Katika kuhakikisha uhifadhi unakuwa endelevu suala la ardhi ni muhimu sana kuangaliwa. Vitu vyote vinatakiwa kuwa kwenye mlinganyo unaoeleweka na wa sawa hasa kwenye matumizi ya ardhi. Makundi yote muhimu yanayohitaji ardhi kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo ni muhimu yakazingatiwa. Makundi haya ni makundi yenye idadi kubwa ya watu na shughuli nyingi za kipato na chakula hupata kupitia ardhi ambayo ndio mkombozi wao. Mfano kuna wakulima, wafugaji na serikali. Ukiangalia wakulima wanahitaji ardhi kubwa nzuri na yenye rutuba, ukiangalia wafugaji nao wanahitaji ardhi kubwa nzuri na yenye malisho kwa mifugo yao, serikali nayo inahitaji ardhi kwa ajili ya uwekezaji, uhifadhi wa wanyamapori na misitu nk.

Tanzania ina eneo kubwa sana la ardhi, na endapo matumizi na mipango bora ya ardhi itafanyika na kueleweka kwa watu vizuri basi maeneo mengi kungekuwa na maendeleo makubwa sana. Kutoeleweka kwa maeneo mengi ya ardhi ya Tanzania kumesababisha matumizi holela ya ardhi, na matumizi holela ya ardhi ndio hupelekea uharibifu wa ardhi hiyo na mazigira kwa ujumla wake.

Ingawa tuna sheria za ardhi za vijiji na sheria za ardhi za jumla, bado kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi kwenye ardhi yetu. Chanzo kukibwa cha migogoro hiyo ni matumizi ya ardhi yasiyofuata utaratibu. Changamoto hii isipotatuliwa mapema itatuletea shida kubwa hapo baadaye kwasbabu watu wanaongezeka, na matumizi ya ardhi yanaongezeka pia, hivyo kuepusha migogoro hii ni muhimu kupitia mara kwa mara utekelezaji wa sheria na mipango ya matumizi bora ya ardhi.

Tanzania ina idadi kubwa ya wakulima na wafugaji, na makundi haya ya watu yanahitaji ardhi kubwa ya uzalishaji. Kwa mfano wafugaji wanahitaji maeneo makubwa na yenye malisho ya uhakika kwa mifugo yao. Hii ndio imepelekea wafugaji wengi kuishi karibu na maeneo ya hifadhi ya wanyamapori na misitu ili kulishia mifugo yao maeneo hayo.

Kutokana na hali hiyo kumekuwa na migogoro kati ya wahifadhi wa wanyamapori na wafugaji. Na endapo mifugo itaingia kwenye maeneo ya wanyamapori adhabu yake ni kubwa na mfugaji ndio atawajibika kulipa adhabu hiyo kwa wakulima nao ni hivyo hivo, kwa wale ambao mashamba yao ya mazao yapo karibu na hifadhi za wanyamapori ni shida kubwa sana kwa wakulima pale ambapo wanyamapori wanapovamia na kula mazao ya wakulima.

Pamoja na hayo yote uharibifu unaosababishwa na wanyamapori kwenye mazao ya wakulima na mifugo ya wafugaji haupewi uzito unaotakiwa. Kwasababu ya fidia ndogo sana wanayopata wahanga wa migogoro hii. Kwa kuwa tunahifadhi wanyamapori kwa manufaa ya jamii nzima, sula la fidia liangaliwe tena kwa lengo la kuongeza kiasi hicho.

Hata hivyo kuna miradi ya serikali na mashirika binafsi yanayojihusisha na masuala ya ardhi. Lengo likiwa ni kutoa elimu muhimu ya ardhi, kuandaa mipango bora ya matumizi ya ardhi, na kuainisha maeneo mbali mbali kwa ajili ya shughuli mbali mbali za matumizi ya ardhi. Kwa mfano shirika la kimataifa la uhifadhi wa wanyamapori, African Wildlife Foundations (AWF) wanajihusisha sana na mpango huu kusini mwa Tanzania.

AWF ambayo inasaidia jamii namna ya matumizi bora ya ardhi ili kuwe na matumizi bora ya ardhi yatakayoepusha uvamizi kwenye maeneo muhimu ya wanyamapori. Hii ni kutokana na kukua kwa kilimo maeno ya kusini mwa Tanzania na watu wanatumia fursa hiyo kulima maeneo makubwa ambayo yanapelekea uharibifu kwa mazingira na maeneo ya wanyamapori.

Suala la ardhi ni la kuangaliwa sana katika nchi yetu, pia wananchi waeleimishwe zaidi kuhusu uhusiano wa maendeleo ya kilimo na uhifadhi wa mazingira ya viumbe hai. Bila kueleweka kwa elimu na umuhimu wa kuhifadhi maeneo ya wanyamapori watu watakosa sababu za kuthamini wanyamapori na maeneo muhimu yaliyohifadhiwa kwa sababu hizo.

Nimalizie makala hii kwa kusema, kila hatua ya ukuaji wa maendeleo kwenye sekta yoyote ile unatakiwa kuendana na uhifadhi wa mazingira na makazi muhimu ya viumbe hai. Maendeleo mazuri ni yale yanayofanyika bila kuathiri maendeleo ya vitu vingine muhimu. Kila miradi ya kiserikali na ya watu binafsi hata kama ni ya kuleta faida kubwa haitakiwi kuwa ni mbadala wa wanyamapori na maeneo yao muhimu ya asili ya kuishi.

Na hapo ndipo inahitajika hekima na busara zaidi, hapo ndipo inahitajika kufanyika maamuzi yasiyo na hisia kwa kuangalia maslahi ya muda mfupi. Uhifadhi endelevu wa wanyamapori na misitu yetu upo mikononi mwetu wenyewe, sisi ndio tunaamua mwisho wa viumbe hai hawa muhimu kwenye mfumo wa maisha ya binadamu. Tukiacha mazingira na viumbe hai hawa ambao hulindwa kwa gharama kubwa vikitoweka, na maisha yetu yanakuwa hatarini pia.

Tuache mazingira asili yabaki kwenye uasili wake; ni kwa faida yetu wenyewe!

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255683 862 481/+255742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaam.net/wildlifetanzania