Habari za leo rafiki na msomaji wa makala za Wildlife Tanazania, karibu kwenye barua ya jumapili ya leo ambayo tunaangalia upande mwingine wa uhifadhi. Na leo hatuangalii uhifadhi kwenye nchi kavu kama vile hifadhini au kwenye mapori ya akiba, leo tunaingia baharini, tunaangalia uhifadhi kwenye maeneo ya bahari, mziwa na mito. Kuna siku niliandika makala hapa inaelezea dhana pana ya uhifadhi wa wanyamapori, nikaelezea kwa kina vitu vinavyoguswa tunapozungumzia uhifadhi wa wanyamapori na sikuacha kuitaja bahari maana uwepo wake ni muhimu sana kwenye kuwezesha kukamilika na kukaa sawa kwa ikolojia ya wanyama, mazingira na mimea.
Kama nilivyowahi kukuandikia kwenye makala zilizopita kuwa siku ya jumapili ni siku ya kupata barua ya wazi, barua ambayo ni ya kila mtu anayeishi juu ya uso wa ardhi, barua hii inamuhusu kila mtu kwasababu kila mtu ana nafasi yake kwenye utunzaji na uharibifu wa mazingira. Kwa asilimia kubwa kuharibika kwa mazingira yetu ya asili, kupotea kwa udogo na kuenea kwa ukame na mabadiliko ya tabia nchi yanasababishwa na shughuli nyingi za kibinadamu. Hivyo naamini kupitia makala hii tunaweza kupata maarifa ya kuamua kuacha vitendo na shughuli zote ambazo zinatishia uharibifu wa mazingira. Pia naamini kupitia makala hizi tutakuwa na uelewa mpana wa kujua mazingira yakiharibika sehemu moja madhara yake yatasambaa na kwenda mbali zaidi na kuwaathiri watu wengine sehemu nyingine duniani, lakini si hivyo tu madhara yake yanaweza kwenda kuathiri mamia na mamilioni ya maisha ya vizazi vijavyo.
Katika barua ya leo nataka tuangalie kwa uchache uhifadhi kwenye fukwe zetu za bahari. Tanzania ni nchi ambayo ipo kwenye moja ya nchi za mashariki mwa Afrika, kuna nchi nyingine ambazo zipo mashariki mwa Afrika ambazo ni Kenya, Uganda, Ruanda na Burundi, hizo ni baadhi tu kwa uchache ila zipo nyingi. Kati ya nchi hizo Tanzania na Kenya ndio nchi pekee zilizopakana na bahari ya Hindi kwa upande wa Mashariki. Kuna faida nyingi sana za kiuchumi, kijamii na kimazingira ambazo zinatokana na uwepo wa bahari au kupakana na bahari, mimi sitazungumzia faida za kiuchumi wala kijamii ingawa uhifadhi mzuri kwenye maeneo haya ya bahari ndio hasa husababisha uwepo faida zote za kiuchumi, kijamii na kimazingira.
Kwa wale ambao walishawahi kutembelea maeneo ya bahari au kwenye fukwe za bahari watakubaliana na mimi kuwa kuna mazingira ya aina fulani fulani, kwenye fukwe hizi kuna mchanga, kuna uoto wa nyasi, kuna uoto wa mikoko (mangroves) na pia kuna uwpo wa miamba inayojulikana kama coral reefs, hivi ni baadhi tu ya vitu ambavyo vinaweza kuonekana unapokwenda baharini au kwenye fukwe za bahari. Kwa hakika hakuna ambacho kipo maeneo hayo kwa bahati mbaya au kimejiotea tu bila sababu yoyote kila kilichopo kwenye maeneo haya kinasababu yake kubwa sana ya kuwepo pale, na cha ajabu kabisa ni kwamba sio kila uoto unaweza kuota maeneo haya, maeneo haya yana aina yake maalumu ya uoto ambao hustawi na kushamiri sana kwenye maeneo haya ya fukwe na huwezi kukuta mahali popote uoto huu umeota, lazima iwe ni kwenye maeneo ya kingo za bahari, pwani, maziwa na mito mikubwa.
Kuna siku nilikuwa nasoma gazeti moja maarufu kwa ajili ya mambo ya uhifadhi wa wanyamapori, mazingira na mambo ya utalii wa uwindaji gazeti hili linaitwa “Miombo” kwenye ukurasa wa kwanza kabisa niliona kichwa cha habari kilichoandikwa kwa kingereza “The Protective Role Of Coastal Mangroves Against the Destructive Forces Of Tsunami”. Yaani kwa Kiswahili kisicho sanifu anamaanisha Ulinzi wa Mikoko ya pwani dhidi ya nguvu za uharibifu zinazosababishwa na tsunami. Mwandishi wa makala hiyo alirejea nyuma kuelezea tukio la kihistoria kuwahi kutokea kwenye maeneo mengi ya pwani ya bahari ya Hindi, alielezea madhara makubwa yaliyosababishwa na tsunami, nchi zilizoharibika zaidi na ambazo hazikuharibika sana. Pia aliandika sababu zilizopelekea maeneo mengine ya nchi kuwa na uharibifu mkubwa na mbaya na mengine kuwa na uharibifu wa kiwango cha kawaida na hapo ndipo alipotaja sababu zilizopelekea madhara kuwa makubwa kwenye baadhi ya nchi zilizoathiriwa na tetemeko hili lililotokea chini ya bahari na kusababisha mawimbi yenye nguvu kubwa sana na kusababisha uharibifu wa mali na maisha ya watu kupotea.
Aidha kwa wale mnaokumbuka vizuri tetemeko hili kubwa la chini ya bahari lilitokea mwaka 2004 katika Pwani yote ya bahari ya Hindi. Mwandishi wa makala hiyo alieleza vizuri kuwa sehemu ambazo hazikupata madhara mabaya ni sehemu ambazo Pwani au fukwe zao zilikuwa na misitu ya mikiko na coral reefs, ambazo zilitumika sana kupunguza nguvu za uharibifu za mawimbi ya bahari kuwafikia watu na makazi yao. Ukienda baharini utaona misitu minene ya kinaji ilijiotea kwenye kingo za fukwe au kando ya bahari misitu hii ndio hujulikana kama mikoko au kwa kingereza inaitwa mangrove, hii ni misitu muhimu sana na ina nguvu za ajabu sana kiasi cha kuzuia mawimbi yenye nguvu yanayosababishwa na matetemeko chini ya bahari au nguvu nyingine za bahari. Tofauti na misitu na miti mingine hii ndio miti ya ajabu sana ambayo ina kazi yake kwenye maeneo haya ya bahari.
Hakika, kila alichokiumba Mungu alikiwekea mipaka na kanuni zake za kufanya kazi, hakuna alichoumba Mungu ambacho kipo kipo tu bila kuwa na kusudi lake hakipo. Fikiria Mungu alipoiweka bahari alijua kabisa kuna siku bahari itajaa, kuna siku kutakuwa na matetemeko amabyo yatasababisha mawimbi makali na yenye hatari kwa binadamu, hivyo akaamuaa kuruhusu mikoko na mimea mingine kuota kwenye maeneo haya kwa ajili ya kazi hiyo tu. Na hakuruhusu mti wowote kuotea tu, aliweka miti yenye nguvu, na inayoweza kuota kwenye maji ya chumvi na yenye uchafu na makemilali mengi ambayo kwa kawaida mimea na miti mingine isingeweza kuota kwenye mazingira hayo.
Cha ajabu na cha kusikitisha zaidi sisi binadamu tunajifanya wajuaji mno, tunaangalia mambo mafupi na kutatua mambo ya muda mfupi kwa kuharibu mambo mazuri ya muda mrefu. Kutokana na makala nilioisoma inaonyesha kuwa maeneo yote yenye uharibifu wa mikiko na misitu hii ambayo huota kwenye fukwe za bahari ndio sehemu ambayo madhara mabaya ya tsunami yametokea, nchi kama Thailand ambako wameharibu kabisa fukwe na kukata misitu ya kingo za bahari, upanuzi wa maeneo ya kilimo umesababsha uharibifu mkubwa wa maeneo haya. Kwa Tanzania na nchi nyingine zenye maeneo haya yenye mikoko na misitu mingine kwenye Pwani za bahari zao hawana budi kutunza na kuweka usimamizi mzuri wa maeneo haya. Kwa Tanzania maeneo haya ya misitu ya Pwani au mikoko ipo mingi na inatakiwa kuhifadhiwa na kusimamiwa vizuri sana.
Uhifadhi wa maeneo haya, sio tu kwa ajili ya kuzuia nguvu za uharibifu wa mawimbi ya bahari laikini sehemu hizi ni muhimu kwa ajili ya mamia na maelfu ya viumbe hai kama vile ndege, wanyama jamii ya nyani, kima, makazi ya aina za samaki na sehemu muhimu za reptilia kama vile kobe, mamba na wanyama wengine muhimu kwenye ikolojia ya majini au baharini. Uhifadhi kwenye maeneo haya utasidia sana kuokoa maisha ya binadamu na maisha ya viumbe hai wngine. Aidha endapo juhudi kubwa za uhifadhi zitafanyika kwa umakini maeneo haya ya pwani ni muhimu sana kwa utalii, maeneo ya fukwe za bahari yakiwa na mandhari nzuri zenye kuvutia na za asili basi zitakuwa ni kivutio kikubwa sana kwa watalii kuja kutembelea na kwa njia hii tutapata fedha nyingi za kigeni.
Asante Rafiki yangu kwa kusoma makala hii, naamini umepata mambo mapaya ya kukusaidia kuchukua hatua nzuri kwenye uhifadhi wa maeneo haya ya fukwe za bahari, na pia naamini utakuwa mwalimu mzuri na balozi mzuri kwa wanaotaka kufanya shughuli za kuharibu mazingira ya maeneo haya ya fukwe za bahari na maeneo mengine muhimu. Endelea kujifunza hapa na kuwashirikisha wengine makala hii.
Ahsante sana
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569