Habari msomaji wa makala za mtandao huu wa wildlife Tanzania, karibu tena siku ya leo kwa ajili ya kujua na kujifunza mambo muhimu niliyokuandikia kwenye barua hii. Kwenye barua kama hizi ninazokuwa naandika kila jumapili huwa naandika mambo ya jumla kwa watanzania wote ili kwa namna moja au nyingine tubadili mitazamo tuliyo nayo kuhusu maliasili, utalii, na utunzaji wa mazingira. Kwenye barua hii nitaelezea tabia ya uzalendo hasa uzalendo kwa nchi yeu wenyewe. Uzalendo ni dhana pana kidogo inagusa mambo mengi lakini msingi wake mkuu ni tabia ya wazi inayoonekana na watu wengi. Ni dhamira ya dhati ya kusimamia maslahi mpana ya nchi, kutetea, na kusimamia kwenye haki kwa ajili ya wengi.
Uzalendo ninaoongelea hapa nitalenga kwenye uhifadhi wa maliasili zetu. Na ninaamini kabisa huwezi kuwa mzalendo ukakosa uwajibikaji, uwajibikaji unaenda sambamba na uzalendo, kiongozi akiwa mzalendo anawajibika, mwananchi akiwa mzalendo huwa anawajibika. Kwenye sheria na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka kuwa kila wananchi ana wajibu wa kusimamia na kutunza rasilimali za nchi. Na rasilimali zote zilizopo kwenye nchi yetu ya Tanzania ni mali ya watanzania wote. Na serikali imeamua kutunga sheria na kanuni mbali mbali kwa ajili ya usimamizi na uhifadhi wa rasilimali hizi na kuhakikisha uwepo wa rasilimali hizi unawanufaisha wananchi wote.
Hivyo basi, jambo la msingi tunalotakiwa kujua ni kuwa popote pale tulipo tuna wajibu mkubwa wa kuzitunza, kuhifadhi na kunufaika na rasilimali za nchi hii. Watu wanapofanya wajibu wao ni rahisi sana kupewa haki yao au kudai haki zao. Kwa mantiki hii sisi kama watanzania tunapaswa kuelewa kuwa kutunza mazingira ni moja ya majukumu yetu ya msingi kikatiba na kisheria. Pia tunatakiwa kuelewa kuwa tunapoona mambo yanakwenda bila taratibu tuwajibike na kusema ili yarekebishe. Tunapoona viongozi na wasimamizi waliowekwa kusimamia maliasili zetu wanakula rushwa tunatakiwa kuwawajibisha mara moja, au wanashindwa kutimiza mambo yao ya msingi tunatakiwa kuwakemea huu undio uzalendo.
Kuna wakati mambo yanakewanda hovyo sana kwenye sekta ya maliasili, kuna watu ambao sio waaminifu, wanafanya mambo ya kuhujumu rasilimali za umma ili wazitumie kwa maslahi yao binafsi, na watu wengine wanashiriki na wengine wanatambua na hawasemi chochote wanaacha mambo hayo kuwa hivyo. Tutoe sauti za kizalendo kukemea ubinafsi na watu wenye nia mbaya na maliasili zetu. Pia kuna wakati tunawaona wenzetu wakiharibu vyanzo vya maji, wakikata mito hovyo, wakichoma moto hovyo na tunawaacha bila kuwachukulia htaua zozote. Huu sio uzalendo wa kweli kwenye maliasili zetu. Najua kuna changamoto kubwa kwenye mambo haya lakini jifunze kuwa mkweli na mtetezi wa watu wengine, ambao ni viazi vijavyo.
Wazalendo ndio wanaokumbukwa kwa mema na vizaji vijavyo, wanakumbukwa kwa ujasiri na kusema ukweli, dunia inawaheshimu watu wazalendo, watetezi na wenye dhamira ya dhati ya kuinufaisha jamii ya sasa na jamii ijayo. Hivyo tunatakiwa kufikiri kwa mapana juu ya vizazi vijavyo, tunatakiwa kuelewa kuwa sauti yetu na juhudi zetu za kuhifadhi mazingira na maliasili nyingine zitawasaidia na kuwagusa wao. Nakupa shauri uwe sauti ya vizazi vingi vijavyo, toa sauti yako kupinga uharamia, rushwa na tamaa mbaya ambayo hutishia kuharibu maliasili zetu.
Mwisho, tuwajibike, tuwe wazalendo na tuache urithi wa kutosha kwa vizazi vijavyo. Kuwa sehemu ya kutenda wema na kuacha alama ya wema kwa jamii yako nchi yako, na popote pale ulipo. Asante sana nakutakia siku njema na tafakari nyema. Mungu akubariki sana.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania