Katika Sayari hii tunayoishi kuna mambo mengi sana yanatokea na yanatufanya kusumbuliwa kila upande. Utulivu umepungua hapa duniani, mambo yanakwenda kwa kasi sana, na matarajio ya watu wengi waliozoea mfumo mmoja wa kuendesha mambo umepotea kama sio kupoteza ladha na mwelekeo wake. Naamini kuna namna mambo yanavyotakiwa kuwa na kuendelea kuwa hapa duniani, japokuwa kumekua hakuna utulivu wala hakuna jawabu moja la kumridhisha kila mtu. Sheria na kanuni za asili bado zipo pale pale. Sayari hii aliyoiumba Mungu haijiendeshi tu kiholela bila mpangilio na kufuata kanuni kila kitu kinaenda kwa utaratibu wa kanuni za asili.
Ndugu msomaji wa makala za wildlife Tanzania, kama nilivyowahi kukuandiakia kwenye makala zilizopita kwamba kila siku za Jumapili nitakua naandika barua za wazi ambazo zinalenga kuleta mabadiliko kwa kila mtu hasa kwenye eneo la mazingira na mambo ya maliasili. Hivyo basi jumapili ya leo tunakwenda kuangalia vitu vya msingi na vinavyopaswa kuchukuliwa na kufanywa na kila mtu hasa kwenye mazingira yanayomzunguka. Ninaamini ingawa tunazungukwa na kuzongwa na mambo mengi bado kuna mambo yanayohitaji umakini na busara katika kuyafanya, ingawa kuna kelele nyingi bado kuna mambo ambayo hatupaswi kuyapuuzia kwenye mazingira yetu, pia ingawa kuna vipaumbele vingi tunavyojiwekea bado hata hiki tunachokwenda kujifunza hapa ni muhimu sana, hata kama tuna majukumu mengi kiasi gani bado kuna majukumu ya msingi ambayo hatupaswi kumsukumia au kumwachia mtu mwingine kuyafanya.
Kila mtu anaishi kwenye ardhi, hakuna mtu ambaye hatumii ardhi, fikiria hivi siku zote unapotumia hiyo ardhi kwa ajili ya shughuli zako mbali mbali, je, hiyo ardhi itafaa tena kutumika baadaye, fikiria watoto na wajukuu ambao bado hawajazaliwa je wataweza kuitumia kuzalisha kama unavyozalisha wewe sasa. Ndio kinaonekana kama ni kitu kidogo lakini nimeona watu wakifanya maamuzi yasio mazuri kwenye ardhi zao, wanafanya maamuzi ya kibinafsi, pia fikiria unachokifanya kwenye ardhi hiyo kina manufaa kwa mwenzako atakayekuja kuishi hapo endapo utaondoka au utauza eneo hilo. Fikiria hayo na fanya kwa wema usifanye kitu tu kwa kuangalia upande mmoja tu, angalia na upande mwingine unanufaikaje na maamuzi yako, ishi na fanya kila kitu chako kwa wema,kama ni ardhi usiifanye jangwa, usiiharibu kwa kuweka vitu vitakavyoifanya ardhi hiyo isitumiwe tena.
Vipi mtazamo wako upoje kwenye suala la utunzaji wa mazingira, bado una ile tabia ya kunywa maji au soda na kutupa chupa sehemu ambayo haistahili, je bado unaponunua vitu na kufungiwa kwenye mifuko ya nailoni au gazeti baada ya kutumia mifuko na magazeti au vifungashio vingine unatupa hovyo hiyo mifuko na vifungashio bila kuweka sehemu inayostahili? Ndugu yangu kwanini unafanya hivyo? Kila siku tunafundishwa kuhusu usafi wa mazingira yetu na umuhimu wake, lakini matokeo yake unapotoka barabarani au unapotembea na kuyaona makaratasi na mifuko ya lailoni imezagaa zagaa hovyo ujue tu bado watu hawajajitambua na hawajajua thamani ya mazingira kuharibika; kama kuna jambo linalonikera sana basi ni hili.
Kwa mfano upo kwenye gari umenunua maandazi au chipsi zako unakula ndani ya gari halafu baada ya kula unatupa vifungashio au hiyo mifuko nje ya gari kupitia dirishani, aisee huwa naumia sana, halafu mbaya zaidi unaweza kukuta ni mtu mzima kabisa anafanya jambo hili, je anatoa taswira gani kwa wanaomwangalia. Ingawa kwenye magari na sehemu zetu kwenye mazingira tunayoishi kuna maeneo maalumu ya kuweka uchafu na taka zote ambazo unatumia lakini bado watu wanaendelea kutupa hovyo bila utaratibu, hawaangalii sehemu ya kutupa hizo taka wanatupa tu ili mradi. Kuna mtu mmoja alifanya jambo la namna hii, nika muuliza haloo, mbaona unatupa matakataka yako nje kwanini usiweke ndani ya gari hili kuna sehemu ya kuhifadhi uchafu? Alichonijibu daah, nilichoka alisema wapo watu wataokota huko nje.
Mitazamo tuliyonayo kwenye utunzaji wa mazingira sio mzuri, kwanini ufikiri mtu mwengine aje afanye kitu ambacho ulipaswa kukifanya, kwanini usianze wewe mwenyewe kwanza. Hata kama upo na wenzako wengi ambao wana tabia za namna hii usiwaige waonyeshe mfano, waelekeze namna ya kuweka uchafu sehemu inayostahili. Hata kama wakikataa wewe endelea kufanya jambo jema wakati wote, hata kama unajua ukitupa taka taka hakuna anayekuona na kukuchukulia hatua za kisheria usifanye jambo hilo, fanya jambo jema na sahihi wakati wote hata kama hakuna anayekuona. Tuyahurumie mazingira yanayotulea, tuyafanye mazingira yetu kuwa sehemu bora ya kuishi viumbe wengine.
Pia kuna wanaochafua vyanzo vya maji, au kutupa taka kwenye maji yanayotumiwa na mamilioni ya watu. Unaweza kuwaona watu wanaoga mtoni, wananywesha ng’ombe, wanafulia nguo zao humo, wengine wanaoshea magari yao humo, wengine wanatumia mito ya maji kama sehemu za kutupa taka taka mbaya na uchafu wa majumbani. Ukiangalia sheria za mazingira zinakataza jambo hili lakini watu hata hawasikii, pia kuna watu wengine wanajisaidia ndani ya maji yanayotumiwa na watu wngine, looh! Tutaepukaje magonjwa kwa namna hii ya maisha, kila mtu anafanya tu kwasababu anaona anapata faida yeye binafsi bila kuwaangalia mamilioni ya watu wengine wanaotumia rasilimali hiyo. Tunatakiwa kufikiri mara mbili kwenye jambo la namna hii ili tuokoe mazingira yetu na maisha yetu pia.
Madhara yanayotokana na uchafuzi na uharibifu wa mazingira ni makubwa sana, kwanza kabisa tunaharibu mfumo wa hewa, pili tunaharibu mfumo wa maisha ya mamilioni ya viumbe hai ambavyo ni wanyama na mimea. Hebu fikiria mtu ana kiwanda ambacho kinaelekezea maji yake kwenye sehemu za makazi au mazingira ya wanyamapori na watu. Hapo moja kwa moja hakuna usalama kabisa kwani ni kuhatarisha afya za viumbe hai na mfumo wa maisha yao. Kwanini tusifikiri mara mbili mbili, ubinafsi uta tuua, ubinafsi utawanyima haki ya kuishi watoto na vitukuu vyetu, ubinafsi utawanyima haki ya kuishi wanyamapori na viumbe wengine, ubinafsi utaiharibu na kufanya mazingira ya kuishi nkuwa magumu sana kwa mimea.
Ewe mtanzania, ee rafiki yangu unayesoma barua hii hadi kufikia hapa, naomba nenda kafanyie kazi haya uliyojifunza, nenda tu kafanyie kazi hata kama utakuwa mwenyewe unayefanya jambo hili jema kwenye jamii yako, nakuahidi hauko peke yako, dunia itakushukuru, viumbe hai watakushukuru na pia kwa kufanya jambo hili la kutunza mazingira utakuwa unafanya maagizo ya Mwenyezi Mungu, kama alivyotupa Sayari hii nzuri yenye ukamilifu wote na kutuagiuza tuitunze, basi hatupaswi kufikiri kuna mtu bora sana kuliko sisi atakayekuja kuyatunza na kuyahifadhi mazingira yetu, hakuna, ni sisi wenyewe. Na pia hakuna muda mwengine mzuri wa kuanza kufanya jambo hili kama sasa.
Nimalizie kwa kukushukuru maana naamini utakwenda kuchukua hatua za makusudi kwenye jambo hili, uatawafundisha wengine jambo hili. Jiwekee akiba ya wema kwa kuwa mmoja ya watu ambao wanasababu ya kuishi hapa duniani kwa sababu ya kuwatengenezea watu na viumbe hai wengine mazingira bora ya kuishi. Fanya kila kitu kwa upendo, hisia na maamuzi yako yawe yenye tija kwa wengi zaidi. Washirikishe wengine maarifa haya utaiokoa dunia na Tanzania kwenye uharibifu na hasara zitokanazo na uharibifu wa mazingira.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255742092569/ +255 683 862 481
www.mtalaamu.net/wildlifetanzania