Kila mwaka tarehe 31 Julai, dunia inasherekea siku ya askari wa wanyamapori. Askari wa wanyamapori au kama wanavyoitwa kwa kingereza Rangers, ni watu muhimu sana katika sekta ya maliasili. Watu hawa ni askari waliopewa mafunzo na mbinu mbali mbali za kijeshi na kiaskari ili waweze kulinda na kusimamia maliasili zetu.
Huwa nawaza sana, hivi ingekuwaje kama tungekuwa hatuna watu hawa muhimu katika hifadhi na misitu yetu? Bila shaka hali ingekuwa mbaya sana kwenye maliasili na rasilimali za nchi zetu. Kila nchi duniani zenye rasilimali mbali mbali kama vile wanyamapori na misitu zimeweka watu ambao kazi yao kubwa ni kusimamia na kulinda maliasili za nchi dhidi ya vitendo vyote vya kihalifu vinavyoweza kufanywa na majangili.
Nimeandika barua hii makusudi kabisa kwanza kwa ajili ya kuwapongeza kwa kazi yao kubwa wanayoifanya, pili kwa ajili ya kutoa rai kwa watanzania na watu wote duniani kushirikiana na askari wa wanyamapori katika ulinzi wa wanyamapori na maliasili nyingine zilizopo hifadhini na kwenye misitu yetu.
Katika kipindi hiki dunia imeshuhudia hatari kubwa sana inayowakabili wanyamapori, hatari hii ni ujangili uliopitiliza kuliko wakati wowote katika historia ya uhifadhi wa wanyamapori duniani. Na wanyamapori wanaoongoza kwa kuuwawa ni tembo na faru. Na hii ni kutokana na mahitaji ya meno ya tembo na pembe za faru kuwa makubwa katika masoko ya nchi nyingi za Ulaya na Asia.
Licha ya kuwepo kwa mikataba na sheria kali za ndani ya nchi na sheria za kimataifa, bado uhalifu dhidi ya wanyamapori umeongezeka kila pembe ya dunia. Wanyamapori siku hizi wamekuwa na matumizi mengi sana ambayo ni kinyumme na asili kabisa, nchi za Asia kama vile China hudai kuwa huhitaji viungo mbali mbali vya wanyamapori kwa ajili ya matumizi ya dawa za asili.
Matumizi ya wanyamapori hasa ya tembo na faru ndio huongoza katika nchi mbali mbali, tafiti zinaonyesha kwa kiasi kikubwa meno ya tembe na pembe za faru hutumika kama mapambo na kutengeneza visanamu kwenye nchi tajiri kama China, Taiwani, Vietnam, Japani na baadhi ya nchi za Ulaya.
Hali hii ndio inayoleta matishio makubwa sana kwenye uhifadhi wa wanyamapori. Tafiti nyingi za biashara haramu za wanyamapori zinaonyesha kiasi kikubwa cha meno ya tembo na nyara nyingine za wanyamapori hutoka katika bara la Afrika. Hivyo kwa kiasi kikubwa wanyamapori katika bara la Afrika wapo katika hatari kubwa sana. Tafiti zinaonyesha tena kuwa kati ya wanyamapori waliopungua sana kutokana na ujangili kwa miaka ya hivi karibuni ni tembo. Tembo wanaendelea kupungua kila kukicha; kuna tafiti zinaonyesha kila siku wanakufa tembo 55, jambo ambalo linatupa hofu kwa maliasili zetu na wanyamapori hawa muhimu kama wanaweza kufikia vizazi vingi vijavyo.
Katika hali hii, wanokua hatarini siku zote sio tu tembo au wanyamapori wengine, bali hata maaskari wa wanyamapori wanakuwa katika hatari kubwa sana kwa sababu ulinzi wa wanyamapori ni kazi ya hatari ambayo askari wetu wanaifanya. Zipo taarifa za kuuwawa kwa askari wa wanyamapori sehemu nyingi duniani, na askari hawa huuwawa na majangili wakiwa katika majukumu yao ya kuwalinda wanyamapori.
Hivyo katika vita hivi dhidi ya ujangili tunatakiwa tuamke na kushirikiana na askari wetu katika uhifadhi wa maliasili zetu. Kama unavyojua ni kazi ya hatari ambayo bila ushirikiano wa kutosha kutoka kwa jamii zetu hatuwezi kufanya makubwa na majangili wataendelea kuzidi na kuleta uharibifu kwenye maliasili zetu muhimu.
Pia kumekuwa na taarifa nyingi kwenye ripoti mbali mbali zikionyesha namna baadhi ya maaskari waovu wanavyoshirikiana na majangili kuua wanyamapori. Maaskari wanapokea rushwa na wanaotoa nafasi kwa majangili kuingia na kuuwa wanyamapori hovyo. Jambo ambalo ni kinyume na sheria pia ni ukosefu wa maadili na uzalendo kwa askari ambaye anajihusiha kwenye vitendo vyovyote vya kijangili.
Najua adha na hatari wanayokutana nayo porini, licha ya kwamba kuna majangili ambao wana silaha kali wanaoweza kuwaua lakini bado pia kuna hatari mbali mbali za wanyama wakali kama vile simba, tembo, nyati na mamba.
Hivyo ningeomba serikali iboreshe vitendea kazi na pia iboreshe maslahi ya askari kwa kuwapa motisha mzuri ili wafanye kazi yao kwa moyo na kwa uzalendo.
Nawapongeza sana maaskari wote wazalendo wanaofanya kazi hii muhimu ya kuwalinda wanyamapori wetu na maliasili zetu muhimu. Kazi yenu ni muhimu sana, sio tu kwasababu inawapa mishahara kwa ajili ya familia zenu, lakini kwa sababu inawapa mamilioni ya familia za vizazi vingi vijavyo nafasi ya kuona uzuri na faida za uwepo wa wanyamapori na mazingira mazuri kwa viumbe hai wote.
Endeleeni kufanya kazi zenu kwa weledi na kujituma; mkijua kabisa bila ninyi hatutakuwa na wanyamapori kwenye mapori yetu, bila ninyi hatutakuwa na misitu kwenye hifadhi zetu. Bila ninyi tutakosa wanyamapori lakini pia mazingira yetu yataharibiwa sana. Simameni imara kwenye kazi zenu siku zote, Mungu aliyeziumba mbingu na nchi, akaumba na wanyama na mimea yupo pamoja nanyi katika kazi hii njema.
Asanteni sana!
Hillary Mrosso
+255 683 862 481
www.mtalaam.net/wildlifetanzania