Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Baadaye Mungu aliendelea kuumba vitu vingine ikiwemo wanyama wa mwituni kwa jinsi yake na wanyama wa kufugwa kwa jinsi yake. Baada ya uumbaji wa vitu vyote kukamilika mwadadamu ndiye aliyefuata kwa uumbaji. Na mojawapo ya majukumu ya msingi na ya mwanzo kabisa aliyopewa mwanadamu ni kutawala, kulinda na kutunza uumbaji wa Mungu hapa duniani.

Mwanadamu alipewa utawala na usimamizi wa uumbaji wa Mungu. Kitendo hiki alichokifanya Mwenyezi Mungu cha kumpa mwanadamu jukumu la kusimamia vitu alivyoumba inaonyesha ni kwa kiasi gani Mungu anataka vitu vyake alivyoviumba viendelee kuwepo hapa duniani na kustawi kwa wingi. Kwa namna nyingine Mungu hapendi kusikia au kuona wanyama, mimea, ndege, wadudu na vyote alivyoviumba vinatoweka katika uso wa dunia kwasababu yoyote ile.

Kwahiyo, tunaweza kusema Mungu ndiye mhifadhi namba moja, na kwasababu hiyo Mungu aliamua kutupa moja wapo ya sifa ya uungu ambayo ni uhifadhi. Hivyo ndugu, jua kuwa uhifadhi wa mali na uumbaji wa Mungu ni sifa njema na ni jambo ambalo Mungu mwenyewe analifurahia. Napenda ujue kuwa uliumbwa kuwa mhifadhi na mahali popote ulipo hakikisha unasimamia uhai wa viumbe wengine, hiyo ndio kazi kuu tuliyopewa na Mungu.

Jukumu la uhifadhi ni jukumu takatifu, maana limeasisiwa na Mungu mwenyewe. Pia napenda ujue kuwa kwa namna ambavyo Mungu alivyoiumba dunia na vitu vyote, tunategemeana sana katika kuishi. Ndio maana maamuzi yote ya kifo na uzima hapa duniani yapo mikononi mwa binadamu. Yani Mungu ametupa mfumo wa maisha ya hapa duniani ili tuuendeshi sisi, na Mungu anafurahi kuona tunauendesha kwa mafanikio. Mfano, kama tutaamua kutunza mazingira, mazingira yatatutunza, kama tutayaharibu mazingira maisha yetu yataharibika pia. Kama tunataka uhai tuendelee kutunza uhai wa viumbe wengine.

Lakini kwa hapa tulikofikia kila moja wetu anafahamu, sidhani kama Mungu anafurahia, tumeharibu uzuri na uumbaji wa Mungu kwa kaisi kikubwa. Mungu aliiumba dunia kuwa ndio sehemu salama na inayotufaa sisi binadamu kuishi na sio sehemu nyingine. Inasikitisha sana kuona tulivyoiharibu dunia mpaka tunafikia hataua tunatafuta maisha kwenye sayari nyingine. Kama inavyoendelea kwa nchi za Magharibi, wanatafuta sehemu nyingine za kuishi tofauti na duniani, wanatumia mabilioni ya dola kuwekeza na kutafuta makazi mengine nje ya dunia hii.

https://greenliving.lovetoknow.com/image/225070~Environmental-Pollution-Concept.jpg

Hali tuliyonayo inafikirisha na kusikitisha, hao wanaofanya uwekezaji kwenye sayari nyingine inawezekana kuna kitu wamekiona hapa duniani, wameona mwenendo wa dunia na mifumo ya maisha ya binadamu hatufiki mbali, ndio maana wanaamua kutafuta maisha sehemu nyinyingine tofauti na duniani. Siandiki haya ili kuponda juhudi zao, la hasha! bali naandika haya ili tubadili mfumo wetu wa maisha uwe rafiki kwa mazingira yanayotuzunguka.

Mifano ipo mingi sana inayoonyesha namna tulivyochoka, tulivyoharibu na tunavyoendelea kuharibu mazingira asilia. Kama wengi tunavyoona majanga ya njaa, mabadiliko ya hali ya hewa, mafuriko, ukame na ongezeko la jangwa, magojwa na kushamiri kwa vitendo vingi vya uvunjaji wa sharia kama vile biashara haramu za wanadamu, wanyamapori, mimea nk. Matokeo haya ni ishara kuwa tumeharibu mazingira, tumewaua viumbe waliokuwa wanayatunza mazingira hayo. Majanga haya yanachangia sana kufupisha maisha yetu hapa duniani.

Tafiti kutoka ripoti maalumu ya umoja wa mataifa (World Wildlife Crime, 2020) inaonyesha hali ya hatari zaidi kwa binadamu na viumbe hai wengine. Kwa miongo kadhaa tuliyoishi hapa duniani, tumeshughudia maafa mengi sana kwa wanyamapori ambayo yameleta athari za moja kwa moja kwa binadamu. Mfano karibia robotatu ya magonjwa yote yanayoambukiza “zoonotic” kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu yamechangiwa sana na uharibifu wa mazingira.

Ripoti hii imetaja kuwa kuna muunganiko mkubwa sana kati ya biashara haramu za wanyamapori na hali za hatari za kiafya. Uharamia na ujangili wa wanyamapori umechochoea sana kusambaa na kuibuka kwa magonjwa ya kutisha, hata COVID-19 imetajwa kuwa ni matokeo ya biashara hizi haramu za wanyamapori.

Biahara ya wanyampori imetwajwa kuwa ni miongoni mwa biashara kubwa haramu hapa duniani baada ya silaha na madawa ya kulevya ikihusisha usafirishaji wa nyara na wanyamapori kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine. Inakadiriwa zaidi ya spishi 6,000 za mimea na wanyama zilikamatwa kati ya mwaka 1999 hadi 2018. Karibia kila nchi hapa duniani ikihusishwa katika biashara haramu za wanyamapori.

Baadhi ya wanyamapori wametajwa sana kuhusishwa na biashara hizi haramu, mfano tembo na mengo ya tembo, faru na pembe zake, kakakuona, simba na nyara zake na aina nyingi za mimea kama rosewood imetajwa sana kama ndio bidhaa zinazosafirishwa kwa kiasi kikubwa kwa njia haramu.

Licha ya kuwepo kwa biashara halali za wanyamapori na nyara zake, bado tunashughudia usimamizi usioridhisha katika maliasili hizi, maeneo mengi ya ukaguzi na maeneo mengi ambapo nyara hizi za wanyamapori hutolewa, rushwa na udanganyifu umetajwa kuwa ndio chanzo cha kushamiri kwa vitendo hivi vya kihalifu dhidi ya wanyamapori na mimea asilia.

Kwasababu jambo hili limeshakuwa la kimataifa, utekelezaji wake unahitaji ushirikiano wa kila taifa kuwa sehemu uhimu ya kupambana na uhalifu huu. Juhudi za makusudi zinahitajika kwa ngazi zote, kwa kila mmoja wetu kusima imara mahali popote alipo katika kona ya dunia hii kulinda na kusimamia uhifadhi endelevu wa maliasili hizi tulizopewa na Mungu kusimamia.

Ndugu msomaji wa makala hii, napenda ujue kuwa uhifadhi ndio jukumu lako la msingi hapa duniani. Endapo tutatunza na kuyalinda mazingira yetu ipasavyo, sio tu tutakuwa tumetimiza amri ya Mungu hapa duniani, bali tutakuwa tumeifanya dunia kuendelea kuwa sehemu salama zaidi kuishi.

Makala haya imeandikwa na

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com