More

    Changamoto Kubwa Kwa Wakulima Walio Kando Ya Hifadhi

    Habari ndugu msomaji wa makala hizi za kitalaamu zinzohusu masuala yote ya uhifadhi wa wanyamapori. Leo tunaangalia maswali na hali nilizoziona kwa wakulima  wadogo wanaolima karibu na hifadhi au mapori ya vijiji, au karibu na maeneo ya wanyamapori. Nimeamua kuandika makala ya leo ili kuwafanya wadau na serikali hata watalaamu mbali mbali waweze kuwa na uwanja mpana wa kufikiri kwenye swala zima la uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine muhimu kwenye maeneo yetu.

    Ndugu msomaji wa makala hii lengo langu la kuandika haya sio tu kukufanya uone jinsi wakulima wanavyopata shida kuendesha maisha yao la hasha, bali sisi kama watalaamu wa mambo haya tunatakiwa kuwa na uwanja mpana wa kufanya maamuzi kwenye masuala yote ya maliasili bila kuacha vipengele muhimu vinavyochukuliwa bila uzito unaotakiwa na wafanya maamuzi kwenye eneo hili.

    Tunajua dhamira ya dhati ya serikali yetu kwenye uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine kwenye sekta hii nyeti, ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia pato la nchi kupitia utalii, utafiti, na matumizi mengine endelevu kwenye maliasili zetu. Hali ambayo imesababisha kuwepo kwa sheria kali za uhifadhi wa maliasili, mazingira na uongozi wa sekta hii. Hivyo bila kuwa na uwanja mpana wa kuamua mambo haya ili yawe na tija ya moja kwa moja kwenye jamii hasa jamii zilizopo pembezoni mwa hifadhi au karibu na makazi ya wanyamapori bila shaka hatuwezi kufika mbali kwenye harakati hizi.

    Kumekuwa na kilio cha muda murefu kutoka sehemu mbalimbali zinazosababisha migogoro isiyoisha kwa sababu ya uharibifu wa wanyamapori kwenye maeneo ya wakulima na wafugaji wanaoishi karibu na maeneo haya. Pamoja na kwamba watu hawa wamekuwapo katika maeneo haya kwa muda murefu, wengi wao walihamishwa na kufukuzwa ili kupisha upanuzi wa maeneo ya wanyamapori na hifadhi zao. Ijulikane kwamba hata faida zinazotokana na uwepo wa wanyamapori hawa kwenye maeneo yao imekuwa sio ya kuridhisha na wakati mwingine kutokuwepo kabisa. Tafiti nyingi zinaonyesha kwa uwazi kabisa jambo hili katika hifadhi nyingi na mapori tengefu ya nchi yetu. Migogoro isiyoisha na kutokuwepo kwa uhusiano mzuri kati ya uongozi wa hifadhi na wananchi walio karibu na maeneo yao.

    Hivi karibuni rafiki yangu mmoja katika eneo nililokuwa nafanyia utafiti aliniambia yupo shambani kwake analinda wanyama waharibifu wanaovamia na kula mazao yake, hivyo hulazimika kuyalinda mazao yake usiku na mchana dhidi ya uharibifu wa wanyama hawa, ambao ni nyani nguruwe, viboko na tembo. Hivyo wakati wa mchana anahangaika kukaa shambani akiwafukuza nyani, tembo  na ndege, lakini wakati wa usiku huwafukuza nguruwe, viboko na wengine waharibifu. Hali kama hii hupelekea kuendelea kuwepo kwa hali duni na umasikiuni usioisha kwa jamii hizi kwa sababu nguvu kubwa ya uzalishaji ianpungua kutokana na usumbufu wa wanyamapori.

    Ndugu yangu hembu mtafakari mkulima huyu anayelima kwa shida na kwa gharama kubwa, lakini haishii kulima tu na kuyaacha bali inamlazimu kuyalinda hadi mazao yake yakue, haya ni zaidi ya mateso kwa wakulima kwenye maeneo haya. Lakini pamoja na taabu yote na kutumia muda mwingi kwenye uzalishaji finyu kama huu, kuharibiwa mashamba yake na wanyama hawa bado hakuna mpango madhubuti wa uhakika wa kumfidia mkulima huyu mdogo kutokana na kuharibiwa kwa mazao yake na wanyamapori, na hata kama mpango huo upo bado una mapungufu mengi sana.

    Tunatokaje hapa, kama tuantaka kutengeneza uhusiano mzuri na ulio bora kwa mustakabadhi wa maendeleo ya maliasili zetu kuendelea kuwepo kwa miaka mingi ya vizazi vijavyo lazima tuakae chini tupange jinsi ya kwenda pamoja na wenzetu wanaoishi karibu na maeneo haya yenye makazi ya wanyamapori. Tunahitaji kukaachini na kupanga sera na sheria ambazo ni rafiki kwa kila upande kupata faida kutokana na uwepo wa maliasili zilizopo kwenye maeneo yao. Kwa kufanya hivi tutatuliza hasira na watu wataona faida wanayopata hivyo kushiriki kikamilifu kwenye uhifadhi wa maliasili na mazingira kwa ujumla.

    Hapa inabidi tufanye kila linalowezekana kwa kuhakikisha kunakuwepo na faida inayoonekana kwa jamii, pia kuwepo na mpango kabambe wa kutoa fidia kwa wakulima walioharibiwa mashamba yao na wanyamapori.

    “Kamwe hatuwezi kutengeneza uzalendo wa kweli  sehemu yenye ubaguzi, unyonyaji, na sehemu ambayo haki haitendeki”

    Nakushukuru kwa kusoma makala hii iliyoandikwa na

    Hillary Mrosso

    0742092569/0683248681

    hillarymrosso@rocketmail.com

    Latest articles

    Related articles

    1 Comment

    Leave a reply

    Please enter your comment!
    Please enter your name here