Habari wahifadhi na wasomaji wote wa mtandao huu, namini unajifunza mambo mengi kwa kadri unavyoendelea  kusoma makala hizi kwenye blog yako ya wildlife Tanzania. Kila kukicha mambo mengi yanaoyendelea kutokea sehemu mbali mbali yanatupa kuona na kujua sababu mbali mbali ya kutokea kwa mambo hayo, inaweza kuwa ni matokeo mazuri yanayosababishwa na juhudi na weledi katika kazi, au ni matokeo mabaya ambayo hayakukusudiwa yanayosababishwa na uvivu, uzembe, kukosa umakini au kutojali, kila kinachotokea katika sekta yoyote ile kina sehemu kimeanzia.  Kwa kuwepo kwangu kwenye sekta hii ya wanyamapori kumenifanya nijifunze vitu vingi sana na pia kumenifanya nione udhaifu ambao unaweza kuzuilika endapo hatua stahiki zitachukuliwa katika sekta nyeti.

Sekta hii ya wanyamapori ni moja ya sekta kubwa sana katika nchi yetu, na hii ni kutokana na mchango wa sekta hii kwenye pato la taifa na maendeleo ya jamii. Uwepo wa sekta hii kwenye nchi yetu ni jambo kubwa sana la kumshukuru Mungu, lakini pia ni jukumu letu kama nchi na jamii kwa ujumla kuhakikisha sekta hii ya wanyamapori inaendelea kuwepo vizazi na vizazi kwa kuwa makini na watu tunao wapa dhamana ya usimamizi wa sekta hii nyeti.

Baada ya kuona mambo yanavyonda kwenye sekta hii ndipo nikaamua kuandika barua hii ya wazi kwa wafanyakazi na wataalamu kwenye sekta hii ya wanayamapori nimeona hitilafu ambayo isipochukuliwa kwa haraka inaweza kuleta shida kwenye maendeleo ya maliasili zetu. Najua serikali inaajiri maafisa wengi wenye sifa kwenye  sekta hii, pia hata TANAPA wanafanya hivyo, kwa kupata maaskari na wahifadhi wenye sifa na weledi kwenye kazi hii. Mimi shida niliyoiona ipo kwa baadhi ya maaskari wa wanyamapori, kuna baadhi ya askari wa wanyamapori wana moyo wa kweli wa kuwahifdhi wanyama, yani amedhamiria kutoka ndani ya moyo wake atalinda wanyama na atahakikisha kuendelea kwa uhai wa wanyama hawa, atatumia mbinu na ujuzi wake kuhakikisha analinda maliasili hizi. Askari hatakiwi kuwaza kuua tu pale mnyama anapoleta fujo vijijini, au anaposababisha hasara kwa jamii, anatakiwa kuwa na mbinu za ziada kuhakikisaha mnyama hauliwi na anafukuzwa kwenda sehemu yake husika.

Pia askari wanatakiwa wapewe elimu ya kutosha kuhusu wanyama hawa, wanatakiwa wawaelewe vizuri, mfano unataka kumuua simba jike mwenye watoto wadogo, au tembo au wanyama wengine wanaosababisha migogoro kwa jamii. Elimu kuhusu umri na mnyama mzima kwa ujumla ni muhimu sana kwa askari wetu hawa . Wasifanye haraka kwenye maamuzi ya kuua, bali wanatakiwa kuangalia kila njia, kila uwezekano, kila fursa, kila upenyo, kila nafasi, kila linalowezekana, kila mazingira, kila wazo, kila uwezekano wa kuhakikisha wanaokoa maisha ya wanyamapori, na hapo ndipo penye ushujaa na ukomavu wa mafunzo ya kiaskari, kiakili na kwa nguvu pia, anatakiwa afanyie kazi kiapo chake cha kulinda na kuhifadhi wanyamapori popote anapokwenda. Kama rafiki yangu Laurence Okode anavyopenda kusema tukiwa tunaongelea masuala ya uhifadhi, huwa anapenda kusema “ Uhifadhi lazima uwe kwenye damu yako”.

Sambamba na hilo kazi yoyote ya uhifadhi kamwe huwezi kuifanya mwenyewe, ndio maana serikali inaruhusu wadau wengine wenye nia ya dhati kuja kuwekeza kwenye uhifadhi wa wanyamapori. Kuna wanaofanya kazi hii vizuri sana na kwa weledi na kwa kuzingatia sharia zote za nchi na pia sheria za wanyamapori. Mimi ombi langu kuu ni hili, baada ya serkili na mamlaka zinazohusika kwenye sekta hii kutoa vibali kwa mashirika na watu binafsi kuja kushirikiana nasi kwenye suala hili la uhifadhi wa wanyampori, isikae kimnya na kuona kuwa ndio imemaliza kazi, badala yake inatakiwa kuwa na mfumo mzuri kabisa wa ukaguzi wa kazi zinazofanywa na mashirka haya, ili kwenye pongezi watoe pongezi na kwenye kurekebisha parekebishwe. Hivyo basi kwa kuzingatia utalaamu na weledi kwenye sekta hii naomba hili liwefanyiwe kazi. Na pia si suala tu la kufanya ukaguzi wa kazi bali hata wanaosimamia miradi au mashirika haya wawe kweli ni wahifadhi, watu wanaojua wanachokifanya, yani wawe wenye taaluma hii ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori au taaluma nyingine inayoendana na kazi hii ya uhifadhi.

Sisi ndio tunawajibu wa kusimamia afya ya mazingira, wanyama na maliasili zetu, afya ya mazingira ikiharibika hakuna atakayekuwa salama, hivyo basi kwa kutambua hilo tunatakiwa kuzingatia weledi na utaalamu wetu kwenye kazi ya uhifadhi wa wanyamapori na rasilimali nyinginne. Tunatakiwa kujenge misingi mizuri ya uzalendo kwenye rasilimali zetu, ili hata watoto, wajukuu na vitukuu vyetu wajue jinsi tulivyopigania na kusimama imara kwenye kuuhakikisha wanyamapori na maliasili zote zinaendelea kuwepo na kunufaisha vizazi vingi vijavyo.

Kwa dhamira safi kabisa napenda niipongeze serikali kwa juhudi inazoweka kwenye sekta hii, niwashukuru shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), niwashukuru sana mamlaka ya uhifadhi wa wanyamapori Tanzania (TAWA), niwashukuru na mashirkia mbalimbali yenye dhamira safi ya kuhakikisha yanashirikiana na serikali yetu kwenye uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori, mchango wao ni wa thamani sana na ni wa muhimu sana kwenye maendeleo na uwepo wa maliasili zetu, yapo mashirika mengi sana, zipo juhudi kubwa za makundi mbali mbali na pia hata watu binafsi wamejitoa kwa dhati kwenye suala hili la kuhakikisha maliasili hii adhimu ineaendelea kuwepo kwa  vizazi vingi vijavyo.

Asante sana kwa kusoma  barua hii.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

0742092569/0683862481

hillarymrosso@rocketmail.com