Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu kwenye makala yetu ya leo tunajifunza kwa pamoja kuhusu matumizi endelevu. Matumizi endelevu ni dhana ambayo umewahi kuisikia sehemu mbali mbali popote pale ulipo, naamini kwa kiasi kikubwa umewahi kusikia matumizi endelevu ya misitu, matumizi endelevu ya wanyamapori, matumizi endelevu ya vyanzo ya nishati au maji, gesi, madini nk. Matumizi endelevu ni maneno muhimu sana kwenye tasnia ya uhifadhi wa maliasili hasa wanyamapori na misitu. Unaweza kujiuliza maswali matumizi endelevu maana yake ni nini? Au mtu ana maanisha nini anaposema matumizi endelevu?
Matumizi endelevu kwa maana ya jumla ni kutumia kile ulicho nacho sasa kwa namna ambayo utanufaika sasa na baadaye. Au ni kutumia rasilimali ulizo nazo kwa manufaa ya sasa na ya baadaye. Ninapozungumzia rasilimali hapa namaanisha vitu vingi kama vile ardhi, misitu, wanyama, ndege, maji madini, gesi nk. Hivyo ni baadhi tu ya rasilimali zinanazoweza kupatikana karibu kila nchi hapa duniani. Uwepo wa rasilimali hizi ni muhimu sana kwa nchi yoyote ile kiuchumi na kimaendeleo, hivyo uwepo wa rasilimali kwenye nchi yoyote unadai sio tu kujua namna ya kuzitumia na kufaidi rasilimali hizo bali unadai kitu kingine muhimu zaidai uhifadhi na namna ya kutumia ili ziweze kunufaisha vizazi vingi vijavyo.
Kila nchi inatofautiana na nchi nyingine kwa uwingi wa rasilimali ulio nao, nikimaanisha kuna nchi zenye rasilimali nyingi kuliko nchi nyingine, kuna zenye rasilimali chache kuliko nchi nyingine. Kutokana na kuwepo kwa rasilimali au maliasili hizi kwenye ardhi za nchi mbali mbali, nchi nyingi sana zimeamua kutunga sera na sheria zitakazosimamia matumizi endelevu ya maliasili zao. Hii ni kutokana na umuhimu wanaouona kwenye rasilimali hizo na pia ni kutokana na mchango mkubwa unaoletwa na rasilimali hizi kwenye nchi husika, na jinsi ambavyo rasilimali hizo zinaboresha na kuinua maisha ya wananchi. Kwa kutambua hilo matumizi hayatakiwi kufikiriwa kwa wale waliopo sasa tu, bali hata kwa wale watakao kuwepo baadaye.
Sio kwamba tuna rasilimali nyingi ndio maana tunazitumia na kuwabakizia wengine, hapana! Sio kwamba rasilimali tunazoziacha kwa ajili ya kizazi kijacho sisi hatuzihitaji au hazitufai sisi, sio kwamba rasilimali tunazozitunza ziendelee kuwepo kwa miaka mingi tunazipenda sana, hapana! Sio kwamba rasilimali tunazotaka ziendelee kuwepo kwa miaka mingi ijayo tuanataka ziwepo kwa ajili ya urembo au njia ya kujipatia sifa kwa nchi nyingine kwamba tuna rasilimali nyingi, tunahifadhi rasilimali zetu sio kwa sababu ya kuwa kivutio kwa wengine, wala hatuziachi rasilimali na maliasili tulizonazo kwa vizazi vingi vijavyo kwa sababu za kiuchumi na kitamaduni pekee; tuna sababu nyingine yenye nguvu na ndio msingi wa uhifadhi wa maliasili zetu kama vile wanyamapori na misitu.
Sababu kuu wakati wote na siku zote inayotakiwa kutusukuma katika uhifadhi wa wanyamapori na misitu inatakiwa kuwa ni kuhifadhi wanyamapori na maliasili nyingine ili maisha yaendelee kuwepo hapa duniani kwa miaka mingi ijayo. Kwasababu ya mifumo ya maisha ya mwanadamu ilivyotengenezwa ni kwamba anatakiwa kuishi kwenye mazingira mazuri yanayoendana na jinsi alivyoumbwa, ndio maana huwezi kukuta watu wanaishi kwenye maji kwa muda mrefu, au kwenye majangwa, au kwenye barafu. Hii yote ni kwasababu mwanadamu ameumbwa aweze kuishi kwenye mazingira yanayoendana na uumbaji wake.
Hivyo basi uhifadhi endelevu sio tu kwa faida za kiuchumi kwa vizazi vijavyo bali kwa maisha yao yaweze kuwepo; hivyo njia nzuri ya kufanya hivyo ni kuwatengenezea mazingira kwa kuhifadhi na kutumia maliasili tulizonazo sasa kwa hekima na busara ili maisha ya watoto, wajukuu na vitukuu vyetu yawe yenye afaya bora na mazingira yao yachangie kuboreha maisha yao na sio kuharibu. Siku zote mtu anayebakiza mali yake au anayewarithisha watoto wake au wajukuu wake mali maandiko matakatifu yanasema mtu huyo amebarikiwa na ataendelea kubarikiwa, na pia ni mtu mwenye hekima na busara nyingi. Hivyo ndivyo ilivyo hata kwa nchi inatakiwa kutumia na kuacha urithi wa kutosha kwa vizazi vingi vijavyo. Na nchi ambayo ina mipango mizuri ya uhifadhi wa maliasili nchi hiyo itabarikiwa sana, na itaonekana ni nchi yenye hekima. Na inaongozwa na watu wenye hekima na watu wake watakuwa na hekima.
Fikiria kama wezee wetu wa kale wasingetambua jambo hili la uhifadhi endelevu, ina maana kwa kiasi kikubwa tusingekuwa na wanyama na maliasili nyingi tunazoziona leo, walihifadhi sio kwasababu walikuwa hawapendi kula nyamapori au hawakuwa na matatizo ya kiuchumi, walijua misingi na wakaiheshimu, walijua ili vizazi vijavyo viwe na maisha bora wanahitaji mazingira bora ya asili, na walifanya hivyo kwa kuhifadhi maeneo mengi ya wanyamapori na misitu.
Hivyo basi Tanzania kama nchi yenye maliasili nyingi tuna wajibu mkubwa sana wa kuhakikisha malisili hizi tulizo nazo haziishiii kwenye kizazi chetu pekee bali kunufaisha maelfu na mabilioni ya maisha ya viumbe hai wa baadaye. Hekima na busara ndio vinatakiwa kutuongoza kwenye jambo hili ili tusimamie kweli matumizi endelevu kwa wananchi wote. Hivyo serikali inatakiwa kuja na njia nzuri na zenye tija kwenye uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine.
Kwa kufikia hapa naamini umejifunza dhana hii ya uhifadhi endelevu, matumizi endelevu ya maliasili zetu. Unaweza kuwashirikisha wengne maarifa haya muhimu ili na yenye ajifunze na kupiga hatua.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania