Idadi kubwa ya viumbe wanaopatikana duniani miili yao imefunikwa na leya nyepesi au nzito iitwayo ngozi, japkuwa kuna viumbe wachache wasio na ngozi. Ngozi ni ganda la nje linalofunika mwili wa mnyama. Wanyama na ndege huwa na aina za ngozi tofautitofauti kulingana na mazingira wanapoishi na ukoo wa spishi mbalimbali za viumbe husika.

Je kuna faida gani ya kuwa ngozi?

  1. Ngozi husaidia   kurekebisha joto mwili la viumbe.
  2. Ngozi hukinga sehemu za mwili dhidi ya athari za nje, hasa vijidudu Vinazoweza kusababisha magonjwa.
  3. Ni kinga dhidi ya kukauka kwa ngozi kwa kutunza maji mwilini
  4. Ngozi huwa na mifumo ya fahamu mingi ambayo inasaidia kutambua mazingira mbalimbali kama vile  baridi, joto, kuguswa, tetemeko n.k.
  5. Huweza kuonyesha hali ya afya na hisia  kwa mnyama mfano kusisimka.
  6. Ngozi hutumika pia kuchukua vitamini D toka kwenye mwanga wa jua ili kutumiwa na mwili

UTENGENEZWAJI WA NGOZI KWA VIUMBE HAI

Ngozi hutengenezwa katika mfumo wa kibaolojia ambao huweza kuainisha ngozi halisi ya kiumbe. Rangi ya ngozi ya  viumbe hutokana na kurithi kutoka kwa wazazi wake baada ya mchanganyiko wa vinasaba kati ya wazazi wawili (crossing over). Yaani mwanamke na mwanaume. Katika utengenezwaji wa ngozi ya kiumbe , kunaweza kutokea hitilafu za vinasaba au vichocheo,(genetics) ambapo huweza kutokea wakati wamchanganyiko wa vinasaba kwa wazazi au kwa kiumbe mwenyewe wakati wa ukuaji.

Athari zake huweza kuwa na historia katika familia husika. Pasipokua na hitilafu katika urithi, kiumbe huzaliwa akiwa na ngozi yake halisi Ila ikitokea hitilafu katika utengenezwaji wa ngozi ya viumbe hupelekea kiumbe kuwa na ngozi isiyo ya kawaida kwa wanyama. Zipo aina kuu mbili za ngozi zisizo za kawaida zinazoweza kumpata kiumbe yeyote ambazo ni;;

  1. Uchache au wingi wa chembechembe zinazochochea utengenezaji wa ngozi za viumbe (Melanism). Yaani kukosekana kwa uwiano wa chembechembe zinazotengeneza ngozi.
  2. Ukosefu wa chembechembe zinazochochea utengenezaji wa ngozi, macho na nywele (Ualbino=Albinism).

Tofauti kati ya Melanism na Albinism

MELANISM

Hii hutokana na kuzidi au kupungua kwa chembeche zinazotengeneza ngozi za wanyama, na huwa na madhara ya nje  yanayo athiri muonekano wa  rangi ya ngozi ya mnyama, lakini macho na nywele au manyoya yanakuwa na muonekano wa kawaida.

Hali hii imeripotiwa sehemu nyingi duniani na imekuwa na madhara si kwa wanyamapori tu, bali hata baadhi ya makundi ya ndege,  viumbe wa majini kama mamba na baadhi ya jamii za nyoka  na kupelekea kupoteza rangi halisi ya ngozi zao. Baadhi ya a wanyama walioathiriwa na hali hii inahusisha simba, nyati , twiga, nyumbu, n.k

Athari katika ngozi za wanyama huweza kutokea katika namna kuu mbili, ambazo ni:

  • Kuzidi kwa chembechembe zinazochochea utengenezwaji wa ngozi za wanyama.
  • Katika kutengenezwa kwa ngozi ya mnyama au ndege husika, vichocheo  vinavyochangia kuundwa kwa ngozi ya mnyama au ndege huweza kuzidi kupita kiasi kinachohitajika. , Hiihuweza kusababisha mnyama au ndege kuwa na rangi iliyoiva sana na wakati mwingine husababisha mnyama kuwa na rangi tofauti na wanyama na ndege wa kundi lake.
  • Kupungua kwa chembechembe zinzochochea kutengenezwa kwa ngozi za wanyama na ndege.

Hii huwa na madhara tofauti kidogo na yanayotokana na kuzidi kwa chembechembe zinazochokea utengenezwaji wa ngozi, kwa kawaida hali hiii hupelekea kiumbe kupoteza  ngozi yake halisi na kufanya awe na ngozi angavu sana na yenye weupe mwingi.

Baadhi ya wanyamamapori kama twiga na pundamilia , hali hii hupelekea kupotea kwa michoro yao ya kupendeza (pattern) katika miili yao au kuwa na hali ya kupauka kutoonekana vizuri kama ilivyo kawaida. Hali hii imeripotowa maeneo mengi duniani ikiwemo Tanzania, katika Hifadhi ya Taifa  ya Tarangire na Katavi. Katika hifadhi ya Tarangire aliwahi kuonekana twiga  mwenye rangi nyeupe na alipewa jina la OMO .

Pichani : Twiga akiwa rangi nyeupe huku miraba yake ikionekana kwa uhafifu.(OMO)

UALBINO

Ualbino  husababishwa na ukosefu wa chembembe za rangi katika ngozi, macho na nywele (manyoya) za wanyama na ndege.

Madhara haya Hutokana na hitilafu katika shanga za urithi na ni tatizo la urithi. Hali hii hutokea kutokana na kuwepo kwa hali hiyo katika familia .Mnyama au ndege mwenye ualbino huwa na rangi nyeupe ya ngozi , nywele na manyoya kwa ndege, pia huwa na macho meupe au bluu na huwa yanapepesuka (blinking of eyes) .Hii hufanya  mnyama kuwa na uoni hafifu (vision), hususani kwa wanyama wawindaji (carnivores) kama simba na wale wanaofanya mawindo usiku kama bundi. Hali ya ualbino imeripotiwa kuathiri wanyamapori kwa asilimia chache na imejitokeza kwa baadhi ya wanyamapori kama simba, twiga, pundamilia, jamii za swala, tembo  n.k

Picha ikionyesha baadhi ya wanyama walioathiriwa na Melanism
Pichani: Pundamilia  mwenye ualbino na macho yake yakionesha kuwa na chembe chembe za rangi ya bluu.

MADHARA WANAYOPATA VIUMBE HAI WENYE UALBINO NA MELANISM.

  1. Huwa na uoni hafifu ambao hupunguza na kuathiri uwezo wa kuwinda na kukwepa maadui.
  2. Wengi huathiriwa na mwanga wa jua na kwa wanyama wenye melanism huathiriwa sana na wingi wa joto kutokana na ngozi zao kushindwa kuakisi joto hilo.
  3. Huwa kwenye hatari ya kutoweka kutokana na kuuawa na wenzao wakiona niwatofauti (hutokea sana kwa mbwa mwitu).
  4. Nirahisi sana kuonekana na adui pamoja na wawindaji haramu kutokana na kuwa na rangi ya kung’aa .
  5. Nirahisi kuathiriwa na uchafuzi wa mazingira na hali ya hewa kupelekea kutoweka kwa mazingira salama kwa ajili ya ukuaji wao.

Kwa kuhitimisha makala hii, ni nadra sana kuwaona wanyama ambao wamekumbana na kadhia hii ya kuwa na ualbino au melanism. Hivyo, wadau mbalimbali wa uhifadhi wanahitaji kuongeza uangalizi pindi inapotokea mnyama ameonekaa kuwa na changamoto hiyo katika mwili wake. Hii ni kutokana na kwamba mnyama mwenye hali huwa ni kivutio kwa wageni wanaofika na kutembea vivutio vyetu vya utalii pia kungeza tafiti mbalimbali zakubaini na kuvumbua uwepo wa wanyamapori  na ndege wenye ualbino na melanism, kusudi kujua idadi na kuweka mikakati ya kuwahifadhi na kuwalinda vyema.

Makala hii imeandikwa na Shoo Marylove Gasper wa Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro na kuhaririwa na Alphonce Msigwa, Mwikolojia wa Hifadhi za Taifa Tanzania

Ahsante sana kwa kusoma makala hii, kwa maswali maoni ushauri na mapendekezo kuhusu makala hii usisite kuwasiliana na mwandishi kwa mawasiliano hapo chini.

Simu:255(0) 783 682 765

email: marylovegasper478@gmail.com