Habari za Jumapili ya leo Rafiki yangu, karibu kwenye barua ya leo, barua hii kama nilivyowahi kukuandikia kwenye makala zilizopita kwamba kila Jumapili ni siku ya kupata barua moja ya wazi ambayo itatutufakarisha na kutufanya kuchukua hatua stahiki. Katika barua ya leo tunakwenda kumulika eneo moja ambalo ni muhimu lakini tunashindwa kupata muda na mazingira mazuri ya kutosha kulitumia. Lakini baada ya kuangalia kwa makini maisha yetu nimegundua, hatujakosa muda wa kupumzika, bali tumekosa na mazingira ya kupumzika. Hivyo karibu kwenye makala hii tuone jinsi ambavyo tunaharibiwa mazingira yetu ya kupumzika.
Kwanini nimesema tunakosa mazingira ya kupumzika? Hii ni kwasababu ya uhalisia wa maisha yetu ya kila siku, na jambo hili lipo kwa kila mtu, kama ni mfanyabiashara utakutana na watu kwa ajili ya biashara yako, kama ni mfanyakazi utakutana na watu ili kufanikisha kazi yako. Kimsingi kwa kiasi kikubwa sana tunakuwa tumezungukwa na watu wengi na kwa hali ya namna hii ukisema unapumzika utakuwa unajidanganya. Hii ni kwasababu ya uhalisia wa maisha yetu, hata ukisema nitakwenda nyumbani kupumzika, sio keli kwamaba unakwenda kupumzika huko nyumbani bado kutakuwa na usumbufu.
Kelele kwenye maisha yetu zipo kila mahali, nyumbani kuna kelele, ukienda kazini nako kuna kelele, ukienda shuleni nako kuna kelele, ukienda kuwatembelea wazazi au ndugu zako bado unakuwa hujatatua tatizo la kelele. Kelele zipo kila sehemu ya maisha yetu. Na kwa kiasi kikubwa ni ngumu kushinda hali hii. Hivyo kusema unahitaji muda mzuri usio na usumbufu wa aina yoyote utakosa, na hapa nimekuja kugundua sio kwamba watu wanakosa muda pekee wa kupumzika, lakini pia wanakosa na MAZINGIRA kupumzikia.
Rafiki yangu, kama kweli unataka kupumzika na usiwe na usumbufu wowote kwenye mapumziko yako, unatakiwa kufikiria zaidi. Kuna wengine wanafikiri kukaa nyumbani na familia zao ndio watakuwa wamepumzika, kumbuka nyumbani ndio sehemu yenye kelele nyingi na usumbufu mwingi sana, wata watakupigia simu, kuna redio, kuna televisheni, kuna majirani, tena wakijua una likizo ya mapumziko watakutembelea hadi nyumbani, watoto nao hawatakuacha hivi hivi, kuna changamoto za hapa na pale ambazo watu wanahitaji msaada wako kuzitatua, tena wakati mwingine utakaa hapo nyumbani kwako na kuoona kitu fulani hakijakaa sawa na utaanza kukifanyia kazi. Hivyo utaendelea kuwa na shughuli zako kila siku bila kupumzika vya kutoshahadi likizo inaisha na unarudi tena kwenye shughuli zako za kila siku, hivyo unajikuta unafanya hivyo kwa miaka mingi.
Na usipoangali kwa makini utakuta unafanya jambo hilo kwa muda mrefu kwa maisha yako yote bila kutambua. Kwanini ni muhimu kuwa na muda na mazingira mazuri ya kupumzika? Kwasababu ni muhimu kuyatafakari maisha yako, nimuhimu kutafakari mambo mbali mbali unayoyafanya kwenye maisha yako, ni muhimu kwa sehemu tulivu kabisa isiyo na usumbufu wowote kwa ajili ya kuangalia na kupitia tena maono yako binafsi, maono ya familia yako, na maono ya jamii yako. Kufanya mambo haya unahitaji utulivu wakutosha usiosumbuliwa na kitu chochote. Tafakari ni muhimu sana kwenye maisha, kwa sababu itakusaidia kupungua makosa ya mara kwa mara unayofanya kwenye maisha yako, pia tafakari itakupa nguvu za rohoni, na hamasa ya kusonga mbele na kufanya mambo makubwa.
Swali linakuja unapataje mazingira mazuri na tulivu ya kufanya mambo hayo? Mazingira yapo mengi sana ya utulivu na yenye hadhi nzuri sana ya kukufanya utulie na kufikiria kwa kina maisha yako ya baadaye. Tanzania ina maeneo mengi sana yenye utulivu kwa ajili ya watu wanaopenda kutembelea sehemu mbali mbali. Kuna misitu, kuna fukwe za bahari, kuna hifadhi na mbuga za wanyama nyingi sana. Haya ni maeneo ambayo yana utulivu mkubwa sana kwa ajili ya kukaa wewe mwenyewe au wewe na familia yako. Kuna maeneo yenye maporomoko ya maji, kuna sehemu zenye hali nzuri sana ya hewa ambapo hakuna mtu unayemfahamu huko ili aanze kukusumbua au kukutembelea.
Watu wengi hatuna utamaduni wa kutembelea vivutio au sehemu zenye hali nzuri ya utulivu kwa ajili ya kufikiria namna ya kupanga maisha yako na namna ya kutekeleza malengo yako. Umezoea ukipata likizo unakimbilia kwenda nyumbani kwenu, unafikiri kwenda nyumbani kwenu ndio utapumzika vizuri, sio kweli tena uaenda kuongeza msongo wa mawazo na hali hiyo itapelekea kukosa muda wa kuyafurahia maisha yako. Kwa kusema hayo simaanishi kwamba kwenda nyumbani kijijini kwenda kuwaona wazazi ni vibaya, la hasha!, kwenda huko ni jambo jema tena la baraka. Lakini leo nataka tufikiri wakati uanapoamua kwamba unataka kupumzika sehemu ambayo unahitaji muda na mazingira ya kutosha ili utulie biala kuona au kusumbuliwa na kitu chochote kile.
Jambo hili ndio linaloniaminisha sababu kubwa ya wazungu na watu wengine wanaolipa gharama kubwa kwa ajili ya kupata mazingira yanayofaa kwa ajili ya kufurahia maisha yao binafsi. Tena wengi hupenda kwenda sehemu za mbali sana ambazo hakuna mtu wanayefahamiana naye, hasa huku Afrika. Wengi huja kujifunza kutafakari na kupitia safari za maisha yao. Wanajua kule kwao hakuna utulivu, na pia hakuna mazingira mazuri ya utulivu, hivyo huingia gharama ya kusafiri kwenda kutafuta mazingira bora kwa ajili yao.
Angalia namna unavyoweza kupangilia likizo yako, fikiria unataka mapumziko ukiwa na nani, je unataka usafiri na familia yako, au wewe binafsi au ukiwa na mwenzi wako? Hivi ni vitu vya msingi au unataka kusafiri na ndugu jamaa na marafiki? Tafuta mazingira bora ya kupumzika na kuyapitia maisha yako, ni bora ulipe gharama kubwa kupata mazingira bora na upumzike kuliko kuendelea kukaa sehemu zenye makelele na kushindwa kupumzika.
Naelewa kipindi hiki watu wengi wanapanga kwenda kwenye mapumziko maeneo mbali mbali. Niameandika makala hii kukupa mwanga na kukwambia nenda sehumu usiyoijua, na kwa watu usiyowajua wazungu wanasema “take adventure” kama unataka mapumziko na hujui uende wapi, usisite kuwasiliana nami kwa mawasiliano yaliyopo mwisho wa makala hii.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania