Habari za sasa hivi wapenzi wasomaji wa makala hizi za wanyamapori. Leo nimewaletea mezani Makala inayohusu uhifadhi shirikishi jamii. Makala hii inahusu namna ambavyo wananchi wanashirikishwa katika uhifadhi wa wanyamapori.

NINI MAANA YA UHIFADHI SHIRIKISHI JAMII?

Ni mkakati wa uhifadhi wa mazingira unaozingatia ushirikiano na jamii zinazozunguka katika maeneo ya hifadhi. Mkakati huu unalenga kuwawezesha wananchi mbalimbali wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi katika kushiriki kwenye shughuli mbalimbali zinazohusiana na usimamizi wa wanyamapori na rasilimali mbalimbali zinazopatikana katika maeneo ya hifadhi.

Pia, miradi mbalimbali ya kijamii imeudwa ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusiana na umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali zetu.

Picha hii imetolewa kwenye kurasa ya Liwale district council.

HISTORIA YA UHIFADHI SHIRIKISHI JAMII.

Jitihada za uhifadhi zimebadilika kwa kiasi kikubwa kadri miaka inavyoenda . Hapo mwanzo uhifadhi ulikuwa unatumia mfumo wa njia ya juu hadi chini (top-down system) ambapo maamuzi yote yanayohusiana na uhifadhi yalifanywa na watu wa juu au menejimenti ya sehemu husika.

Uwepo wa uhifadhi shirikishi wa jamii ulianza kupata umaarufu mnamo karne ya ishirini ambapo majaribio ya awali ya njia hii yalianza pale ambapo serikali ilianzisha miradi mbalimbali ili kuwajumuisha jamii katika juhudi za uhifadhi, kuudwa kwa maeneo yaliyosimamiwa na jamii Pamoja na miradi ya uhifadhi iliyoongozwa na jamii katika nchi mbalimbali.

Miradi hii ya kwanza ilibainisha kwamba wenyeji wanaozizunguka hifadhi walikuwa na ufahamu na kuthamini ikolojia ya maeneo yaliyowazunguka.

Mabadiliko katika historia yaliyowahusisha jamii katika shughuli mbalimbali za uhifadhi yalionyesha kwamba njia ya uhifadhi iliyokuwa inatumika zamani haikuwa nzuri na ilisababisha kuleta  matokeo yasiyotarajiwa kama vile kuhamishwa kwa lazima, migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, na ukosefu wa kipato endelevu kwa jamii zinazozunguka hifadhi mbalimbali.

Hii ikapelekea uhifadhi shirikishi jamii kupata kasi kubwa kwani mashirika, serikali na taasisi za kimataifa zilitambua kwamba uhifadhi endelevu hauwezi kufikiwa bila ya kushirikisha jamii za watu wanaozunguka maeneo haya ya hifadhi.

MALENGO YA UHIFADHI SHIRIKISHI JAMII.

Kwa ujumla malengo ya uhifadhi jamii yanalenga kupata usawa kati ya uhifadhi wa rasilimali zetu na maendeleo ya kijamii kwa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.

Mpendwa msomaji wa Makala hii behu sasa tukaone malengo ya uhifadhi shirikishi jamii ni yapi?

  1. Uhifadhi wa mimea, wanyama, ikolojia na makazi ya asilia kwa njia inayozingatia utamaduni na ustawi wa jamii.
  2. Uwezeshaji wa jamii zinazozunguka maeneo mbalimbali ya hifadhi kwa kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali za maamuzi.
  3. Uhifadhi wa maarifa ya asili, mila na desturi ya jamii huku ukihakikisha malengo ya uhifadhi yanatimia.
  4. Kushughulikia migogoro kati ya shughuli za kihifadhi na mahitaji ya maendeleo ya jamii husika
  5. Kuleta hisia, uwajibikaji  na hali ya umiliki kwa jamii kwa kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali toka mwanzo mpaka mwisho wa shughuli hizo.
  6. Kutoa elimu na kuongeza uelewa kwa jamii za wenyeji kuhusu umuhimu wa uhifadhi endelevu kwa manufaa yao na nchi kwa ujumla.
  7. Kuhamasisha sera mbalimbali zinazohusiana na uhifadhi kutambua thamani na umuhimu wa kuwashirikisha jamii katika uhifadhi.

MIFANO YA MIRADI MBALIMBALI INAYOWAHUSISHA JAMII KATIKA UHIIFADHI NCHINI TANZANIA.

Tanzania imeanzisha na kutekeleza miradi mbalimbali ya uhifadhi huku ikishirikisha jamii katika utekelezaji wa miradi hiyo. Ifuatayo ni mifano ya miradi hIyo;

  1. Mradi wa uhifadhi na maendeleo ya Mpingo (MCDI).

MCDI inashirikiana na jamii zilizopo Kusini mwa Tanzania kuhamashisha usimamizi endelevu wa mti wa mpingo (African blackwood) ambao unakabiliwa na hatari ya kutoweka, kwa kutoa mafunzo kwa jamii kuhusiana na mbinu za uvunaji wa mti huu huku wakisaidia jamii mbinu mbalimbali za biashara ya mti huu wa mpingo.

                    Picha hii imetolewa katika ukurasa wa MCDI_tanzania.

  • Mradi wa kuwezesha jamii katika usimamizi shirikishi wa misitu na mabadiliko ya tabia za nchi.

Mradi huu unatolewa na MJUMITA huku lengo likiwa ni kuwasaidia wananchi kwa kutoa mafunzo ya utawala bora wa misitu na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

  • Mradi wa Bonde la Kilombero Wetland.

Mradi huu unahusika na usimamizi wa mazingira ya maji ya bonde la Kilombero kwa kuwahusisha jamii wenyeji katika kusimamia mazingira haya ya maji kwani jamii pia inatumia maji haya kwa kilimo Pamoja na matumizi mbalimbali ya kila siku.

  • Mamlaka ya Eneo la Uhifadhi la Ngorongoro (NCAA).

Eneo la uhifadhi wa Ngorongoro, Eneo la Urithi wa Dunia la UNESCO, Jamii za wamasai wanaishi ndani ya eneo hili na kushiriki katika Jitihada za uhifadhi kwa kufanya matumizi endelevu ya ardhi, miradi ya maendeleo ya jamii utalii na ulinzi wa wanyamapori.

ikolojia ya eneo hilo.

Picha hii imetolewa katika tovuti ya oaklandinstitute.org

Mradi wa kuboresha usimamizi wa mariasili na kukuza utalii kusini mwa Tanzania (REGROW).

Mradi huu unatekelezwa katika hifadhi za Nyerere, Ruaha, Mikumi na Milima ya Udzugwa  Pamoja na maeneo mengine yenye vivutio vya utalii Kusini mwa Tanzania, kwa kutoa mafunzo ya usimamizi wa wanyamapori na utalii Pamoja na kufadhili masomo wanafunzi Zaidi ya 476 kutoka vijiji vilivyo Jirani na hifadhi.

Kwa ujumla hiyo ni mifano tu ya miradi mbalimbali inayohusisha jamii katika uhifadhi.

FAIDA ZA UHIFADHI SHIRIKISHI JAMII KWA WENYEJI.

  • Kuboresha kipato cha kimaisha.

 Kushirikishwa kwa jamii katika shughuli mbalimbali za uhifadhi kumepelekea kipato cha          wenyeji wengi kuwa bora kwani mara nyingi wanapata fursa mbalimbali na endelevu za kipato    mfano utalii,uvunaji wa rasilimali ambapo inawasaidia jamii kuboresha kipato chao na Maisha yao kwa ujumla.

  • Uhifadhi wa tamaduni ,mila na desturi za jamii za wenyeji

Uhifadhi shirikishi jamii unatambua na kuthamini mira na desturi za jadi ya jamii husika na maarifa ya jadi ya jamii hizo hivyo husaidia sana kuhifadhi utamaduni na jadi za wenyeji.

  • Usimamizi wa rasilimali

Jamii zinazoishi karibu na hifadhi hupewa elimu mbalimbali kuhusiana na usimamizi wa rasilimali hivyo jamii inakuwa na

uelewa wa usimamizi wa rasilimali mbalimbali.

  • Kuboresha miundombinu.

Jamii mbalimbali zimenufaika uhifadhi shirikishi kwa kuboreshewa miundombinu kama vile ujenzi wa shule, vituo vya afya , huduma za maji na barabara.

Picha hii imetolewa katika ukurasa wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro.

  • Ajira

Watu mbalimbali waishio Jirani na hifadhi wamekuwa wakipata ajira mbalimbali katika shughuli za uhifadhi kama vile kubeba mizigo ya watalii, ulinzi na ufanya usafi katika

maeneo ya hifadhi hii yote ni kwa sababu jamii inashirikishwa katika shughuli mbalimbali za uhifadhi

       Picha hii imetolewa katika tovuti ya zoologische Gesellschaft

FAIDA ZA UHIFADHI SHIRIKISHI KWA MAMLAKA YA USIMAMIZI WA HIFADHI.

  • Kuboresha ufuatiliaji.

Kushirikisha jamii katika uhifadhi kunaisaidia kuboresha ufuatiliaji wa shughuli mbalimbali  na mipango mbalimbali iliyowekwa .

Picha hii imetolewa katika ukurasa wa single news

  • Kupunguza migogoro.

Kuwashirikisha jamii katika kufanya maamuzi kunasaidia sana kupunguza migogoro kwani husababisha wananchi kuwa na hisia za umiliki wa shughuli au mipango mbalimbali iliyowekwa hivyo kupunguza sana migogoro kutoka kwa wananchi.

  • Upatikanaji wa maarifa ya jadi.

Wanajamii husika wana maarifa mbalimbali kuhusiana na ikolojia ya eneo hilo hivyo kushirikisha jamii itasaidia sana kupata maarifa mbalimbali ya jadi ambayo ni muhimu katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuhufadhi.

Picha hii imetolewa katika ukurasa wa Daily news

  • Kupunguza ujangili.

Mara nyingi majangili huwa ni watu wanaotoka katika jamii inayozunguka maeneo ya hifadhi hivyo kushirikisha jamii itasaidia kupambana na kutoa taarifa kuhusiana na majangili na sehemu wanapopatikanaa.

CHANGAMOTO ZA UHIFADHI SHIRIKISHI JAMII.

Uhifadhi shirikishi jamii unakabiriwa na changamoto zifuatazo

  1. Migogoro ya rasilimali

Kupatanisha mahitaji ya wananchi na uhifadhi  kunaweza kuleta migogoro kuhusiana na matumizi ya rasilimali kama maji, ardhi na maeneo ya marisho.

  • Upungufu wa rasilimali

Kushirikisha jamii katika uhifadhi kunahitaji rasilimali fedha ili kuweza kuendesha shughuli mbalimbali lakini mara nyingi huwa kuna upungufu wa fedha hivyo inazuia utekelezaji mahsusi wa shughuli mbalimbali za kihifadhi na kijamiii

  • Mabadiliko ya mira, desturi ,na tamaduni

Mabadiliko ya mitindo ya Maisha yanasababisha kupungua kwa maarifa ya jadi yanayohusiana na uhifadhi hivyo kuharibu uwezo wa jamii kusimamia rasilimali

  • Migogoro ya kisiasa

Migogogro ya kisiasa na mabadiliko ya utawala yanasababisha kushindwa kufikia malengo ya uhifadhi shirikishi jamii kwani kunaweza kuvuruga mipango ya uhifadhi shirikishi jamii.

  • Ongezeko la idadi ya watu

Kumekuwa na tatizo la idadi wa watu kuongezeka mara dufu katika maeneo

mbalimbali ya Jirani na hifadhi hiyo kupelekea ukosefu wa rasilimali katika maeneo yao na kusababisha kuwe na shinikizo la kuingia katika hifadhi na kutumia rasilimali zilizo ndani ya hifadhi ambapo inahatarisha jitihada za uhifadhi.

MAPENDEKEZO.

Mapendekezo yangu kuhusiana na uhifadhi shirikishi jamii ni kwamba

  • jamii ishirikishwe katika kila hatua ya maamuzi ili kuhakikisha wanatoa mchango wao.
  • Kutoa mafunzo,

uwezo na misaada mbalimbali kwa jamii ili kuimarisha ujuzi na uwezo wa jamii

  • Wanajamii washiriki kikamilifu katika kushirikina na mamlaka ya hifadhi mbalimbali ili kuhakikisha tunalinda na kutunza hifadhi zetu kwa manufaa ya sasa na ya baadae.

HITIMISHO.

Kwa kumalizia uhifadhi shirikishi jamii ni mkakati mzuri na mahsusi kuhakikisha jamii inafanikiwa na pia uhifadhi unaendelea .Makala hii imechunguza malengo, faida na changamoto za uhifadhi shirikishi jamii .Jamii mbalimbali zinazoishi karibu na hifadhi zinaweza kunufaika maradufu na mkakati huu ikiwa watakuwa wako tayari kushirikina na mamlaka husika kuweza Kulinda na kusimamia rasilimali zetu .Kwa hiyo ni wakati wa kuongeza juhudi na kupaza sauti kuhusiana na uhifadhi shirikishi jamii ili kuweza kuongeza mifano bora ya uhifadhi shirikishi jamii na kulinda hazina ya asili kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Ikumbukwe¸ UMOJA HUZAA ULINZI.

MONICA C. MAHILANE

mahilanemonica49@gmail.com

0652267935