Mada; Miongoni mwa rafiki wachache tulionao porini (mbugani) ni pamoja na ndege huyu Mwenzi wa asali, mwenye uwezo mkubwa wa kusikia sauti ya binadamu ikimuita na kuitii.
Habari mpendwa msomaji wetu wa Makala za wanyamapori katika darasa letu huru, ni matumaini yangu unaendelea vyema. Nina kila sababu ya kipekee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na afya njema japokuwa kwa sasa dunia inapitia kipindi kigumu cha gonjwa hili la mapafu linalosababishwa na virusi vya corona (COVID 19), na pia kwa kuiwezesha makala hii kukamilika hatimaye imekufikia mkononi mpendwa msomaji wetu ilitujifunze zaidi kuhusu ndege huyu aitwaye Mwezi wa asali,mahali anapopatikana, uhusiano naye ulianza lini na kwanini upo pia ngazi ya uhifadhi wake, karibu tujifunze…
Utangulizi;
Pamoja na uwezo mkubwa Mwenyezi Mungu aliotujalia wa kufikiria na utimamu mkubwa wa akili bado binadamu tunauwezo mdogo wa kuamini kila kitu, hivyo kumechangia binadamu kuwa na marafiki wachache sana porini (mbugani) hasa kwa hawa viumbe pori. Baadhi ya marafiki hao wachache tulionao ni kama ndege huyu Mwenzi wa asali, Mnandi ambae amekuwa akitumiwa na wavuvi wa asili hasa katika tamaduni za Japani na China ambapo huongozana moja kwa moja mpaka kwenye kina chenye samaki wengi hivyo baada ya kuvua samaki hugawana; na rafiki mwingine tuliye nae ni Panya ambae amekua akisaidia katika kuvumbua mabomu yanayokuwa yamefukiwa chini ya ardhi pia matumizi ya Mbwa maalumu ambao wamekuwa wakitusaidia katika ulinzi.
Tukirudi kwa rafiki yetu huyu mkubwa ndege Mwenzi wa asali, katika upangaji na uchambuzi wa kibiologia wanaelekeana na ndege waimbao (order Passeriforms). Ndege huyu Mwenzi wa asali katika jamii yao wametawanyika sana maeneo ya kitropiki ya bara la Afrika, Asia na Ulaya ikiwa upande wa Afrika tumejaliwa spishi nyingi na spishi mbili tu kuwepo barani Asia. Ndege huyu ana umbile dogo kati ya inchi 4.5-8 lillilopambwa na rangi nyeusi ya kupooza (kupauka) na njano inayongaa sana kwenye bega karibu na mbawa, rangi nyingine nyeupe kwenye mkia wake na rangi ya pinki kwenye midomo yake hii ni kwa spishi zote zinazopatikana barani Afrika.
Asili ya chakula anachotumia;
Ni miongoni mwa jamii chache za ndege wanaokula mara kwa mara kwenye lava wa nyuki na masega ya asali, mara chache kwenye masega yaliyotengenezwa na wadudu wenye magamba, na pia wanakula wadudu warukao na watambaao, buibui na mara chache kwenye matunda ya miti. Uwezo wao wa kula asali umechangiwa na ngozi nene ya miili yao isiyopitisha miiba ya nyuki na pia mfumo wao wa umengejaji ambao upo kwa jamii chache za ndege ambao unaweza kumengenya masega ya asali kutokana na bakteria waliomo ndani yao wasiopatikana kwa ndege wengi.
Uzalianaji wa ndege huyu Mwenzi wa asali;
Ni miongoni mwa ndege wanaotaga kwenye viota vinavyotumika na ndege wa jamii nyingine kabisa hasa viota vya white eyes na warblers, Na viota hivi vingi vipo chini ya ardhi sana sana kwa jamii za ndege wanaokula nyuki. Ndege huyu Mwenzi wa asali hutaga mayai matano kwa kipindi cha siku tano hadi siku saba na ndege huyu jike huhakikisha vifaranga vyake huatamika mwanzoni kwa sababu wanauwezo mkubwa wa kuanza kuyaatamia mayai yao kabla ya kutaga, pia anafahamika kwa kutenga vitoto vya ndege wale walioatamia (ndege wenyeji), ambapo hutenga mayai ya mwenyeji wake na kuyapasua au kuua vifaranga kwa kutumia midomo yao ambayo kwa juu umeumbika kama sindano iliyochongeka mwishoni.
Uhusiano wa ndege huyu Mwenzi wa asali na binadamu pamoja na mnyama Nyegere; ndege huyu amejipatia umaarufu mkubwa juu ya uhusiano mzuri alionao na binadamu hasa kwa hizi spishi mbili za barani Afrika katika kuwaongoza wawindaji wa asali (hasa jamii nyingi za watu wa porini wakiwemo wa Hadzabe-Tanzania na Yao-Msumbiji) kwenye mizinga ya nyuki ambayo ipo sana kwenye miti kama mibuyu na miti mingine mirefu. Ndege hawa wamekuwa wakizitambua sauti za wawindaji hao pindi wanapoitwa na kutii hivyo kuwafikisha sehemu yenye asali na baada ya wawindaji kutoa asali wkenye miti hiyo hulazimika kuwa lava wa nyuki na masega yao ambayo ndege huyu huyatumia kama chakula. Uhusiano huu inaaminika uliana miaka ya 1500 na wengine husadiki ni miaka milioni 1.9 iliyopita.
Si kwa binadamu tu, pia na kwa mnyama nyegere ambae chakula chake kikubwa ni asali hivyo hufuatana na ndege huyu na baada ya kuchukua asali humwachia masega na matoto ya nyuki kama chakula na kudumisah urafiki wao wa kusaidiana kutafuta chakula.
Ngazi ya uhifadhi
Himaya nyingi za ndege huyu zimetawanyika sana katika maeneo mengi tofauti hivyo kumesaidia kutokuwepo katika orodha ya viumbe ambao wapo kwenye mazingira au idadi hatarishi kutoweka duniani (Least Concern). Katika ukubwa wa maeneo ya himaya zao ni kilomita za mraba 20,000 na ukubwa huu umesaidia na kuchangia kwa kiasi kikubwa idadi ya ndege huyu kuzidi kuongezeka.
Kutokuwepo katika orodha ya wanyama walio hatarini kutoweka duniani haina maana hawakutani na changamoto zozote hasa zile zitokanazo na binadamu. Ikumbukwe kuchoma misitu, mikaa, kusafisha mashamba, kubomoa na kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo shorobo za wanyama pori (wildlife corridors), utupaji taka hovyo na mambo mengine mengi yanaharibu makazi ya aina zote za baianua kwa njia moja ama nyingine kama sio kwenye maji basi kupunguza maeneo yenye usalama zaidi kwa makazi ya wanyama au kuchafua hali ya hewa hivyo kuchochea magonjwa yatokanayo na kuenezwa kwa njia ya hewa.
Ni matumaini yangu wasomaji wote wa Makala hizi za wanyama pori ni mabalozi wazuri katika kutunza, kuhifadhi na kutetea viumbe hawa na mwisho kabisa tujitahidi kupandikiza roho za uhifadhi kwa rafiki, ndugu, jamaa na watu wetu wa karibu.
Asanteni sana kwa usomaii wenu wa Makala hizi,
Imeandikwa na;
Leena Lulandala
Mwanafunzi-UDSM
Mawasiliano; lulandalaleena@gmail.com.
Simu: 0755369684.