Habari Rafiki, karibu kwenye barua ya leo ambayo tunajifunza haki na wajibu wetu kwa jamii yetu hasa kwenye mambo yanayohusu mazingira na maliasili zake. Kwa miongo mingi tumeishi na kuona mienendo mizima ya watu waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za nchi yetu kuwa sio waadilifu. Kwa muda mrefu tumekuwa hatushiriki kwenye masuala ya usimamizi wa rasilimali za nchi yetu kwa maana ya kufuatilia na kujua kwa undani mambo yote yanayofanyika ndivyo sivyo kwenye maliasili hizi, tumewaamini sana viongozi na watendaji kwenye usimamizi wa rasilimali hizi, hivyo tumejiondoa kweye ushiriki na hata usimamizi wa rasilimali hizi. Jambo ambalo ni kinyume na katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba 5 ya mwka 2009, na sheria nyingine za ardhi zinatamka wazi kuwa rasilimali zote zilizopo katika ardhi ya Tanzania ni mali ya watanzania wote, na wana wajibu wa kulinda na kuhifadhi maliasili hizo. Pia sheria imetamka wazi maliasili zote za nchi zinamilikiwa na serikali kwa niaba ya wananchi wote. Hivyo unaweza kuona sehemu nyingine imeandikwa rasilimali zote za nchi zipo chini ya Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya wananchi wote. Ndio maana serikali imetunga sheria na sera mbali mbali za kusimamia rasilimali hizi, pia imeteua na kuweka watu mbali mbali kwenye sekta hizi kwa ajili ya kuhakikisha rasilimali za nchi zinatunzwa na kuwanufaisha wananchi wote kwa mujibu wa sheria.

Kwa kuwa sheria zipo wazi kwamba ni wajibu wa raia wote wa Tanzania kushiriki na kusimamia maliasili za nchi kwa maslahi makubwa na mapana. Hii ikiwa na maana ya kwamba jamii inatakiwa kuelewa kinachoendelea kwenye maliasili zetu, kuwahoji viongozi na wasimamizi wa rasilimali hizo, wananchi wanatakiwa kuwa wakali kudai utekelezaji wa wazi wa shughuli zote za ulinzi na usimamizi wa maliasili hizi muhimu. Ni haki ya wananchi kudai uwajibikaji, kudai taarifa za mapato na matumizi, kudai au kujua matumizi na njia za uwekeaji kwenye ardhi yao.

Lakini mambo hayaendi kama inavyotakiwa kwenye sheria. Hii ni kutokana na watu wengi kutojua wajibu wao kisheria na hakuna watu waliojitolea kuwafundisha wanajamii kuhusu haki zao, wengine ni waoga wanaogopa kuwahoji viongozi, wanaogopa kuuliza maswali viongozi wao, wangine hata hawashiriki kwenye semina na mikutano ya vijiji kuhusu maliasili zao. Hili ndio jambo lililonifanya nikaandika makala hii ili angalau watu wafahamu kuwa suala la ushiriki kwenye uhifadhi wa wanyamapori na misitu pamoja na rasilimali nyingine za nchi ni la jamii nzima, na kila mwanajamii ana haki ya kufahamu na kujua taarifa aza kiutendaji, mapato na matumizi, hali ya uchumi na uwekezaji kwenye maeneo yao.

Sasa kwa kuwa watanzania wengi tumejengewa hofu, na wakati mwngine sisi wenyewe tumejijengea hofu kwamba hatuna haki ya kuwauliza uliza viongozi na watendaji maswali. Tumekuwa wapole mno na kuwaachia viongozi na watendaji kwenye sekta hii mwanya mkubwa sana wa kufanya mambo ya hovyo bila kuzingatia sheria. Tunatakiwa kuamka na kusimamia rasilimali zetu, tunatakiwa kufahamu na tunatakiwa kadai uwazi na uwajibikaji kwenye maliasil zetu.

Hivyo ni haki na wajibu wetu kufuatilia na kunufaika na rasilimali zetu, tunahitaji elimu ya utambuzi wa masuala ya kisheria kuhusu haki zetu za msingi hasa kwenye masuala ya maliasili. Kutokujua haki na wajibu wetu kumetufanya kuwa waoga na wasioweza kuhoji chochote kwenye maliasili, lakini kwa elimu mbali mbali watu wataelewa kuwa wajibu wao mkuu kwenye jamii ni ulinzi na usimamizi wa rasilimali zao ili ziendelee kuwa endelevu, na pia tutakuwa wakali pale ambapo watu wanaharibu mazingira au wanakiuka matakwa ya sheria kwenye usimamizi na hata wakati wa kutoa faida kwa jamii. Na hii ndio sababu mashirika na miradi mingi inapokuja kwenye jamii inajikita kwenye kuelimisha jamiikuhusu elimu ya mazingira na uhifadhi wa wanyamapori. Lakini nimegundua kuwa ni mashirika machache sana yanayojikita kwenye utoaji wa elimu ya sheria na kuhusu haki na wajibu wa wananchi hasa kwenye masuala ya rasilimali na usimamizi wake.

Kwa hali ilivyo kwenye maeneo mengi bado tunahitaji elimu hii iendelee kuwepo na kuwafikia watu wengi zaidi ili wajifunze na kuwa wawajibikaji. Pia sisi wenyewe wananchi tunatakiwa kufuatilia na kujifunza vitu hivi kwa nguvu, tusisubiri mpaka ubembelezwe, unatakiwa kutafuta maarifa na taarifa sahihi ambazo zinamsaada mkubwa kwa kila mtu. Wakati kunapokuwa na mikutano na semina tunatakiwa kuwa msitari wa mbele kwenda kusikiliza na kujifunza vitu hivi kwa undani. Ili tujue haki zetu na wajibu wetu kwa nchi na jamii yetu.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania