Habari rafiki yangu kwenye sekta hii ya wanyamapori, karibu tena siku ya leo tuweze kumulika mambo ambayo yanatukwamisha kusonga mbele kwenye sekta hii pia inaweza kuwa na kwa sekta nyingine. Kati ya vitu vinavyochangia maendeleo sehemu yoyote ile duniani ni mitazamo na fikra zilizo sahihi ambazo zinawawezesha watu kuchukua hatua muhimu kwa maslahi mapana. Ninapozungumzia fikra hapa namaanisha mkusanyiko wa mambo mengi yaliyojengeka na kujengwa katika fahamu na akili za watu kwa miaka mingi, ambayo ndio yanatengeneza mfumo wa maisha wenye kuamini sawasawa na fikra za mtu huyo. Fikra zinaweza kuwa nzuri zenye manufaa na mchango mkubwa kwa mtu kupiga hatua kwenye maisha au zinaweza kuwa fikra mbaya ambazo haziwezi kubadilika na kukubaliana na hali duni ya maisha na kuamini kwamba hakuna njia au namna nyingine ya maisha tofauti na wanavyoamini.
Hii ndio changamoto kubwa sana kwenye jamii yetu, ambayo imejengwa kwenye mifumo duni ya utamaduni ambao kwa kiasi kikubwa hauna maslahi mapana kwa jamii, kutokana na malezi na makuzi kwenye jamii zetu, mifumo ya elimu ambao umetufanya kuwa wabinafisi, na wasio na maono makubwa kwa nchi yetu ndio yanayowatesa wengi sana ukianzia na viongozi mpaka wazazi wetu wa nyumbani. Tumejengwa kwa kiasi kikubwa kwenye kutokujiamini na kutokuamini vile tulivyo navyo, kwa watu binafsi, viongozi wetu na hata kwenye rasilimali zetu. Ehee! Nisiwe mwanafalsafa sasa kukueleza haya, ngoja sasa tuingie kwenye somo la leo.
Ukisikia utalii unawaza nini? Au ukisikia meneo yenye vivutio unafikiria nini na nani? Au ukasikia hifadhi za Taifa na wanyamapori ni mtazamo gani unakuwa nao? Haya maswali na mengiene mengi ndio yamenifanya kukaa chini na kuandika makala hii. Maswali yote hayo yanaweza kuonyesha ni kwa kiasi gani tunahitaji elimu ya ukombozi wa kifikra dhidi ya namna tunavyochukulia mambo hayo na jinsi ambavyo tunahitaji kukombolewa kutoka kwenye fikra duni zilizopo kwa watu wengi.
Kuna watu wakisikia tu mambo yoyote ya utalii au vivutio mbalimbali vinavyopatikana hapa Tanzania na sehemu nyingine wanajitoa na kuona wao hawahusiki na hawawezi kuwa watalii, pili kinachowajia haraka kwenye akili zao zilizozoeshwa kwa miaka mingi kwamba mtalii ni mzungu tu, na wala hawezi kuwa yeye au watu wengine ambao sio wazungu. Dhana hii ya kufikiri hivi inamadhara makubwa sana kwa mtu mmoja na kwa jamii nzima, kwani mzazi au kiongozi mwenye kufikiria watalii ni wazungu tu, hivyo ndivyo anavyoamini na ndivyo atakavyo wafundisha watoto wake na watu wengine, kwa hiyo jamii nzima inaamini hivyo, na ikiamini hivyo kwa muda mrefu hapo ndipo inapokuwa ndio mfumo wa maisha na mfumo wa maisha ndio unaojenga tamaduni tulizo nazo.
Sasa tukiwa na jamii inayoamini hivi kwa muda mrefu kwamba wao hawawezi kuwa watalii na watalii ni wazungu tu, kazi ya kubadilisha mfumo huo wa kufikiri inakuwa ndio kazi kubwa kuliko zote duniani. Naomba unielewe vizuri kazi kubwa haimaanishi haiwezekani, lahasha! Ni kazi ambayo inawezekana kabisa. Kwa hiyo tatizo la jamii yetu lipo kwenye mifumo ya maisha na ya kufikiri tuliyoikuta na mingine tumejijengea wenyewe ambayo inatuzuia kuchukua hatua za kuokoa uchumi wetu wenyewe kwa kutembelea hifadhi za taifa na maeneo mengine yenye vivutio.
Hembu fikiria ndugu Mtanzania mwenzangu idadi kubwa ya watalii wanaokuja kutembelea hifadhi zetu na vivutio vyetu wanatoka nchi za mbali sana na pia wanalipia gharama kubwa sana. Sio kwasababu wana hela sana ndio maana wanakuja kutembelea hifadhi zetu namaeneo yenye vivutio, bali ni utamaduni walivyofundishwa kwa miaka mingi na nchi zao kutembelea maeneo yenye vivutio kwa faida yao na kwa faida ya nchi na jamii nzima. Najua tunaaminishwa kwamba wazungu wana hela ndio maana wnakuja kututembelea hifadhi na maeneo yenye vivutio mbali mbali kwenye nchi yetu na nchi mbali mbali. Hivyo kauli ya kusema kuwa wazungu ndio wana hela ndio maana wanatembelea hifadhi na maeneo ya vivutio ni kauli ambayo inawafanya watu wengi hasa Watanzania kuwa tegemezi kwenye kila kitu mpaka kutembelea hifadhi zetu tunahitaji wafadhili! Ohh, Tanzania hapana, tutoke kwenye huu ujinga wa kufikiri hivyo. Badala yake tunatakiwa kujenga misingi mizuri kwa watu wetu wawe na utamaduni mzuri wa kutembelea hifadhi na vivutio mbali mbali, tunatakiwa kuonyesha namna ya kuwa na utaratibu wa kutembelea hifadhi zetu. Tutengeneze mfumo rahisi ili watu wahamasike kuja kutembelea hifadhi zetu.
Kwa hiyo basi, tatizo la msingi kwa Watanzania kutokuwa na utamaduni wa kutembelea hifadhi sio fedha, wala usiniambie kabisa kwamba Watanzania hawana fedha ndio maana hawatembelei hifadhi na maeneo yenye vivutio, kwa hilo nitakukatalia kwa mifano hai kabisa. Tatizo la msingi ni mfumo wa jamii zetu ulivyotulea na jinsi unavyoendekeza tabia mbaya za utegemezi kwenye mambo ambayo tunaweza kuyafanya wenyewe. Fikiria Watanzania sasa tupo zaidi ya milioni 50, tuseme kati ya hao milioni 10 wanaenda hifadhini na kutembelea maeneo yaliyohifadhiwa kila mwaka, tutakuwa na fedha kiasi gani hapo, huoni jinsi tunavyoweza kuchangia fedha kupitia utalii wa ndani?
Takwimu zinzonyesha kwa mwaka Tanzania inapokea wageni/watalii milioni moja tu, kutoka sehemu mbali mmbali duniani kwa ajili ya kuja kutembelea maeneo yenye vivutio mbali mbali ndani ya nchi yetu. Sasa fikiria hao milioni moja wasije, hali inakuaje kwenye sekta hii ambayo imejengwa kwa kutegemea wageni kutoka nje ambao naona wanakuja kama wafadhili. Sikatai wala sipingi juhudi hizi zinazofanywa na serikali na mashirka mengine ya kibiashara kwenye hii sekta, bado kufanya hivyo ni jambo jema sana. Lakini kwanini nguvu nyingi ipo huko? Kwa nini tusipambane na hawa Watanzania mpaka wakatuelewa? Tunahangaika sana, na kuingia kwenye ushindani ambao wakati mwingine unatushinda. Sisi tukomae na watu wetu hawa wanapesa kabisa zaidi ya hizo tunazotegemea kutoka kwa watu ambao hawatabiriki.
Nona vivu jamani, napenda kuona Watanzania wakiona fahari juu ya vitu vyao, maliasili yao, napenda kuona Watanzania wakitembelea hifadhi na maeneo ya vivutio, napenda kuona jambo hili likitokea katika nchi yangu, utamaduni wa kutembelea hifadhi za wanyama na maeneo mengine yenye vivutio sio tu yatachangia kwenye kukuza mapato ya ndani kwa nchi yetu, bali itajenga misingi ya wema na uzalendo ulipotea kwa wengi, utajenga Imani na kushiriki kikamilifu kwenye maswala yote ya uhifadhi wa wanyamapori na utunzaji wa mazingira kwa watanzania wengi. Napenda kuona wakiwa na uwezo wa kusimamia na kutoa maamuzi yenye msaada kwa maliasili zetu. Nakupenda Tanzania.
Ahsante sana kwa kusoma makala hii, iliyoandikwa na kuandaliwa na
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
0742092569/0683248681