Maendeleo ya binadamu na ukuaji wa teknologia ya viwanda na mawasiliano imejenga sura mpya kabisa kwenye ulimwengu wa sasa, na kusababisha mabadiliko yasiyokwepeka kwa maisha ya watu wengi duniani. Ukweli wa mambo ni kwamba mwelekeo wa dunia kwenye mfumo mpya wa maisha unakwenda kwa kasi sana na hivyo kusababisha watu kuchukua hatua ambazo zinzwafanya waendane na kasi ya dunia kwenye hali hii ya mabadiliko ya kiteknologia. Hali hii imesababisha vitu vingi kufanyika kwa ufanisi na kwa haraka, Katiak enzi hizi wanaita ni enzi au zama za taarifa. Ambapo kila mtu anaweza kupata na kujua kinachojiri ulimwenguni. Kasi ambayo imesababisha uchukuliwaji wa maamuzi yasiyo zingatia uwepo na kuendelea kwa asili ya vitu, hasa mazingira yetu.
Ni ukweli usiopingika kwamba mabadiliko ya kimfumo na ya kiteknologia yameacha watu wengi wakiwa hawajui washike lipi, mambo ambayo yalichukuliwa kwa umakini na kwa tahadhari sasa umakini umepungua sana hasa kwenye suala la kuyafanya mazingira yawe rafiki na yabaki kwenye uhalisia wake. Hivyo basi hali ya mazingira yetu yamebakia kuwa sio salama tena kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu, ongezeko la watu na kupungua kwa umakini wa vipaumbele kwenye njia nzuri na salama za uzalishaji. Mambo yanayochangia uharibifu wa mazingira ni mengi sana ambayo kati ya hayo mengi, pia mengi yanaweza kuzuilika endapo tutarudi kwenye misingi.
Kutokana na ushindani na mifumo ya ukuaji wa uchumi kwenye nchi mbali mbali, imekuwa ndio nguvu inayovuta kila upande na kuchangia kuharibika kwa mazingira halisi ya nchi zetu. Watu wanatafuta vipato vya ziada kwa njia nyingi ambazo nyingi sio njia rafiki kwenye mazingira yetu. Kukosa umakini na usimamizi imara unaomtaka kila mtu awe mlinzi wa mazingira yanayomzunguka, kunakuwa na hali ya kukosa uzalendo, rushwa, ulafi, na tamaa ya kupata mali au utajiri wa haraka kwa kuharibu sehemu muhimu zenye mchango mkubwa kwa utunzaji wa mazingira. Mfano ukulima wa holela kwenye vyanzo vya maji, ukataji miti kwa ajili ya matumizi mbali mbali, ongezeko la watumiaji wa nishati ya mkaa, upanuzi wa miundombinu, makazi na shughuli nyngine za kibinadamu zenye athari kubwa kwa usalama wa mazingira.
Mitazamo ya watu wengi kwenye hili la kutunza na kulinda mazingira imekuwa ninwajibu wa watu maalumu tu walioteuliwa au kikundi cha watu maalumu tu. Hii sio sawa hata kidogo, kila mmoja wetu anatakiwa kusimama kidete kwenye ulinzi na utunzaji wa mazingira yetu, popote pale tulipo iwe ni wajibu wetu kuhakikisha mazingira ya eneo tulilopo yapo salama kabisa. Toa elimu kwa ambao wanaharibu mazingira kwa kutupa taka hovyo, kuchoma mioto hovyo, kukata miti bila sababu za msingi, au kuharibu vyanzo muhimu vya maji.
Kwenye Maisha kuna vitu ambavyo kwa asili hatuwezi kuvitenganisha ambavyo ni binadamu na mazingira yake ya halisi. Kuendelea kuwa na uhalisia wa kitu kimojawapo kati ya mazingira na binadamu, lazima vyote viewe au vibaki na uhalisia, kwa mfano binadamu anapoacha uhalisia wake, mazingira nayo kwa kiasi kikubwa hayawezi tena kubaki na uhalisia wake. Hivyo mazingira halisi yalindwe na vitu halisi. Dunia inatumia pesa nyingi sana na gharama kubwa sana kwa mambo ambayo kwaasilimia kubwa tumeyasababisha wenyewe. Tunatafuta hela kwa kuharibu mazingira, na tunatumia tena hela nyingi zaidi kuyatunza na kuyahifadhi mazingira. Tujiongeze sana kwenye hili.
Tunaweza kuandika mambo mengi sana kuhusu mazingira na uunzaji wake, magojwa yanayoibuka kila kukicha ni kutokana na kuharibika kwa mazngira yetu, hali ya ukame tuliyo nayo tumeisababisha wenyewe kwa kutokuwajibika kwe utunzaji wa mazingira yetu. Nchi kama za kwetu huku Afrika zinakabiliwa sana kuharibika kwa mazingira, kuongezeka kwa hali ya ukame haya yote yanasababishwa na kuharibika kwa mazingira.
Tuamke sasa tupambane na kuweka kila kitu kwenye misngi yake imara ili kuwe na mazingira mazuri kwa afya yetu wenyewe na pia afya za wanyama wengine wakufugwa na wasiofugwa. Kila mtu awajibike kwenye hili, kila mtu mwenye eneo ambalo anaishi lazima ayatunze mazingra kwa kuyafanya kuwa safi wakati wote, jamii ziwe na utamaduni wa kupanda miti, mara kwa mara.
Asante kwa kusoma makala hii, endelea kufuatilia makala nyingine zijazo wa kupata maarifa na ufahamu zaidi
Hillary Mrosso
0742092569