsi, mashirika, tunaomba msaada wa vifaa na vitendea kazi kwenye jambo hili.

Nawaomba watanzania wenzangu tuchangie na kuwaunga mkono mashujaa wetu wanaofanya kazi hizi za kusimamia na kulinda maliasili zetu. Naamini watanzania wana uwezo wa kutoa mchango wao wa mawazo, fedha, na hata vifaa kwa ajili ya kuboresha kazi hizi  zinazofanywa na askari wanyamapori. Tuungane na kushirikiana na Askari wanyamapori kulinda maliasili zetu.

Ahsanteni sana, Mungu awabariki Asakri Wanyamapori wetu kwa kazi kubwa mnazofanya kwenye sekata ya Maliasili. Tupo pamoja.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255683248681/+255742092569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania