Mpendwa msomaji wa Makala mbalimbali za wanyapori, utalii na mazingira , awali ya yote namshukuru mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na kutuwezasha kuandaa Makala hii. Napenda kukaribisha katika makala ambayo inaelezea namna ambavyo mnyama aina ya Tembo anaweza kuwasiliana ikiwa ni pamoja na kutoa ishara mbalimbali. Pamoja na hilo, natoa shukrani kwa kuwa msomaji mzuri wa makala ambazo zinaandaliwa kupitia mtandao huu
Utangulizi
Tembo ni miongoni mwa wanyama wanaovutia na kupendwa na watu wengi duniani huku muda mwingine amekuwa akiitwa binadamu wa pili kutokana na matendo yake ambayo hufananishwa na binadamu kama vile kuwa na hisia za huzuni, furaha pamoja na uwezo mkubwa wa akili. Mpendwa msomaji, tembo anayo mengi maajabu ila kwa leo kupitia makala hii nipende kukukumbusha haya machache;
- Ni myama mkubwa kuliko wanyama wote waliopo nchini kavu.
- Ni myama anayebebeba mimba kwa muda mrefu zaidi (miezi 22) na humyonyesha mototo wake kwa takribani miaka mitano.
- Ni mnyama mwenye uwezo wa kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu sana, na ana uwezo mkubwa wa akili.
- Ni mnyama anaye hatarishwa na shughuli za binadamu hususani ujangili na shughuli kama kilimo ambazo huchangia uwepo wa migigoro kati ya tembo na binadamu.
Njia za mawasiliano katika Tembo
Ulishawahi kujiuliza ni namna gani tembo wanawasiliana, ikizingatiwa tembo huishi katika familia kubwa ambayo inaongozwa na jike mkubwa kwa umri yaani bibi. Tofouti na wanyama wengine ambao tumekuwa kukisikia milio yao ama sauti zao ambazo hutumika kwa mawasiliano kwa tembo imekuwa nadra sana kusikia sauti hizo. Swali ni je inaama Tembo hawawasiliani? Jibu ni hapana
Kama ilivyo kwa nanyama wengine tembo huitaji mawasiliano hususani kwa ajili ya kuhakikisha usalama katika familia zao, kutoa tahadhari hasa pale wanapokumbana ama kuhisi Hali ya hatari, kuongoza wanafamilia, kuomba msaada ama mahitaji na pia mawasiliano kati ya tembo dume na jike ili kuwezesha shughuli za uzazi.
Mawasiliano ya sauti
Watafiti wa tembo wameeleza kuwa tembo hutumia zaidia ya aina 70 za sautiambazo husafiri katika uelekeo tofauti (omnidirectional) na hivyo kuweza kuwafikia tembo wengi kwa wakati mmoja ikiwemo waliokusdiwa na ambao hawakukusudiwa. Mara nyingi sauti hizi huwa ni za muda mfupi sana hivo ni mahususi kwa ajili ya kutoa taarifa za haraka na ambazo sio za kawaida katika mazingira yao kama vile kutoa tadhari wakati wa hatari. Wanasayansi wamebaini kuwa tembo hutoa sauti za chini ambazo husafiri kwa umbali mrefu sana. Mwanasayansi B. Christy katika chhapisho lake lijulikano kama “What Elephant Calls mean, 2014” ameonyesha kuwa sauti au milio ya tembo ambao hutofautiana kuanzia za chini ambazo hata binadamu hawezi kuzisikia hadi zile tunazoweza kuzisikia huwa na ujumbe tofauti, na sauti hutolewa kwa kukoroma (snorts), kubweka (barks), miguno (grunts) na sauti mithili ya tarumbeta
Mawasiliano ya ishara
Licha ya kuwa tembo ni mnyama mwenye uoni hafifu, bado hutumia ishara katika mawasilaiano. Hutumia viungo mbalimbali ikiwemo kichwa, mkonge, pembe na mkia kutoa ishara. Mifano ya ishara zitumiwazo na tembo katika mawasiliano ni pamoja na tembo kusimamisha masikio na kuyaupigapiga kwa kasi (rapid ears flapping), kukodoa macho huku akiuchezesha mkia wake upande kushoto na kulia mithili ya mkia wa mbwa ikiwa ni ishara ya furaha au hali ya amani. Wakati wa hofu, huzuni ama hasira mwili, masikio na macho hupanuka nahuusimamisha mkia wake katika nyuzi 90⁰. Ni vyema zaidi kuchukua tadhari dhidi ya Tembo kwani anaweza kufanya mashambulizi na kumdhuru mtu aliye karibu naye kwa wakati huu.
Picha 1; Tembo mwenye hasira, chanzo Magazine

Picha 2; Tembo mwenye Amani: Chanzo; Zambia daily Mail. Articles/WWF
Mawasiliano kwa njia ya harufi
Njia hii huwa ni mahususi kwa Tembo wanata ambae ni Tembo jike aliye tayari kumpokea dume (receptive female) . Hii hufanyika kwa kuzalisha kemikali (sex pheromones) ambazo hutolewa kupitia mkojo wa Tembo jike. Tembo dume huweza kunusa harufu ya kemikali hizo, na huchukua mkojo wa jike na kuuweka mdomoni kwa kutumia mkonge na kuulamba mkojo huo. Kitendo hicho kitaalamu kinaitwa flehemen. Hivyo, kwa namna hii Tembo jike hutoa taarifa kwa dume kuashiria utayari wa kumpokea dume, na kwa kunusa Tembo dume humtambua jike mwenye utayari.

Picha 3; Tembo dume akinusa mkojo wa jike( Chanzo; ResearchGate).
Mawasilaino kwa njia ya kugusana
Tembo hutumia mguso kama njia mojawapo ya mawasiliano kwa kugusana kwa makusudi kwa kutumia mkonge, mkia, masikio na sehemu nyingine za mwili. Njia hii hutumika katika mukutadha mbalimbali ikiwemo; kucheza, hasira, kuhudumiana, kujilinda na hata katika mahusiano kati ya jike na dume. Tembo hutumia mkonge kuashiria salamu au umoja miongoni mwa wanafamilia. Pia Tembo husuguana masikio kuashiria kucheza au miongoni mwa jike na dume wenye mahusiano. Pia Tembo akiwa na mimba Tembo wengine hutumia mkia kugusa tumbo kama ishara ya kumjulia hali.
Picha 4; Tembo wakisalimiana na kuwasiliana kwa njia ya kugusana Chanzo; elephantsvoices.org
Mawasiliano ya Tembo kuashiria hali ya hatari
Matukio kadha wa kadha ya binadamu kuuwawa na Tembo husikika katika mabara ya Africa na Asia ambapo Tembo hupatikana. Ikumbuke Tembo si mnyama ambaye anapenda kumdhuru ama kumshambulia binadamu. Tembo kabla hajamshambulia au kumdhuru binadamu huonesha dalili za kutofurahishwa na hali hii, kama ukizielewa dalili hizi mapema ni rahisi kujiokoa dhidi ya mashambulizi haya. Yafuatayyo ni mambo yanayofanywa na Tembo kuashiria hali ya hatari;
- Kugongagonga miguu au visigino chini na kutimua vumbi. Katika hali hii ni vyema kuchukua tahadhari dhidi ya Tembo huyo kwani huashiria kutoridhika na hali.
- Tembo huyatanua masikio kuelekea pembeni. Tembo hufanya hivi kuonesha namna gani alivyo mkubwa ili kumtisha adui na kumpa nafasi adui kuchagua kati ya kukimbia au kupambana naye. Ishara hii ni tofauti na tabia ya Tembo ya kugonga masikio kwa ajili ya kuupoza mwili hususani wakati wa joto kali. Katika hali hii masikio huonekana marefu na sio mapana kama ya Tembo mwenye hasira.
- Kutingisha kichwa. Hii ni ishara ya hatari zaidi kwani huonesha utayari wa Tembo kufanya mashambulizi. Kabla Tembo hajamfata adui hutingisha kichwa kwanza na anaweza kufanya hivo mara moja, mbili au tatu.
- Kusimamisha mkia. Hali ya Tembo kuweka mkia usawa wa nyuzi 90⁰, huashiria hali ya hatari. Huna budi kuchukua tahadhari.
- Kutoa mlio mithili ya tarumbeta; sauti hii hutolewa wakati Tembo anafanya au anajiandaa kufanya mashambulizi.
Hii ndio tamati ya makala yetu , Pasi na shaka, umejifunza na kufurahia makala hii. Kwa pamoja tuendelee kujifunza na kufarahia mazingira, Wanyama pori na utalii kupitia makala zetu murua.
Asante Sana kwa kusoma makala zetu.
Makala hii imeandaliwa na Lucia Romward, mhitimu Chuo Kikuu cha Dar es salaam katika fani ya Sayansi ya Uhifadhi wa Viumbe pori, na pia imehaririwa na Alphonce Msigwa, Mwikologia Hifadhi za Taifa Tanzania.
Mawasiliano
Linkedlin; Lucia Levelian Romward
Email; luciaromward@gmail.com ,
Mobile phone +255(0)743927610




We’ll done 👍 bro
Tunashukuru sana Octavian, tuendelee kujifunza na kuwashirikisha wengine mambo haya muhimu. Asante sana kwa feedback.
Shukurani kwa makala nzuri kuhusu mawasiliano ya tembo
Ni makala nzuri sana
Tunashukuru sana Julius, karibu tena kwa makala zaidi za wanyamapori na utalii hapa hapa. Asante sana kwa feedbacks
Ni makala nzuri… Mungu akujalie sana unapokuwa unaendelea kufafanua kwa watu wengi tusiojua mambo mengi zaidi kuhus wanyama pori na tabia zake mbalimbali katika mazingira yao na nje ya mazingra yao.
Tunashukuru sana Fidson, karibu tuendelee kujifunza zaidi kuhusu maliasili na wanyamapori kwa ujumla. Asante sana kwa feedback
Keep on because wildlife issues was being taken as a nonsense matters so we as a youth we have to wakeup and anounce our heritage
Very sure Rhino Fausta, we need at least to raise the awareness concerning our valuable natural resources, because most of Tanzanian don’t know what is going on in our wildlife and other natural resources. So our work is to make this information accessible to them in a very simple language. You are most welcome Fausta and thank you for Feedbacks
Tunashukuru sana kwa kuweza kutujuza na kutugundisha mambo mengi kuhusu wanyamapori hususani kwa Lugha yetu hii inadhihirisha ukomavu wa uzalendo wako pamoja na kutaka jamii yetu izidi kujifunza na kuelewa zaidi tabia za wanyama wetu hii itasaidia sana jamii zetu hasa zinazopakana na hifadhi zetu kujikinga na kuchukua hatua pindi waonapo dalili hizi hatimaye migogoro itapungua .Asante sana na uendelee kutuelimisha
Hakika, sisi kama wahifadhi wenye ujuzi na weledi katika sekta hii tunatakiwa kuyafanya mambo yote muhimu yanayoonekana kuwa magumu yawe rahisi na ujumbe uliokusudiwa kuwafikia walengwa ambao ni watanzania. Hivyo ndio kusudi la blog hii na kuhakikisha tunatoa maarifa na ujuzi wetu katika kutetea na kulinda maliasili zetu adhimu kwa njia hii ya uandishi na kupeana maarifa na ushauri. Nakushukuru sana Mwanga kwa mrejesho huu, naamini hata mwandishi wa makala hii atafarijika na kutenga muda wa kutosha kuandaa makala nyingine bora zaidi kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii yetu. Pamoja sana Mwanga.