Kila mara tunapata na kusikia taarifa nyingi za wanyamapori kugongwa na magari, idadi kubwa ya wanyamapori wanaokufa, kuvunjika na kusababishiwa vilema inaongezeka. Wanyamapori muhimu kama swala, fisi, nyani, twiga, nyati ngiri, nk, wanapoteza maisha yao kwa kugongwa na magari.

Licha ya changamoto nyingi zinazowakabili wanyamapori, kama vile uharibifu wa makazi yao, magonjwa, mabadiliko ya tabia nchi, ujangili, biashara haramu, na ongezeko la kubadili makazi yao asili kuwa mashamba, barabara, viwanda na makazi ya watu; wanyamapori kugongwa na magari limekuwa ni janga kubwa ambalo linachangia idadi yao kupungua.

Pamoja na changamoto hizo, tunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa baadhi ya changamoto ambazo zinapelekea vifo vya wanyamapori vya mara kwa mara. Mfano, tunaweza kupunguza au kuzuia kabisa vifo vya wanyamapori vinavyosababishwa na kugongwa na magari barabarani.

Najua kuna baadhi ya changamoto ambazo ni ngumu kuzizuia kama vile magonjwa, mabadiliko ya tabia nchi. Lakini tunaweza kuzuia ambazo zipo ndani ya uwezo wetu, kama vile ajali za barabarani. Ajali nyingi na vifo vingi vya ajali za barabarani zinazowapata wanyamapori kwa asilimia kubwa ni uzembe, mwendo kasi, kutoheshimu na kufuata sheria za barabarani, hasa maeneo yenye wanyamapori.

Madereva, tunatakiwa kuongeza umakini na kufuata sheria za barabarani, hasa tunapoendesha magari sehemu zenye wanyamapori. Tunatakiwa kufahamu kuwa wanyamapori hawana utashi mkubwa kama sisi binadamu, hivyo wakiwa kwenye maeneo yao tunatakiwa kuwaheshimu na kuchukua tahadhari zote muhimu kuepuka ajali na vifo.

Ajali zinazowapata wanyamapori barabarani, zinaweza kuzuilika na pia zinaweza kuepukika endapo madereva wataongeza umakini wanapoendesha magari sehemu zenye wanyamapori. Kwa bahati nzuri au mbaya, kuna baadhi ya maeneo muhimu ya wanyamapori yamepitiwa na barabara zinazopitisha magari mengi. Mfano, barabara inayokatisha hifadhi ya taifa ya Mikumi, Katavi, Serengeti, nk.

Pia kuna barabara zinapita kwenye maeneo muhimu ya mapito ya wanyamapori kama vile shoroba. Shoroba ni maeneo ya mapitio ya wanyamapori kutoka hifadhi moja kwenda hifadhi nyingine. Mfano, ushoroba unaounganisha hifadhi ya taifa ya ziwa Manyara na Tarangire, kuna ushoroba unaunganisha hifadhi ya taifa ya Nyerere na hifadhi ya milima ya Udzungwa. Soma zaidi hapa

Maeneo hayo yanapitiwa na wanyamapori mara kwa mara, lakini pia yanapitiwa na magari mengi kutokana na uwepo wa barabara kubwa, hivyo tunatakiwa kuongeza umakini tunapoendesha magari maeneo hayo. Tunatakiwa kupunguza mwendo kwenye maeneo yenye wanyamapori, na endapo tutaona wanyamapori wanakatisha barabara hatuna budi kusimama kabisa ili kuzuia ajali.

Baadhi ya wanyamapori wakiona magari hawawezi kuvuka haraka, watabakia wanashangaa tu, mwishowe hugongwa na kufa au kupata vilema. Nyakati za usiku ndio tunatakiwa kuongeza umakini zaidi maana wanyama wengi huwa ndio wanajitafutia chakula wakati huo, hivyo tunapopita maeneo yenye wanyamapori wakati wa usiku tunatakiwa kupunguza mwendo kwenye magari yetu na kuendesha kwa tahadhari.

Tunaweza kutokomeza kabisa vifo vya wanyamapori vinavyotokana na ajali za barabarani kwa kuongeza umakini na kufuata sheria za barabarani. Vifo vingi vya wanyamapori vinatokana na madereva kuwa kwenye mwendo kasi, kaisi cha kushindwa kupunguza pale mnyama anapotokea mbele yao.

Licha ya serikali kuweka sheria na faini kubwa kwa wataogonga wanyamapori, bado kuna matukio mengi yanatokea ya wanyamapori kufa kwa ajali. Mfano, tarehe 19 Octoba, 2024, twiga alikutwa amegongwa katika barabara ya Makuyuni Mbuyuni. Twiga ni wanyama wapole na wasio na ukorofi, inashangaza sana kuona watu wanafikia hatua ya kugonga twiga hadi anavunjika miguu yake na kufa kabisa.

Twiga aliyekutwa amegongwa katika barabara ya Makuyuni

Tuwajibike kuwalinda wanyamapori wetu, tuepuke makosa ya wazi hasa ya kuendesha kwa mwendo kasi maeneo yenye wanyamapori.

Asante kwa kusoma makala hii, naamini utafuta na kuzingatia usalama wa wanyamapori wakati wa kuendesha magari.

Imeandikwa na Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com