Hakuna mtu anayeonekana kuwa na hekima kama mtu anayeacha urithi kwa watoto wake, kwenye maeneo mbali mbali ya maandiko matakatifu kama vile Biblia wamesisitiza sana jambo hili, kwenye kitabu cha Mithali ambacho kimeandikwa na mfalme aliyekuwa na hekima kulikowote hapa duniani, na pia aliyekuwa tajiri kuliko wote hapa duniani. Kwenye moja ya mandiko yake kwenye kitabu hicho maarufu ameelezea kuhusu urithi na tabia za watu wanaoacha urithi kwa familia zao, watoto wao na kwenye jamii yao. Katika kitabu hiki cha Mithali 13:22b anasema kwenye msitari huu kuwa “mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi”. Hapa kwenye msitari huu anaposema mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi hapa ana maana kuwa suala la kuacha urithi linatakiwa kufikiriwa kwa vizazi vya miaka mingi ijayo na sio kwa ajili ya watoto wako tu, bali kwa ajili ya watoto wa watoto wako.
Kwenye masuala ya uhifadhi wa maliasili kuna dhana ambayo hupenda kutumika sana kwa ajili ya kuhamasisha matumizi endelevu ya maliasili. Kuna dhana mbali mbali lakini zote zina dhima moja ya uhifadhi endelevu. Kwa mfano kuna misemo ya kingereza kama “Conservation for sustainability au sustainable development”, na nyingine nyingi ambazo zinahamasisha matumizi ya maliasili kwa manufaa ya sasa na baadaye. Uwepo wa rasilimali hizi kwenye mikono yetu unahitaji hekima na busara kutumia kwa kufikiria kuna wenzetu ambao watazihitaji zaidi, kuna watoto na wajukuu zetu ambao wanazihitaji rasilimali hizi kwa ajili ya maisha yao.
Sisi wahifadhi na watanzania wote ni kama wazazi, sisi ni viongozi, maliasili hizi tunazoziona kwenye mazingira yetu zinahiji utunzaji na usimamizi makini ili tuweze kuwaachia vizazi vijavyo urithi wa rasilimali hizi. Hivyo basi kutokana na hali hiyo tunatakiwa kuishi kwa hekima na busara hasa katika kufanyama maamuzi ya matumizi ya rasilimali tulizonazo. Tukae tukitambua ya kwamba uwepo wa rasilimali hizi sio kwa ajili ya kutunufaisha sisi pekee, bali ni kwa ajili ya kunufaisha vizazi vingi ambavyo bado havijazaliwa. Pia tunapoacha urithi tunaonekana kuwa wema, maana anasema mtu mwema ndio huacha urithi, tufanya yote kwa wema na kuacha urithi wa kutosha wa maliasili tulizonazo na tunazozisimamia.
Aidha kwenye jambo kama hili la matumizi ya rasilimali za nchi yetu, kama vile misitu, madini, wanyamapori na maeneo yenye hadhi mbali bali za uhifadhi kama maeneo oevu, mito, mabwawa na milima inatakiwa ituzwe kwa gharama yoyote. Hapa ndipo tunapohitaji hekima, na busara katika kuishi na katika kufanya maamuzi ya kutumia rasilimali hizi. Kwenye nchi za wenzetu nyingi waliamua kutumia rasilimali zao vibaya, walichoma misitu wakaharibu maeneo ya makazi wa wanyama, ndege na maeneo ya hifadhi za wanyamapori sasa hivi wanahaha kutafuta namana ya kurudiha hali hiyo, na inawagharimu sana maana inaweza kuchukua zaidi karne nzima ili kurudisha hali ya mwanzo.
Leo tutafakari wazo hili na tulifanyie kazi, nakutakia kila la kheri,nenda kafanya mambo kwa hekima na busara uache uridhi kwa wajukuu na vizazi vinginge vingi vijavo. Asante sana.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania